NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha
Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema serikali imedhamiria kuhakikisha
kilimo kinamnufaisha mkulima wa Tanzania.
"Watu wasije kuwadanganya kwamba serikali
haiwajali, siyo kweli. Kuna sababu zilizochangia kuyumba kwa bei ya kahawa
kwenye soko la dunia."
Ametoa kauli hiyo leo mchana alipokuwa
akizungumza na wakazi wa Rubale Latina mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya
shule ya msingi Rubale, wilayani Bukoba, mkoani Kagera.
"Serikali ya awamu ya tano ilipoingia
madarakani, iliazimia kufufua mazao matano ya kimkakati ambayo ni kahawa,
pamba, korosho, chai na tumbaku. Mazao haya bei ilishuka na si katika zao la
kahawa tu.
"Kuyumba kwa bei haikuwa katika zao la kahawa
tu bali katika mazao mengine kama pamba na korosho. Kahawa bei yake
iliathirika kwa sababu ya ugonjwa wa Corona. Korosho bei ilishuka kutoka
sh.3,300 hadi sh. 1,900. Pamba pia ilishuka bei," amesema.
Amesema Kenya ndiko mnada wa kahawa huwa unafanyika
lakini hadi sasa bado wanasumbuliwa na ugonjwa wa Corona kwa hiyo haikuwa
rahisi kufanya biashara katika kipindi chote hicho.
Majaliwa ambaye ameanza ziara katika Mkoa wa Kagera
kumuombea kura mgombea irais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli
ametumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Jason
Rweikiza, mgombea udiwani wa kata ya Rubale, Rwegasira Renatus Rwechungura na
madiwani wengine wa jimbo hilo.
Kuhusu maji, amesema sh. bilioni 4.09 zilitolewa ili
kuboresha miradi ya maji katika vijiji kadhaa ambayo yote imekamilika.
Almevitaja vijiji hivyo kuwa ni Ibwera, Kasharu, Kitahya, Katale,
Itongo, Bituntu, Kibona, Katoro, Mikoni, Kibirizi Ngarama, Ruhoko na Ruhunga.
No comments:
Post a Comment