banner

Saturday, September 12, 2020

CHADEMA yashtusha kwa uongo




NA CHARLES MULLINDA

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeleeza kushtushwa na kusikitishwa na taarifa ya uongo iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tumaini Makene inayoeleza kuwa ratiba ya kampeni za chama hicho imevurugika baada kuzuiwa kutumia Helikopta.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 10 na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, hakukuwa na mpango wowote wa safari uliotolewa taarifa na mtoa huduma kwa mamlaka hiyo, hivyo safari hiyo haikupangwa wala haikuwa kwenye orodha.

Alisema TCAA imeshtushwa na taarifa iliyotolewa na Makene na kusambazwa katika mitandao ya kijamii ikieleza kuwa mikutano mitano ya kampeni za mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu iliyopangwa kufanyika Septemba 10 mkoani Pwani Imevurugika baada ya Helikopta aliyopanga kuitumia kunyimwa Kibali.

" Ukweli ni kwamba Helikopta ya Kampuni ya State Aviation iliyokuwa itumiwe na mgombea na urais wa Chadema imepewa kibali cha muda mrefu na TCAA kwa shughuli za kampeni za uchaguzi mkuu kuanzia Septemba 4, 2020 hadi Oktoba 31.

"Vibali hivi hutolewa kwa watoa huduma ili kuepuka kuomba vibali mara kwa mara wnapopata wateja.



"Mnamo tarehe 9, Septemba 2020, Kampuni ya State Aviation iliomba kibali cha msamaha ili iweze kumtuma rubani mwenye umri zaidi ya miaka 65 ambao ni wa juu kwa mujibu wa sheria za usafiri wa anga kupitia kanuni ya 15 ya kanuni za utoaji wa leseni za watalaamu wa usafiri wa anga ya mwaka 2017.

"Msamaha huo ulikuwa unaombwa kwa ajili ya kampuni hiyo kutoa huduma kwa wateja wake (Chadema) kwa safari iliyopangwa kufanyika tarehe 10 Septemba. 2020." Inasomeka taarifa hiyo.

Aidha, Johari alikanusha kuhusu kuwepo ofisa yoyote wa TCAA a!iyetoa taarifa kwa msafara wa Lissu juu ya kutofanyika kwa safari hiyo kwa sababu taarifa za aina hiyo huwahusu mtoa huduma mteja wake.

Anasisitiza kuwa hakukuwa na Mpango wowote wa safari uliowalisilishwa na mtoa huduma kwa TCAA kwa mujibu wa sheria.

 

No comments:

Post a Comment