NA MWANDISHI WETU
STEPHEN Wassira, Waziri Mstaafu wa Serikali ya Awamu
ya Nne, amewaomba wananchi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara kukipigia kura
Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 kwa sababu
kina ilani makini ya uchaguzi.
Wassira ameyasema hayo Septemba 21, 2020 katika
mkutano wa kampeni wa CCM ulioongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu Taifa ya CCM na pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika uwanja wa Shule ya
Sekondari Mara uliopo Kata ya Nyamatare, Wilaya ya Musoma.
"Tukisema mkapige kura, nendeni mkapige kura
kwa wagombea na vyama vyenye ilani ya uchaguzi. Siyo kukipigia kura chama ili
mradi ni safari tu ya kwenda kupiga kura. CCM inazo sera zake na ndiyo maana
tunawaomba muwapigie kura wagombea wa CCM.
" Hatuwezi kumpa mtu kura za urais kwa sababu
tu tumekutana njiani. Rais ni mkuu wa nchi, mkuu wa serikali na mkuu wa
majeshi. Tunamuombea kura Rais Magufuli kwa sababu amejaribiwa na
ameweza," alisema Wassira.
Alisema Rais Magufuli amefanya kazi kubwa mkoani
Mara, mojawapo ni kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa katika kipindi cha
miaka mitatu, ujenzi ambao ulisimama kwa zaidi ya miaka 40.
Wassira alisema uamuzi wa kujenga hospitali hiyo
ulipitishwa kwa azimio la Chama Cha TANU la mwaka 1974 ambalo lilithibitishwa
na mkutano Mkuu wa TANU mwaka huo huo .
"Hapakuwa na bajeti ya ujenzi lilikuwa ni suala
la kujitegemea kwa hiyo tulianza na michango ya soda ndiyo maana ujenzi wake
umechukua muda mrefu kukamilika," alisema Wassira.
No comments:
Post a Comment