Kayanga ni miongoni mwa miji 28
iliyonufaika na sh. tril. 1.2 za miradi hiyo
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa amesema Serikali imetekeleza miradi
ya maji 1,423 ikiwemo mradi wa kupeleka maji kwenye miji 28 inayotekelezwa kwa
sh. trilioni 1.2.
“Kayanga imepata sh. bilioni 58, ni miongoni mwa
miji 28 iliyopata fedha za mradi wa maji kitaifa ambao unajumuisha mikoa
mingi,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 29, 2020)
wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Kayanga, katika mikutano uliofanyika
kwenye uwanja wa Changarawe, wilayani Karagwe, mkoani Kagera.
Mikoa inayohusika na mradi huo miji yake kwenye
mabano ni Tanga (Handeni/Korogwe, Muheza na Pangani); Njombe (Njombe,
Wanging’ombe na Makambako); Kagera (Kayanga); Mtwara (Nanyumbu na Makonde) na
Singida (Manyoni).
Pia Ruvuma (Songea); Tabora (Sikonge,
Urambo-Kaliua); Mbeya (Rujewa na Chunya); Kigoma (Kasulu); Lindi (Kilwa
Masoko); Mara (Mugumu, Rorya/Tarime); Geita (Geita na Chato); Singida (Singida
Mjini na Kiomboi); Katavi (Mpanda); Dodoma (Chamwino na Chemba); Iringa (Mafinga);
na Morogoro (Ifakara).
Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura
mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi
mgombea ubunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, mgombea udiwani wa Kata
ya Kayanga, na wagombea wa CCM wa kata za wilaya hiyo.
Amesema miradi mingine ya maji inayotekelezwa kwenye
wilaya hiyo imetumia sh. bilioni 5.2 kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya
maji. Ameitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa maji Kijiji cha
Nyaishozi ambao umetumia sh. milioni 706, umekamilika na unatoa huduma.
“Shilingi bilioni 1.6 zilitumika kwa ujenzi wa mradi
wa maji Kijiji cha Chamchuzi, mradi umekamilika na unatoa huduma, shilingi
milioni 805 zilitumika kwa ujenzi wa mradi wa maji Chanika, mradi umekamilika
na unatoa huduma," amesema.
Amesema sh. milioni 63 zilitumika kwa uchimbaji
wa visima vinne na ufungaji wa pampu katika vijiji vya Okakajinja na
Chonyonyo, mradi ambao umekamilika na unatoa huduma.
Amesema fedha nyingine zilizotumika ni sh. milioni
120 kwa ajili ya mradi wa maji uchimbaji wa visima vinne na
ufungaji wa pampu katika vijiji vya Mulamba na Nyarugando, ambao pia
umekamilika na unatoa huduma.
Amesema sh. bilioni 2.4 zilitumika kwa ajili
ya mradi wa maji Nyakakika, ambao uko katika hatua za
umaliziaji na sh. milioni 251 zilitumika kwa ajili ya mradi wa maji
Rugu, ambao nao upo kwenye hatua za majaribio.
No comments:
Post a Comment