NA PIUS NTIGA, SIHA
ZAIDI ya ajira 2,000 zimepatikana Wilaya ya Siha
mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha miaka mitano.
Nyingi kati ya ajira hizo zinahusisha miradi
mbalimbali ukiwemo mradi mkubwa wa Shamba la Mwekezaji la Maparachichi
unaojulikana kwa jina la Africado ambalo limetoa nafasi za kazi kwa wananchi
wengi wilayani Siha.
Sambamba na mradi huo mkubwa wa Africado uliopo
Kijiji cha Kifufu, mradi mwingine mkubwa ulitoa ajira nyingi kwa wananchi wa
Siha ni shamba la uzalishaji Mayai ya kisasa lenye ukubwa wa hekari 507
lililopo Kijiji cha Namwai ambalo mwekezaji wake ni Irvine Family. Miradi hii
imezalisha ajira zaidi ya 700 Kati ya 2,000 za wananchi kuanzia mwaka 2015 hadi
2020.
Akizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM ikilenga
kuainisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John
Magufuli,
Meneja Utawala wa Shamba la Africado, Berinda Meena
amesema shamba hilo limesaidia kupatikana kwa ajira 500 za wananchi wa Siha
zilizowawezesha kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.
Amesema mbali ya kufanisha utoaji wa ajira kwa mamia
ya wananchi wa Siha, shamba hilo la Africado lenye uwekezaji wa mabilioni ya
shilingi linawasaidia wafanyakazi wake kuwajengewa uwezo wa ujuzi wa kilimo kwa
kufunga vikonyo, ambapo sehemu kubwa ya wafanyakazi wana mashamba yao
binasfi.
Meena amesema wafanyakazi pia wanapatiwa pembejeo
bure na mwekezaji na mazao yao wanayauza kwa mwekezaji - Africado lengo likiwa
kuwawezesha kuwa na soko la uhakika.
po Mwekezaji wake ni James Pasoz raia wa Ujerumani.
"Tangu Mwekezaji huyu, James Pasoz ambaye ni
raia wa Ujerumani awekeze katika shamba hili sasa yapata miaka 10 anazalisha
maparachichi na kuyauza Ulaya na Uarabuni.
"Mwaka huu zaidi ya tani 3,600 zimezalishwa
katika shamba hili na kuuzwa nje ya nchi.
'Maandalizi ya shamba la Maparachichi ni miaka
mitatu kuanzia hatua ya kupanda miche hadi kuvuna kwa kutumia mbegu ya hasi
inayokuwa haraka" alisema Meena.
Aidha, amesema serikali imekuwa ikitoa kipaumbele
kwa kutoa leseni kupitia EPZ na msamaha wa kodi na kuwezesha eneo kubwa kwa
kuweka mtaji mkubwa na hivyo ameipongeza serikali kwa kusamehe kodi ya ongezeko
la thamani (VAT) kwa vitu ambavyo mwekezaji ananunua kwa ajili ya shamba hilo.
Meena alisifu uhusiano mzuri baina ya mwekezaji na
serikali ambao umewezesha shughuli za uzalishaji kuwa kutokwama.
"Mazingira ya uwekezaji sasa ni mazuri kwa
kiasi kikubwa, yamekuwa mazingira yanayosaidia kampuni kukuwa kwa kiasi
kikubwa.
"Kwa sababu ya kuwepo mazingira mazuri ya
uwekezaji, mwekezaji sasa anatafuta maeneo mengine ya kuwekeza zaidi wilayani
Siha.
"Shamba hilo limekuwa na msaada mkubwa kwani
kipato kinachopatikana kimekuwa kikisaidia kukuza uchumi wa wananchi
pamoja na kujenga shule ya msingi Karagoha na kutoa kampeni ya matibabu bure ya
macho," amesema Meena.
Wakati huo huo, Meneja Mwendeshaji wa Shamba la Mayai
ya Kisasa la Joseph Kasegama, amesema shamba hilo limeondoa upungufu wa
upatikanaji wa vifaranga vya Kuku na limesaidia upatikanaji wa ajira 120 kwa
wananchi wa Siha na kuongeza pia mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha.
"Shamba hilo la Irvine Family lenye hekari 507
lina Mabanda 507 yenye uwezo wa kuchukua kuku 9,000," amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu
ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa kupeleka kiasi
kikubwa cha fedha za maendeleo katika wilaya hiyo ambazo zimewezesha kukarabati
pia Hospitali ya Wilaya ya Siha.
"Tumepata fedha, fedha hizo zimesaidia
kukabarati Hospitali ya Kibong'oto inayotibu wagonjwa wa Kifua Kikuu
(TB), shilingi bilioni saba zimepelekwa pale huku Hospitali ya Wilaya ya Siha
ikipokea shilingi bilioni mbili zilizofanya ukarabati mkubwa," alisema.
Aidha, amesema zaidi ya shilingi bilioni 50
zimetumika kujenga barabara za lami wilayani humo sanjari na kurahisisha
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
"Mpango wa elimu bure umesaidia kuongeza idadi
ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi na sekondari wakiwemo jamii ya
wamasai.
"Ni kwamba ukanda wa Kasikazini haujasaulika ni
tofauti kabisa na ambavyo imekuwa ikisemwa kuwa ukanda huu umesahaurika kitu
ambacho sio kweli," anasema Buswelu ambaye kauli yake inaungwa mkono
Katibu Tawala wa Wilaya, Joseph Mabiti.
Kuhusu uhusiano na wawekezaji amesema ni mzuri na
hivyo kuwataka watu kupuuza kauli zinazotolewa kuwa hakuna uhusiano mzuri baina
ya serikali na wawekezaji.
Akizungumzia Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea,
Buswelu, amewataka wanasiasa kunadi sera zao kwa utulivu na kuache
mihemuko.
Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutekeleza haki
yao ya msingi kwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu wakachague viongozi
watakaowaletea maendeleo ya haraka.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya
ya Siha, Dk. Andrew Method, amesema hivi karibuni mashine ya X-ray itafungwa na
hivyo kupunguza changamoto ya wanachi kwenda kutafuta huduma ya vipimo KCMC
pamoja na Hospitali ya Mawenzi ya Mjini Moshi.
Aidha Hospitali hiyo ndani ya wiki chache zijazo
majengo ya huduma na mama na mtoto yataanza kutumika, ambapo katika Hospitali
hiyo vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua hadi kifo kimoja kwa mwaka.
Aidha, Dk Method amesema hospitali hiyo itakuwa na
uwezo wa kuwa na jengo la kisasa la kuhifadhi miili 20 ya marehemu kwa wakati
mmoja.
Pia amesema ndani ya miezi mitatu ijayo Hospitali
hiyo ya Siha itapokea kiasi kikubwa cha dawa ambacho kitatoshereza hospitali
hiyo na hata kuzidawa katika vituo vingine vya Afya nje ya Wilaya hiyo.
Nao wananchi pamoja na watumishi wa Hospitali ya
Wilaya ya Siha, wamepongeza uboreshaji wa Hospitali hiyo ambayo inatoa huduma
kubwa za kibingwa ambazo walikuwa wakizipata nje ya Wilaya hiyo ya Siha.
Mwisho
No comments:
Post a Comment