NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT
Wazalendo) kimemwandikia barua msajili wa vyama vya siasa, kikijibu barua yake
iliyotaka kujieleza kwa kukiuka masharti ya kifungu cha 11 A cha sheria ya
vyama vya siasa kikimtaka arejee na kufahamu tafasiri sahihi ya kifungu hicho.
Barua hiyo ya Septemba 24, 2020 yenye kumbukumbu
namba ACT/HQ/MSJ/023/Vol.III/248 inamtaka msajili afahamu maana, tafasiri
sahihi na tofauti ya vyama kuungana chini ya kifungu hicho na mgombea mmoja
kuonyesha imani yake kwa mgombea mwingine katika uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo imesainiwa na Jaran
Bashange kwa niaba ya katibu mkuu, mgombea mmoja kuonyesha imani kwa mgombea
mwingine ni jambo la kupigiwa mfano kwa siasa za Tanzania kuwa licha ya
ushindani wa kisiasa, umoja na mshikamano kama Watanzania unadumishwa.
Sehemu ya barua hiyo ambayo TANZANIA PANORAMA
imeoina inasomeka; 'nakiri kupokea barua yako ya tarehe 22 Septemba, 2020 yenye
kumbukumbu namba HA.322/362/21/90 inayotutaka tuwasilishe maelezo juu ya
mgombea wetu wa urais wa Zanzibar, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad kumuombea kura
mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tundu Antipas Lissu
'Katika barua yako umetukumbusha uwepo wa kifungu
cha 11 A cha sheria ya vyama vya siasa kinachoweka utaratibu wa vyama
"kushirikiana" na ukaenda mbali kuwa kwa vyama kushirikiana
bila kufuata utaratibu uliowekwa ni kukiuka sheria.
'Tunapenda kueleza kuwa mgombea wetu wa urais wa
Zanzibar, mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad hajakiuka kifungu cha 11 A cha
sheria ya vyama kinachoweka utaratibu wa vyama kuungana au vinavyokusudia
kuungana kabla au baada ya uchaguzi.
'Aidha, mheshimiwa Seif Sharif Hamad hakumuombea
kura ndugu Tundu Antipas Lissu kama inavyodaiwa na ofisi yako. Video clip
uliyotutumia haina maneno hayo na nikuombe urejee kuisikiliza upya kwa makini .
'Alichokisema mgombea wetu ni imani yake kuwa ndugu
Tundu Antipas Lissu atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo
ambalo liko wazi sana kutokana na mwelekeo wake wa kuungwa mkono na Watanzania
walio wengi.
'Hii inathibitishwa na namna wananchi wengi na kwa
hamasa kubwa wanavyojitokeza katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea. Hilo
si kosa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.
'Kauli na imani hiyo haina tafasiri ya kuungana kwa
vyama vyetu vya Alliance for Change and Transparent (ACT Wazalendo) na Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ila chama chetu kina Imani kuwa mgombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chama Cha Mapinduzi, Ndugu John Pomne
Magufuli hatakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi wa
tarehe 28 Oktoba, 2020.'
Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilikiandikia ACT
ikikitaka kitoe Maelezo kuhusu hatua ya Maalim Seif kumuombea kura mgombea
urais wa Chadema, Lissu.
No comments:
Post a Comment