NA MWANDISHI WETU
SABUNI ya Unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha
lakini imeuzwa kwa njia ya mnada na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) siyo
salama hivyo haifai kutumiwa.
Tahadhari hiyo imetolewa jana na afisa mwandamizi wa
Shirika la Viwango (TBS), jina lake tunalihifadhi wakati akizungumza na
TANZANIA PANORAMA kuhusu madhara yanayoweza kuwapata watu watakaotumia bidhaa
hiyo.
Akijibu hilo, amesema ni kosa kuuza au kusambaza
bidhaa ambayo muda wake wa matumizi umeisha na siyo salama kuitumia ingawa
matatizo ya kiafya yanayoweza kumpata mtumiaji ni suala la kitabibu na
inategemea kemikali zilizotumika kuitengeneza.
"Matatizo ya kiafya ni suala la kitabibu na
inategemea kemikali gani kwa sababu sabuni zinatofautiana 'composition' ya
kemikali lakini itoshe tu kusema tu bidhaa yoyote iliyo'expire' haifai na siyo
salama kwa matumizi na anayeuza hatendi haki," alisema afisa huyo.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo alipoulizwa
kuhusu suala hilo alisema wanaoweza kulizungumzia ni TBS.
Mapema mwezi huu TRA imeuza kwa njia ya mnada
shehena ya sabuni ya unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha.
Shehena hiyo ya sabuni isiyofaa kutumika baada ya
muda wake kuisha iliingizwa nchini kutoka nje na kukaa bandarini bila kulipiwa
ushuru kwa muda mrefu kabla TRA haijaamua kuiuza.
Habari za uhakika zilizokusanywa na TANZANIA
PANORAMA zimeonyesha kuwa shehena hiyo ni ya mifuko 1,800' ya sabuni ya unga
aina ya AKO na imeuzwa kwa njia ya mnada na maafisa wa TRA huku wakijua kuwa
wanatenda kosa linaloweza kuwa na athari mbaya kwa watakaoitumia sabuni hiyo.
Thamani ya sabuni hiyo ni sh milioni 300 na kabla ya
kunadiwa ilikuwa imehifadhiwa katika bandari kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo alithibitisha kuuzwa kwa shehena hiyo ingawa kabla ya kuthibitisha
alikanusha na kutaka atumiwe ushahidi.
Katika majibu yake, Kayombo alisema "Sasa bwana
ni hivi. Ni kweli huo mzigo unaousema ni kweli ulikuwepo TRA. Ni kweli kabisa.
Na mnada wake wa kwanza ulikuwa Agosti 24, 2020 lakini aliyeshinda hakuja
kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndiyo ukauzika
" Ni kama kulikuwa na pande mbili zilizokuwa
zikiushindania kwa sababu yule mnunuzi wa kwanza hakuja kulipa hivyo ikabidi
ufanyike mnada mwingine ndipo shehena ile ikachukuliwa kwa sh. milioni
21.5."

Johnmbot
ReplyDelete