NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya
Chama Cha Mapinduzi itajenga kituo kipya cha afya katika Kata ya Irugwa, Wilaya
ya Ukerewe mkoani Mwanza ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu wananchi
wa kata hiyo kufuata huduma za kitabibu
Akizungumza leo na wakazi wa Kata ya Irugwa wakati
wa mkutano wa kumuombea kura mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais
John Magufuli, amesema uamuzi huo unakwenda sambamba na ahadi ya Ilani ya
Uchaguzi ya 2020 - 2025.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amesema katika ilani ya uchaguzi ya
2020-2025, ukurasa wa 186 unasomeka, "hadi kufikia 2025 serikali
itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asimilia 20 ya vituo 8,446
vilivyopo sasa; vipaumbele vitawekwa katika ujenzi wa vituo vya afya na
ukamilishwaji wa maboma kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia, idadi ya watu na
wingi wa wagonjwa."
Amesema Serikali ya Rais Magufuli imekwishatoa sh
milioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo moja la kujifungilia katika
zahanati Irugwa.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji
kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi, alisema ilani imeweka mipango
imara ya kushughulikia upatikanaji wa maji vijijini kama hatua ya kutekeleza
azma ya Rais Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kuhusu usafiri wa majini, Waziri Mkuu Majaliwa
amesema Serikali ya CCM ikiingia madarakani inakusudia kujenga vivuko
mbalimbali kikiwemo kivuko cha Irugwa, Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi
Kisorya.
" Kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya CCM,
ukurasa wa 83 hadi 84, Chama Cha Mapinduzi kimeielekeza serikali ikamilishe
ujenzi wa vivuko vipya nane kikiwemo cha Irugwa - Murutanga wilayani Ukerewe.
"Pia ilani imeelekeza serikali ianze kutekeleza
mradi wa ujenzi wa maegesho ya Lugezi - Kisorya mkoani Mwanza, Kome na
Nyakalilo mkoani Mwanza, Utete huko Pwani, Chato- Nkome huko Geita, Iramba na
Majita mkoani Mwanza na Irugwa," alisema.
No comments:
Post a Comment