NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetumia shilingi bilioni 3.29 kukarabati
na kugharamia shughuli za utawala, michezo, mitihani na posho kwa maafisa elimu
kata na walimu wakuu kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2019/2020.
Fedha hizo zimetolewa na serikali kupitia mpango wa
elimu bila malipo unaotekelezwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ambao
hadi sasa umezinufaisha pia shule za sekondari 23.
Hayo yameelezwa jana na Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) katika majukwaa ya kisiasa wilayani Ukerewe ambako amefika
akiwa katika mfululizo wa ziara zake nchi nzima za kumnadi mgombea urais wa
CCM, Rais John Magufuli.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema katika utekelezaji wa
mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa lipa kutokana matokeo (EP4R)
ulioanza kutekelezwa 2015 hadi 2020, sh milioni 309 zilitolewa kwa ajili ya
kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na ofisi kwa shule
mbalimbali zikiwemo Kalandero, Murutunguru na Kakerege.
Alisema kiasi kingine cha sh milioni 873 zilitolewa
kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule za
sekondari mbalimbali nchini zikiwemo Bukongo, Pius Msekwa, Bwisya, Muruti na
Lugongo.
Ziara hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa ilimfikisha
katika Kisiwa cha Bwisya kilichoko Kisiwa cha Ukara ambako alitembelea Kituo
cha Afya cha Bwisya na kukagua wodi ya wanaume na ya Wazazi.
No comments:
Post a Comment