Lissu, Chadema na siri ya kivuli cha mauti
NA CHARLES MULLINDA
KUNA mijadala mingi inayoendelea kuhusu kushambuliwa
na Serikali na Bunge kumtelekeza kwa kutomlipia gharama za matibabu, mgombea
urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Liss aliyeshambuliwa
kwa risasi Septemba 7, 2017, alipokuwa akitoka kwenye kikao cha Bunge
kurejea nyumbani kwake eneo la area D, jijini Dodoma kwa mapumziko ya
mchana.
Mijadala ni mikali hasa kwenye mitandao ya kijamii
ambako baadhi ya wachangiaji, kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakipotosha
ukweli kuhusu uamuzi wa familia ya Lissu na Chadema kuiweka pembeni Serikali na
Bunge kujihusisha kwa namna yoyote ile na matibabu ya Lissu.
Lissu mwenyewe ndiye anayeiibua mijadala hiyo na
kuikoleza baada ya kurejea nchini hivi karibuni akitokea Ubelgiji alikokuwa
akiishi. Hivi sasa anagombea urais na katika hotuba zake anazozitoa kwenye
majukwaa ya kisiasa anapozunguza nchi nzima kusaka kura zitakazomuwezesha kuwa
rais amekuwa akihubiri shambulio hilo dhidi yake tofauti ya uhalisia wake.
Mwandishi Charles Mullinda alifanya uchunguzi wa
kina kuhusu sakata hilo na kuandika ripoti maalumu ambayo haijawahi kukosolewa
au kupingwa na Chadema, Lissu mwenyewe, Serikali, Bunge au chombo chochote cha
kiuchunguzi ndani na nje ya nchi.
Ripoti hiyo ilichapishwa kwanza katika vyombo vya
habari na hapa mwandishi anairejea ili kuweka kumbukumbu sahihi kuhusu tukio
hilo.
Ripoti hii maalumu inaelezea mtiririko wa matukio
baada ya shambulizi hilo la kusikitisha; utata wa Chadema kutaka kumchukua
Lissu akiwa mahututi, matibabu ya awali aliyopatiwa katika Hospitali ya Rufaa
Dodoma, ambayo yalimsaidia kusafiri salama hadi Nairobi Kenya, majadiliano
baina ya Serikali, Bunge, familia ya Lissu, Chadema, NHIF na wadau wengine
kuhusu wajibu na dhamana ya kumtibu, pamoja na taratibu za matibabu ya wabunge
kwa ujumla.
Taratibu za matibabu kwa wabunge zimeonyesha kuwa
wabunge wote, mawaziri na maspika wastaafu, wanastahili kupewa matibabu bure
ndani na nje ya nchi; na Bunge linapaswa kugharamia matibabu hayo.
Hivyo, wabunge wote ni wanachama wa Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya (NHIF), ikijumuisha wenza wao na watoto wanne wa umri usiozidi
miaka 18. Na hii ni kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji Bunge, Sura Na.115
ya Mwaka 2008.
Taratibu hizo zimeonyesha kuwa mfuko husimamia
matibabu ya wabunge ndani ya nchi kwa mujibu wa mkataba wa utoaji huduma hiyo
uliopo.

Kwa yake maneno yake aeleza; "Mwanachama
anayeamua kwenda kujitibu mwenyewe sisi hatuna dhamana naye. Wanachama wetu
huwa tunawaambia vituo au hospitali ambazo wanapaswa kwenda kutibiwa ambazo
tuna mkataba nazo.
"Hospitali au vituo vya afya ambavyo tuna
mkataba huwa vinatuletea madai baada ya kuwatibu wateja wetu wakiwamo wabunge
na sisi tunalipa.
"Bima ya Afya ni kama bima ya magari, gari
lisipogongwa haliendi kutengenezwa lakini likigongwa gharama ya kulitengeneza
ni kubwa na pengine mtu anaweza kupewa gari jipya kabisa. Hivyo hivyo na Bima
ya Afya ukiugua unaweza kutumia gharama kubwa sana kutibiwa.
"Lakini mtu anayeamua kujitibu mwenyewe ndani
au nje ya nchi, huo ni uamuzi wake na sisi hatuna dhamana hapo kwa sababa
kwanza ugonjwa ni siri ya mtu."
Kauli hii ya Konga inatoa picha kuwa mbunge
anapoamua kwenda kujitibu mwenyewe ndani au nje ya nchi bila kufuata utaratibu
uliowekwa na NHFI, gharama za matibabu yake anazibeba yeye mwenyewe.
Utaratibu wa matibabu kwa wabunge na mawaziri
unaonyesha kuwa matibabu ya wabunge nje ya nchi yanasimamiwa moja kwa moja na
Bunge lenyewe.
Kunapokuwa na mahitaji ya mbunge kutibiwa nje ya
nchi, jopo la madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) au Moi ndiyo
hushauri na ndizo taasisii pekee zenye mamlaka ya kupendekeza kwa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Kwa mujibu wa taratibu hizo ili matibabu ya nje
yafanyike ni sharti mbunge atibiwe katika hospitali za ndani zilizosajiliwa na
NHIF na inaposhindikana ndipo rufaa ya kwenda Muhimibili au Moi hutolewa.
Endapo mbunge atapata rufaa ya kwenda kutibiwa nje
ya nchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
hulitaarifu Bunge, ikiweka bayana hospitali anayokwenda kutibiwa, muda wa awali
wa matibabu na endapo kuna hitaji la kusindikizwa na mwana familia, daktari au
muuguzi, rufaa hiyo huweka bayana.
Wajibu wa Bunge baada ya kupokea rufaa, hufanya
maandalizi ya safari ya nje, ikijumuisha gharama za matibabu ya mwanzo, kununua
tiketi ya ndege, posho ya kujikimu kwa mbunge na msindikizaji au wasindikizaji
na kibali cha kusafiri nje ya nchi kwa mujibu wa Amri ya Rais wa Awamu ya Kwanza
“State House Clearance” kwa safari zote za nje bila kujali kama ni matibabu au
shughuli nyingine yoyote kwa yeyote anayelipwa fedha za umma kusafiri nje ya
nchi.
Rekodi zilizoko serikalini zinaonyesha kuwa
haijapata kutokea kwa mbunge aliyepata rufaa kukosa kibali cha Ikulu cha
kusafiri nje ya nchi kwa matibabu.
Sheria ya uendeshaji Bunge inaeleza kuwa mbunge ana
haki ya kupata posho ya jimbo kila mwezi, mshahara wake pamoja na fedha za
mfuko wa jimbo hata pale anapokuwa mgonjwa. Na katika uchunguzi wa sakata hili
ilibainika pasipo shaka kuwa Lissu alikuwa akipatiwa stahiki zake hizo.
Uchunguzi ulionyesha kuwa Lissu alikuwa halipwi
posho ya vikao na posho ya ushiriki na hilo limethibitishwa na mmoja wa maafisa
wa Bunge wa Idara ya Uhasibu aliyetoa ushirikiano mkubwa wakati wa uchunguzi
huu lakini jina lake limehifadhiwa kwa sababu siyo msemaji wa Bunge.
"Haki zake anapata kama ulivyo utaratibu,
tunamlipa mshahara wake, tunampa posho ya jimbo na fedha ya mfuko wa jimbo
lakini hapewi 'sitting allowance' na 'per diem' kwa sababu hizo ni lazima
aingie kwenye vikao.
"Na fahamu kuwa mbunge akifanya safari binafsi
nje ya nchi, Bunge haliwajibiki kumlipa yeye wala msaidizi wake 'per diem',
hata akiwa mgonjwa halipwi kama kaenda binafsi kwa sababu anakuwa hana rufaa
inayotambulika, utaratibu huo uko wazi," alisema afisa huyo.
Taarifa zaidi zilizokusanywa kutoka ndani ya Bunge
la Jamhuri ya Muungano, zilionyesha kuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo,
matibabu endelezo ya wabunge na familia zao hufanyika nchini India katika
Hospitali ya Apollo isipokuwa kama inapendekezwa tofauti kulingana na
aina ya matibabu yanayotakiwa kutokuwepo India na katika Hospitali ya Apollo,
ndiyo uamuzi wa matibabu mbali na India hufanyika.
Kwamba kama ilivyo kwa wabunge wote, Lissu
alistahili kutibiwa katika hospitali na vituo vyote vilivyosajiliwa na NHIF kwa
kuzingatia ‘medical scheme’ ya matibabu ya wabunge ambayo inampatia mbunge
nafuu ya kulipiwa gharama zote, kusafirishwa kwa ndege au helikopta kokote
atakapopata dharura ya matibabu na kuhitaji kupelekwa ambako kuna hospitali
yenye utaalamu zaidi popote ndani ya nchi na huduma za gari la wagonjwa.
Hivyo, uchunguzi ulithibitisha kuwa Lissu
aliposhambuliwa kikatili kwa risasi, gharama za matibabu yake zilipaswa kubebwa
na NHIF kwa jinsi ile ile utaratibu unavyoelekeza na tayari jukumu hilo
lilikuwa limekwishaanza kutekelezwa chini ya usimamizi wa Bunge
Lakini NHIF haikuweza kuendelea kutimiza wajibu wake
huo baada ya familia ya Lissu na Chadema kumtwaa kwa kile walichoeleza kuwa
hawakuwa na imani na Serikali wala Bunge kusimamia matibabu hayo.
Uchunguzi kuhusu sakata la Serikali na Bunge
kutolipia gharama za matibabu ya Lissu ulionyesha kuwa baada ya kufikishwa
Hospitali ya Rufaa ya Dodoma akiwa na majereha mengi ya risasi na akiwa
amepoteza damu nyingi, wabunge wa Chadema wakiongozwa na mwenyeketi wao,
Freeman Mbowe, dereva wa Lissu na wafuasi wao walizingira eneo la chumba cha
upasuaji alikokuwa amelazwa wakitaka kumchukua ili wakamtibu mahali wanapopajua
wao.
Ilielezwa na mashuhuda kuwa purukushani hiyo
ilidumu kwa muda huku walinzi wa hospitali wakipambana na kundi hilo lenye
hasira na jazba. Uongozi wa hospitali uliomba msaada wa askari polisi kutuliza
jazba, lakini hawakufanya lolote zaidi ya kuangalia tu.
Matibabu waliohojiwa wanaeleza kuwa Lissu
alifikishwa hospitalini na wana familia ya Naibu Spika, Tulia Ackson anayoishi
nayo jirani eneo la Area D na gari lililotumika kumfikisha hospitalini hapo ni
la Khadija Akukweti.
Msimamo wa Mbowe, wabunge wa Chadema na wafuasi wao
kutaka kumtwaa Lissu kutoka hospitalini waliujenga katika msingi wa kutokuwa na
imani na hospitali za Serikali hivyo walitaka wapewe wakamtibu wenyewe mahali
wanakokujua.
Wafanyakazi hao wanaeleza kuwa Lissu alifikishwa
hospitalini akiwa na hali mbaya sana. Alikuwa na majereha mengi ya risasi na
alikuwa amepoteza damu nyingi hivyo alihitaji matibabu ya haraka na hasa
kuongezewa damu.
Kwamba kwa namna yoyote ile, kumuondoa hospitalini
kama ilivyokuwa ikishinikizwa na Mbowe na wenzake lilikuwa jambo la hatari
kwa sababu lingeweza kugharimu maisha yake.
Katika mahojiano hayo, matabibu nao walihoji busara
ya kutaka kumchukua ilitoka wapi ikizingatiwa muda ule ilikuwa mchana,
akiwa amepoteza damu nyingi na hajiwezi! Walitaka kumpeleka wapi ambako
walikuwa na imani nako?
Mmoja wa manesi (jina tunalihifadhi) ameeleza kuwa
kwa anayeijua Dodoma vizuri, zaidi ya hospitali za Serikali hakuna hospitali
kubwa ambayo ingeweza kufanya walichokifanya madaktari wa Hospitali Rufaa ya
Dodoma. Anasema hajui kama Lissu analijua hilo na dhamira ya wenzake ya
kutompatia tiba mbadala.
Uchunguzi ulionyesha kuwa madaktari wa
Hospitali ya Rufaa Dodoma pamoja na uongozi wa Bunge, kwa kutambua hatari
ambayo ingeweza kutokea kwa Lissu iwapo asingepatiwa matibabu ya haraka na ya
dharura, busara iliwaongoza kumuita Mbowe na Mchungaji Msigwa ofisini kwa
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Dodoma kufanya naye kikao ili waruhusu Lissu
atibiwe haraka kuokoa maisha yake.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma na Katibu wa Bunge.
Katika kikao hicho yalifikiwa makubaliano kuwa ni
lazima jitihada za kuokoa maisha yake zichukuliwe haraka hivyo Mbowe alitakiwa
aruhusu mara moja aongezewe damu na afanyiwe upasuaji.
Makubaliano mengine yaliyofikiwa kwenye kikao
hicho ni uongozi wa Chadema kuwaondoa wafuasi wao wote waliokuwa wamejazana
hospitalini hapo, polisi wote waliokuwa hospitalini waondolewe na Mkuu wa
Mkoa (RC) na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) watoe taarifa rasmi juu ya tukio
hilo, mambo ambayo yalitekelezwa
Ilielezwa na baadhi ya wanafamilia na jamaa wa
karibu wa Lissu waliofikiwa wakati wa uchunguzi na kuzungumza huko Singida kuwa
haina shaka hata kidogo kuwa Lissu hajapata kuambiwa hospitali ambayo wenzake
walisena hawana imani nayo ndiyo ilimtibu kwanza kwa kumuongezea damu na kuziba
majeraha ya risasi ili damu isiendelee kuvuja pamoja na kumfanyia upasuaji wa
kwanza.
Kazi ya kuokoa maisha ya Lissu iliongozwa na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki
Ulisubisya.
NHIF ilitafuta ndege kwa ajili ya kumpeleka Lissu
Muhimbili kwa matibabu zaidi ambayo iliwasili Dodona majira ya Saa 10 jioni na
kusubiri matibabu ya awali yakamilike ili asafirishwe kwenda Muhimbili au
Moi.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati tukio la Lissu
kushambuliwa linatokea, Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa Dar es Salaam
akiongoza ujumbe wa Bunge Ikulu ya Magogoni, ambako Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alikuwa akiwasilisha kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli taarifa za
Kamati za Almasi na Tanzanite alizokuwa amepokea toka kwa spika jana yake mjini
Dodoma.
Spika alirejea Dodoma baada ya kumalizika kwa tukio
hilo na kwenda hospitalini kumjulia hali Lissu, lakini hakuweza kumuona kwa
sababu alikuwa bado yupo katika chumba cha upasuaji.
Hata hivyo, Spika aliyepokelewa na Waziri wa Afya,
alipokea taarifa ya mganga mkuu kwa Spika kuhusu hali ya Lissu ambaye madaktari
walikuwa katika jitahida za kuokoa maisha yake.
Spika alielezwa kuwa Lissu angehitaji matibabu zaidi
Muhimbili au Moi na endapo itakuwa haitoshi basi apelekwe nje ya nchi.
Baada ya Spika kupokea taarifa hiyo, aliongoza kikao
kilichofanyika jengo la NHIF na kuhudhuriwa na Waziri wa Afya,
ndugu wa karibu wa Lissu, Mbowe, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye pia ni Kamishna
wa Bunge, na makamishna wengine wakiwemo Salim Turki, Idd Azzan Zungu, Katibu
wa Bunge pamoja na mwakilishi wa NHIF ili kujadili matibabu yake zaidi.
Katika kikao hicho, Spika alipewa maelezo ya tukio
zima lilivyotokea na hatua zilizochukuliwa na yeye alieleza wazi kuwa Bunge
litatekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha Lissu anapata matibabu ndani na nje ya
nchi endapo itahitajika kufanya hivyo.
Lakini pia Waziri wa Afya, naye alisema jopo la
madaktari litashauri kama ulivyo utaratibu iwapo Lissu atalazimika kwenda
kutibiwa nje, Serikali itaridhia atapelekwa India au sehemu nyingine ambako
itashauriwa lakini katika hatua ya kushangaza ndugu wa familia alishukuru kisha
akasema hawahitaji msaada wa Serikali wala Bunge kumtibu Lissu.
Anakaririwa katika taarifa rasmi ya Bunge akieleza
kwa maneno yake mwenyewe kuwa "familia ya Lissu na Chadema
wanashukuru sana kwa ukarimu wa Serikali na Bunge lakini tunachokitaka ni
ruhusa ya kumchukua tukamtibu sehemu nyingine ambako tuna imani nako kwa sababu
hatuiamini Serikali wala Bunge na hatuko tayari kuona anapelekwa Muhimbili au
Moi ambako Serikali itakwenda kummaliza kabisa."
Huo pia ndiyo ulikuwa msimamo wa Chadema uliotolewa
na Mbowe mbele ya kikao na kurekodiwa katika kumbukumbu rasmi za kikao hicho na
kwamba waliitaka Serikali na Bunge visijihusishe kwa namna yoyote ile na Lissu
kwa sababu hawakuwa na imani na mamlaka hizo.
Taarifa ya kikao hicho inakwenda mbali zaidi kwa
kuonyesha kuwa Spika hakuwa na jinsi kwa sababu familia ya Lissu na Chadema
hawakuwa na imani na taasisi anayoiongoza hivyo kwa mikono miwili alikubali
matakwa ya familia na Chadema mbele ya makamishna wa Tume ya Bunge na Waziri wa
Afya.
Lakini kumbukumbu zaidi za kikao hicho zinaonyesha
kuwa Waziri wa Afya alitoa rai kwa familia na Chadema kuwa pamoja na uamuzi wao
huo watoe muda kwa jopo la madaktari waliokuwa wakimfanyia upasuaji wamalize
ndipo wamuandae kwa safari.
Inaeleza kuwa wakati kikao hicho kikiendelea, tayari
Rais Dk. John Pombe Magufuli alikuwa amekwishamuagiza Waziri wa Afya kusimamia
na kuratibu mipango yote ya matibabu ya Lissu na maagizo mengine alikwishatoa
kwa vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia tukio hilo.
Sehemu moja ya kumbukumbu ya kibunge ambayo
inathibitishwa na mmoja wa maafisa wa Ikulu aliyezungumzia sakata hilo
inonyesha kuwa Rais Dk. Magufuli alikuwa amemuagiza Waziri wa Afya kuharakisha
mchakato wa rufaa ya Lissu kwenda Hospitali ya Apollo nchini India au
kwingineko ambako ingeshauriwa na madaktari wa Muhimbili au Moi kwa jinsi hali
yake ilivyokuwa na kwamba alikuwa akisuburi ushauri wa madaktari ili kutoa
ridhaa tu.
Afisa huyo wa Ikulu alielzai kuwa baada ya uamuzi wa
familia na Chadema wa kulazimisha kumchùkua Lissu huku wakiionyooshea kidole
Serikali na Bunge kutaka kwenda kumuua iwapo angelazwa katika hosiptali za hapa
nchini, Rais alipopewa taarifa hiyo aliinamisha kichwa chini kwa masikito na
kwamba hakuzungumza chochote tena.
Chadema na familia ya Lissu baada ya kuitosa
Serikali na Bunge na jukumu hilo kubaki mikononi mwao, walianza
maandalizi ya kumpeleka Nairobi Kenya kimya kimya bila kulitaarifu Bunge
wala Serikali. Waliwasiliana na rubani wa ndege ndogo iliyokuwa imeletwa
na NHIF ili imsafirishe kwenda Nairobi na gharama za safari hiyo zingelipwa na
Chadema wenyewe.
Hata hivyo, rubani huyo aliwaambia ndege yake
haiwezi kwenda Kenya wakati huo kwa sababu haina chombo cha kuongozea ndege
wakati wa kutua usiku.
Baada ya hapo, Chadema waliwasiliana na mmoja wa
makamishna wa Bunge, Salim Turky ili awadhamini wakodishe ndege ndogo
imsafirishe kisha watalipa jambo ambalo lilifanyika na Lissu alisafirishwa
majira ya saa sita usiku kwenda Nairobi akiwa ameambatana na viongozi wa
Chadema pamoja na mkewe.
Mahojiano ya pande zote zilizofikiwa yalionyesha
kwamba Bunge na Serikali vilikuwa tayari kutimiza wajibu wa kumtibu Lissu
lakini Chadema na familia yake walikataa.
Hili lilithibitishwa pia na taarifa ya uongozi
wa Chadema na familia ya Lissu walioweka wazi kuwa ni nia ya Serikali kumuua
huku wakijiapiza kutokuwa tayari kuona akipelekwa Muhimbili au Moi.
Nyaraka zote za kumbukumbu ya tukio hilo na watu
wote waliohojiwa havionyeshi msimamo huu kubatilishwa na hilo linajenga
taswira kuwa malalamiko kwamba Lissu alitelekezwa hayana msingi.
Katika uchunguzi wa nani anapaswa kubeba gharama za
matibabu ya Lissu kwa kurejea baadhi ya matukio ya wabunge waliopata kutibiwa
nje ambao mwenendo wa matibabu yao umekuwa ukitolewa kama mfano wa kwanini
Serikali na Bunge visitende hivyo hivyo kwa Lissu, imebainika kuwa;.
Kwa mujibu wa taratibu, rufaa ya mbunge kwenda
kutibiwa nje ya nchi inatolewa baada ya jopo la Madaktari wa Muhimbili au Moi
kutoa mapendekezo kwa Wizara ya Afya kuwa mgonjwa husika anahitaji rufaa ya
kwenda nje ya nchi.
Na kwamba kiongozi wa ngazi ya mbunge, rufaa yake
kwenda kutibiwa nje ya nchi ni lazima mamlaka ya rais itoe ridhaa kama ilivyo
kwa majaji na mawaziri.
Vyanzo mbalimbali kutoka serikalini vilieleza kuwa
utaratibu wa mamlaka ya Rais kutoa ridhaa ya safari za nje kwa viongozi
haukuwekwa na Rais Dk. John Magufuli bali umekuwapo tangu wakati wa Rais wa
Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.
Inaelezwa kwamba Mwalimu Nyerere aliweka utaratibu
huo wakati nchi ikiwa kwenye matatizo ya fedha za kigeni mwaka 1978, lengo
lilikuwa kusimamia safari za viongozi nje ya nchi.
Hivyo kilichofanywa na Serikali ya Awali ya
Tano ni kukumbushia tu takwa hilo ambalo lipo tangu awamu ya kwanza na kama
kulikuwa na kulegalega kwa usimamizi wa kanuni na taratibu hapo katikati hilo
ni jambo jingine.
Aidha, rekodi zaidi za kibunge zilionyesha kuwa
aliyekuwa Spika wa Bunge, marehemu Samuel Sitta, yeye baada ya ubunge wake
kukoma, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alitoa amri ya rais kuwa maspika
wastaafu wote wapewe matibabu kama ya wabunge.
Kwa sababu hiyo, maspika wastaafu wana kadi za NHIF
lakini nao ili wakatibiwe nje ya nchi huwa wanafuata taratibu zote za rufaa.
Imeelezwa kuwa marehemu Sitta alikwenda Uingereza
kwa mambo yake binafsi na kuangalia afya yake, akiwa huko aliugua na
alipozidiwa huku uwezo wa kifedha ukawa mdogo aliwasiliana na uongozi wa Bunge,
ambao ulimkasimu Balozi wa Tanzania nchini Uingereza jukumu la kutoa taarifa ya
hali yake na kuiwasilisha Wizara ya Afya kwa taratatibu nyingine za rufaa, na
baadae akapewa rufaa husika, na ndipo Bunge lilipochukua jukumu lake.
Kumbukumbu hizo zinaonyesha pia kuwa marehemu
Philemon Ndesamburo, naye alipougua ghafla akiwa nchini Uingereza alikokwenda
kwa shughuli zake binafsi, kama mbunge alifuata utaratibu kama ilivyokuwa kwa
marehemu Sitta.
Pia dada yake Lissu, marehemu Christina Mugwai
alipougua na kutakiwa kwenda nje kwa matibabu zaidi kwa ushauri wa Hospitali ya
Aghakhan, ilibidi utaratibu ufuatwe ambapo alihamishiwa Muhimbili na baada ya
jopo la madakari kupendekeza ndio wizara ilitoa rufaa yake ya kwenda
india.

Mwingine katika orodha hiyo ni Dk Eli Macha,
aliyekuwa Mbunge wa viti maalumu Chadema, yeye alipougua alianza kujitibia
binafsi katika Hospitali ya Siliani Arusha, kisha akaenda Nairobi na baadaye
Uingereza.
Alipozidiwa na hali ya kifedha ikawa haimruhusu
kuendelea kujigharamia mwenyewe, akiwa kitandani, aliomba uongozi wa Bunge
umsaidie umgharimie. Taratibu hizo hizo zilifuatwa, lakini haikuwezekana kwa
kuwa alifariki mapema kabla ya kupelekwa India.
Kamishna mmoja wa Bunge alieleza kuwa; “Lakini kwa
namna ya kipekee wabunge wanapopewa rufaa kwenda India na kuamua kwenda
kwingineko kwa gharama zao, hilo haliwezi kuwa kosa kwao sababu ni matakwa yao
binafsi na haijawahi tokea mbunge wa aina hiyo arudi tena kulalamika huku akiwa
amekataa haki yake ya msingi kama alivyofanya Lissu.
"Mbona wapo wabunge wengi tu ambao walipewa
rufaa ya kwenda nje lakini walikataa na kwenda kwingineko na haijawahi kuwa
jambo la kuilalamikia Serikali na Bunge.
“Sambamba na hilo matibabu ya mbunge huwa hayana
chama, lakini hili la Lissu mbona Chadema inakuwa ndio msemaji wake. Wabunge wa
vyama vyote wamekuwa wakipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi na familia zao na
haijawahi tokea chama fulani ndio kikawa msemaji, nadhani hapo kuna
shida.
"Suala la Lissu lisifanywe kuwa la kisiasa na
nadhani hapo ndipo kwenye tatizo, wabunge wa kila kambi ndani ya Bunge wanapata
matibabu kila mmoja kwa binafsi yake na haijawahi semekana kuwa wanakosa
matibabu sababu ya itikadi zao. Hapa tunampongeza sana Spika wa Bunge, Job
Ndugai kwa kusimamia haki ya msingi ya kila mbunge na familia yake.
"Familia yake iwe ndio msemaji, tena ile ya
karibu inayotambuliwa na Bunge na hasa mwenza wake. Na pengine kama Chadema na
familia walifanya kosa kutoa lugha ya kejeli na majigambo na kukataa haki ya
msingi iliyowekwa kisheria, wanaona shida gani kwa utaratibu ule ule
walioutumia kukataa haki ya kumtibu ndani na nje, kurejea tena na kusema
tumekosea tunaomba radhi?”
Mwenendo mzima wa uchunguzi ulionyesha kuwa Chadema
haikuwa na dhamira ya kweli ya kutaka kumtibu Lissu ilipoonyesha nia ya
kumchukua akiwa dhaifu, amepoteza damu nyingi na hajitambui.
Tafasiri ya kitendo hicho ni kuwa Chadema walitaka
kuchelewesha matibabu yake kwa makusudi ili baadaye kipate sababu ya kuilamu
Serikali na Bunge.
Kama siyo jitihada za Serikali na Bunge, leo hii
historia ya Lissu ingekuwa inasomeka kuwa aliyewahi kuwa mbunge wa
Singida Mjini.
Lakini pia Lissu mwenye alipata kukiri mchango na
weredi wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa Dodoma.
Kwa wafuatiliaji wa mambo wanapaswa kujiuliza kuwa
ni kwanini Chadema walitaka kumchukua Lissu huku wakijua kuwa hawana hata senti
kwa ajili ya matibabu yake.
Kwa sababu hata walipopewa akiwa tayari
amekwishafanyiwa matibabu ya awali hawakuwa na fedha ya kulipia ndege na
walikuwa hawakopesheki. Iliwalazimu wasaidiwe kudhaminiwa ndege ambayo malipo
yake ilichukua zaidi ya mwezi mzima baada ya kupitisha bakuli wachangiwe.
Na walilipa baada ya mdhamini wao kutishia
kuwashtaki. Lakini pia Chadema walikataa kutoa namba ya akaunti ili wabunge
wamchangie Lissu kama ilivyokuwa imeombwa na Spika.
Serikali na Bunge kwa kutambua mchango wake, licha
ya Chadema kung'ang'ania kumchukua, ililipia gharama za daktari aliyemsindikiza
hadi Nairobi Kenya.
Hitimisho la uchunguzi linaonyesha kuwa
Chadema walitupa jongoo na mti wake kwa sababu walimzuia hata Spika kwenda
kumjulia hali kwani kila alipoomba kwenda kumuona alipingwa chenga wakati watu
wengine walipageuza Nairobi kuwa sebule na kituo cha kumshambulia Rais Magufuli
na Bunge.
Mwisho
WARAKA WA VIJANA WA ACT WAZALENDO KWA ZITTO, MEMBE
Mgombea urais wa ACT ni Zitto au Membe
SISI Vijana wa ACT kutoka mikoa mbalimbali tunaendelea kusikitishwa na mwenendo wa uendeshaji wa chama chetu ambapo mpaka sasa hatuelewi kampeni inaendeshwa vipi zaidi ya kuona kila kitu kiko kwa mtu mmoja.
Pale Mlimani City tena kwa mbwembwe, chama chetu kilimteua Ndugu Bernard Membe kuwa mgombea urais na akaahidi kampeni ya kishindo. Kiongozi wa chama naye akaahidi hivyo hivyo.
Cha ajabu na ambacho sasa tunahitaji majibu kwa chama ni badala ya mgombea huyo rasmi wa urais kufanya kampeni sasa hivi tunamuona kiongozi wa chama, Zitto Kabwe akifanya mikutano mingi ya kampeni kuliko hata mgombea urais.
Juzi tu Zitto Kabwe alikuwa Dar, akaenda Kigoma na tukamuona kwenye ndege za ATC, akarudi Dar, akaenda Mafia, akaenda Mtwara sasa kaenda Kigoma. Swali huyu ndiye mgombea urais wetu mpya? Ameteuliwa kimya kimya? Mzee wetu Membe kapatwa na nini?
Hivi kwa stratejia hizi zilizoshindwa mapema tukipata kura kiduchu tutaanza vurugu za kudai tumeibiwa kura? Na nani kama mgombea wiki nne sasa hayuko majukwaani badala yake anafanya mtu ambaye siyo mgombea na 'kujibrand' yeye.
Tena bahati mbaya ndugu Zitto wala hamwombei kura mgombea, yeye ni kuhangaika na Magufuli na CCM na kumsifu na kujipendekeza kwa Lissu wa Chadema. Hakika hivi ni vituko!
Zaidi sasa kiongozi wetu wa vijana naye akitoka Kigoma kama Zitto, Abdul Nondo, anamzidi Membe eti naye kusafiri kwenda kuzindua mikutano ya wabunge nchi nzima!!
Hiki chama hakina uongozi, hakina stratejia na kimechoka katika umri mdogo sana. Tunasikitika.
Yani tunaumia sasa sisi vijana tunaohangaika huku mitaani kukitangaza chama, huku kiongozi wa chama na mgombea urais wakituahidi kampeni ya kishindo ndiyo hii ya Zitto kuzunguka kula per diem na Nondo aliyetoka chuoni mwaka jana kuwa ndiyo mwanasiasa wa kwenda kuzindua kampeni za majimbo na wakongwe wa siasa ndani ya chama kuachwa??
Tunahitaji majibu. Yani ACT kimekuwa chama cha kikabila, utasikia Maalim Seif yuko Pemba, Zitto yuko Kigoma, mikoa mingine chama ziiiii. Inatuuma sana.
HUU NI WARAKA WA WAZI WA VIJANA WA ACT WAZALENDO. TANZANIA PANORAMA BLOG IMEUBEBA KUTOKANA NA UJUMBE WAKE MZITO KWA WANACHAMA, WAPENZI NA MASHABIKI WA ACT- WAZALENDO NA PIA KWA WATANZANIA WOTE.
TUMEMSAHAU MTEMI MILAMBO NA KISIMA CHAKE
NA GEORGINA ROESER
HISTORIA ya Tanzania ina mashujaa wake. Mtemi
Milambo wa Wanyamwezi ni miongoni mwa mashujaa wa Taifa letu ambaye historia
yake tumeienzi kwa kuwa na shule za serikali za msingi na sekondari zilizobeba
jina lake.
Kisima hiki hii leo kina umri zaidi ya miaka 160 kinatoa maji watu wanateka wanatumia. Kimeachwa wazi tu mbuzi, paka, mbwa na wanyama wengine wamewahi kutumbukia na kufa humo kisimani. Haijawahi kushtua uongozi wowote hata wa soko tu la hapo barabara ya 13 kuwa kuachwa wazi kisima hicho ni hatari kwa maisha ya watu pia.
Kisima hicho kwa maoni yangu ni historia ya Mtemi
Milambo. Kwanini hatukienzi? Niliwahi kufika Kigoma miaka michache iliyopita.
Kuna eneo Kigoma linamuenzi Livingstone. Muite Livingstone vyovyote
utakavyopenda. Kwangu Mimi alikuwa mkoloni tu wa kizungu!
Tanzania inunue Petroli iweke Akiba
NA GEORGINA ROESER
BEI ya Petroli iimeshuka. Iko chini sana karibu
duniani kote. Hii ilitokana na uzalishwaji mkubwa wa mafuta huko Urusi na Saudi
Arabia.
Mataifa haya mawili yana msuguano wa kibiashara
unaohusu bei ya mafuta. Kwa sababu ya msuguano huo, mataifa haya kila moja
liliamua kuzalisha mafuta zaidi ya maradufu ya uzalishaji wake wa kawaida. Hapa
ndipo neema ya kushuka kwa bei ya mafuta kwa mataifa yasiyozalisha nishati hiyo
ilipoanzia. Vita vya panzi, kuku wanapeta.
Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump
hakuupenda msuguano huo kwa sababu taifa lake kwa sasa ni miongoni mwa mataifa
yenye mafuta mengi duniani.
Historia inaonyesha kuwa Marekani imekuwa ikipigana
vita katika mataifa mbalimbali ya Ghuba kwa miaka nenda rudi na kupora mafuta
yake.
Uporaji huo wa Marekani ndiyo ulioiwezesha kuwa na
hazina kubwa ya mafuta. Hivi sasa Marekani ina jeuri ya kukaa meza moja na
wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani kama Urusi na Saudi Arabia baada ya
kujilimbikizia bidhaa hiyo kwa njia ya uporaji.
Tukiachana na hilo. Ukweli mwingine ni kwamba
Wamarekani wengi waliwekeza katika biashara ya mafuta baada ya biashara zao za
vita kuanguka hivyo wana hazina kubwa sana ya Nishati hiyo waliyopora Mashariki
ya Kati.
Tangu Urusi na Saudi Arabia wamwage mafuta kedekede
duniani, Marekani ilianza kupoteza mapato kutokana na bei ya mafuta kuwa chini
sana miezi ya hivi karibuni. Wafanyabiashara wengi wa mafuta Marekani walikuwa
wakilalamikia sana hali hiyo mwishoni mwa mwaka jana na mapema Mwaka huu.
Kabla ya kivumbi cha Corona, Rais Trump alitangaza
kuwa ataomba 'poo' kwa Urusi na Saudi Arabia waache kufanya uzalishaji mkubwa
wa mafuta ili bei ipande Wamarekani waweze kuuza mafuta yao kwa bei ya juu.
Urusi na Saudi Arabia walikubali kujadili kilio
hicho cha Rais Trump lakini kabla ya kutekeleza hilo Corona ikabisha hodi.
Sijui mazungumzo yalipoishia lakini bei ya mafuta sasa IPO chini kila
kona ulimwenguni.
Kufupisha mjadala huu ni kwamba Corona ikishaondoka
vichwani vya watu, kuna uwezekano Urusi na Saudi Arabia wakafanya uzalishaji
mkubwa ili kujipatia kipato cha kupambana na madhara ya Corona kiuchumi. Hili
likifanyika litakuwa neema kubwa duniani kote.
Kwa upande mwingine kuna uwezekano pia Rais Trump
akawalipa fedha nzuri sana tu Urusi na Saudi Arabia wasizalishe kwa
wingi mafuta yao ili bei ipande, Marekani iuze kwa bei kubwa mafuta yake.
Marekani iko tayari kutoa kiasi kikubwa kwa
wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani kwa sababu haiwezi kuuza mafuta yake kwa
bei ya chini kama Urusi na Saudi Arabia kwa sababu mafuta yake iliyapata kwa
gharama kubwa sana wakati mataifa yanayozalisha yenyewe yanachimba tu. Hii
ndiyo sababu Marekani inataka bei ipande wakati wote.
Upo uwezekano Urusi na Saudi Arabia zitampuuza Rais
Trump lakini hilo hatupaswi kulizingatia sana kwa sababu lolote lile
linawezekana kutokea.
Sasa nini dunia inayoendelea ikiwemo Tanzania,
inapaswa kufanya wakati kama huu?
Kati ya mambo ambayo Afrika inapaswa kuiga kutoka
Marekani; cha kwanza ni choo na mfumo wa maji taka.
Nikiri kuwa nikiwa mkazi wa hapa, vyoo vyao ni
vizuri sana. Tunapaswa kuanza kuiga hilo siyo ule upuuzi wao wa
uhuru wa vyombo vya habari, haki za binadamu na Demokrasia.
Hapa kwenye mafuta tunapaswa kuiga pia. Tunapaswa
kufanya vile vile kama walivyofanya Marekani. Lakini sisi tusiende kupora bali
tukanunue na tuweke hazina kubwa.
Huu ni wakati muafaka kwa nchi yetu kununua
mafuta na kuyahifadhi kama ambavyo Marekani ilifanya miaka ya nyuma. Tukanunue
kwa bei poa ya sasa na tuyahifadhi kama Marekani walivyofanya.
Hatujui tunakoelekea bei itakuwaje. Kuwa na akiba ya
kutosha ya mafuta ni jambo la kuzingatiwa. Nchi kama yetu ikibidi hata tutakope
Urusi au Saudi Arabia mafuta mengi hivi sasa bei ikiwa chini ili baadaye tusije
kupoteza fedha nyingi bei itakapopanda.
Kama tuna fedha taslimu ni vema tulipie mzigo wrote
tutakaonunua lakini hata kama tumepungukiwa tukakope tu hayo mafuta. Urusi kwa
mfano ni marafiki zetu sana, hawatatunyima. Saudi Arabia pia
hawatatunyima.
Kuna uwezekano mkubwa bei ya mafuta itapanda siku
chache zijazo kwa sababu nilizozieleza hapo juu.
Marekani ina ushawishi mkubwa duniani kibiashara.
Urusi na Saudi Arabia watahitaji fedha baada ya Corona. Marekani kwa
ninavyowafahamu watawalipa Urusi na Saudia mabilioni wapunguze uzaliahaji.
Wakati ni huu. Binafsi naiona hii ni fursa kubwa
sana inayoweza kupaisha uchumi wetu tukichanga karata zetu vema.
.
Vita ya Kagera alama ya umoja na uzalendo wa
Mtanzania
NA GEORGINA ROESER
NIMEMALIZA kuangalia kipindi maalumu cha vita ya
Kagera kilichorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC). Ni kipindi chenye matukio
mengi ya kujifunza na binafsi kimeniacha najiuliza mambo kadhaa kuhusu Fashisti
Nduli Idi Amin.
Nawashauri Watanzania wawe na utamaduni wa kutazama
vipindi vya aina hii ili waone matukio halisi yalivyokuwa katika vita hiyo. Ni
katika kipindi hicho mtazamaji ataona wanajeshi wetu waliopigana vita ile
walivyopambana. Asanteni sana wanajeshi wetu.
Ninavuta picha joka lile lingeiteka nchi yetu
tungekuwa na maisha gani leo. Watanzania wanaosema tulimchokonoza Nduli Idi
Amini walishawahi kufikiri hili?
Nimejifunza mengi kwenye kipindi hicho ikiwemo Rais
Yoweri Museveni kupigana upande wa majeshi yetu dhid ya joka lile. Na udumu
huko Uganda Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Wale mnaompigia kelele ati muda wake umefika atoke
hebu kamtizameni huko alivyochezea tope na makombora kibao yakirindima!
Vita ilikuwa na matatizo ya miundo mbinu, sehemu
nyingine wanajeshi walibeba silaha nzito kwa sababu magari yalikuwa hayawezi
kupita kutokana na mvua iiliyokuwa ikinyesha lakini pia majigambo ya Fashiati
Amin yalikuwa yanaumiza sana.
Vita jamani ni majanga. Kama unamfahamu askari
yeyote muheshimu sana. Vita ni kitu kibaya sana. Wananchi walijitolea
vyakula, wanyama unawaona wanaswagwa kuchangia vita. Umoja na Uzalendo ule
naomba Mungu udumu nchini mwetu. Hivi vipindi TBC waangalie utaratibu na wizara
ya Elimu wawaoneshe wanafunzi mashuleni wajue tulipotoka.
Nadhani baadhi yetu huwa tunabeza baadhi ya mambo
kwa sababu hatujui historia.
Hamasa zilirembeshwa na:
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
IDUMU SIASA YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA
ZIDUMU FIKRA SAHIHI
VYOMBO VYA HABARI MAREKANI NA ULAYA MAHUSUSI KWA
PROPAGANDA
VYOMBO vya habari vya mataifa ya Ulaya na Marekani
kwa mfano BBC, VOA, DW ni vyombo vya propaganda vya serikali za mataifa yao.
Hilo si tatizo kwa sababu kwa njia moja au nyingine
serikali za nchi hizo ndiyo wamiliki wa vyombo hivyo wanapotutangazia katika
Idhaa mbalimbali kama Kiswahili, Chichewa, Ndebele na nyinginezo ni kukidhi
matarajio yao ya kueneza propaganda zao.
Ndugu zetu sasa wafanyakazi wageni wanaofanya kazi
katika vyombo hivyo vya habari wanapaswa kuchanganya changanya kidogo akili zao
na zile za mbayuwayu. Kadhalika serikali za nchi zetu nazo zijiongeze pia!
Vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani vinatangaza
kwa lugha mbalimbali ulimwenguni kote. Vina majina makubwa sana na vina nguvu
ya ushawishi wa mambo mbalimbali duniani. Hii inatokana na nguvu kubwa za
serikali za nchi hizo katika dunia. Kwa maana hiyo hatuwezi kuviepuka vyombo
vya habari vya mataifa hayo bali tunapaswa kushughulika navyo kimkakati.
Wenzetu wa nchi za Asia kwa mfano ni wajanja sana.
Nchi zao huweka makachero katika vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani na
matokeo yake propaganda za hawa mabwana wa magharibi huwa zinakwama.
Sisi waafrika tunashindwa vipi kubuni mbinu
kupambana na hivi vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani? Hatuwezi kuwatimua
kwani tunahitaji vidola vyao watatunyima na wataturindimishia madebe matupu
usiku kucha kuwa tunabana Uhuru wa vyombo vya habari. Hapatakalika.
Miaka ya 2000s nilikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo
katika moja ya vyombo hivi huko ulaya. Kulikuwa ni uchaguzi wa Liberia ambapo
mwanasoka maarufu, George Weah alikuwa akigombea urais wa Liberia.
Nakumbuka siku moja nikapewa habari ya kizungu
niitafsiri ili itangazwe katika Idhaa ya Kiswahili. Maelekezo kutoka kwa wenye
nchi yalikuwa "marufuku" kuanza na "Mchezaji maarufu wa soka barani
Afrika, bwana George Weah"Nilitakiwa kuanza na George Weah tu au
"mgombea ..."
Ilikatazwa kumtangaza George Weah kuwa ni
"mwanasoka bora au maarufu". Fikiria habari hiyo ilikuwa inatangazwa
kwa Kiswahili huku Afrika Mashariki. Wa Liberia hawakuwa walengwa na wala
wasingeisikia na hata kama wangesikia wasingeelewa Kiswahili. Lakini magharibi
huwa hawaachi mwanya wowote wakitaka lao!
Serikali ya nchi hiyo ambayo ndiyo wanaomiliki hicho
chombo cha Habari walikuwa wanamtaka yule Hellen Johnson aliyekuja kuwa
Rais wa Liberia baadaye ashinde uchaguzi ule. Hawakumtaka kabisa George Weah.
Nakumbuka nilihuzunika sana nilipopata yale
maelekezo. Nikamfuata mama mmoja, Mtanzania mwandishi mahiri na wa muda mrefu
pale. Nikaanza kujadiliana nae.
Nikamuonyesha ile habari na maelekezo yake.
Akacheka sana akanambia sasa unataka kufanyaje? Nikamwambia huko Afrika
tunamfahamu George Weah kama mchezaji bora na maarufu wa soka kuliko hata hivi
anavyogombea urais. Ukimtaja George Weah soka ndiyo kitu cha kwanza kinachokuja
kichwani.
Nikamwambia yaani nitasemaje tu "mgombea... au
bwana George Weah bila kutaja soka? Mama yule aliendelea kucheka sana akachukua
ile karatasi akaandika sentensi kama "mchezaji maarufu wa soka barani
Afrika, bwana George Weah...Akanambia haya kaendelee, tukacheka sana baadae
akanambia huo ndiyo uhuru wa habari wa jumba hili. kujiongeza ni muhimu. Yule
mama alinifunza jambo kubwa sana siku ile.
Ninachotaka kuzungumza leo ni kwa baadhi ya wenzetu
wenye vibarua katika haya mashirika. Hivi kuna tatizo gani kuripoti kuhusu
habari za Afrika katika mrengo chanya?
Nimeona habari kuhusu Corona katika maeneo
mbalimbali barani Afrika. Habari zote za Afrika Mashariki zinaiponda Kenya,
Tanzania na namna walivyopambana na kudhibiti Corona. Nikajiuliza sasa Afrika
ilipaswa kufanyaje masikini? Magufuli, Kenyatta wote hakuna aliyefanya zuri?
Kweli?
Waandishi wa habari wanaofanya kazi katika Idhaa
hizi zinazotutangazia moja kwa moja wangepigwa darasa la uzalendo kwa nchi zetu
ili wakifika huko wajue namna ya kushughulika na propaganda za nchi
wanakofanyia kazi.
Hatuwezi kuwalaumu kwani misimamo ya nchi hizo na
vyombo vyao ni kuhakikisha propaganda za mataifa hayo ya magharibi zinafuatwa
na kuenezwa barabara.
Kama unaendesha kipindi ukielewa fika lengo ni
kutafuta habari hasi tu unaweza kuweka hiyo hasi lakini bado ukaripoti habari
itakayokuwa chanya kwa Afrika.
Habari ya leo kwa mfano kuhusu Corona Afrika,
ni kama ilikuwa inaonyesha Kenya sasa itapata maambukizi ya Corona kutoka
Tanzania (habari hasi kwa Kenya). Bila shaka Tanzania ikajumuishwa vilevile
kuelezewa kuwa legelege katika kupambana na Corona (habari hasi kwa Tanzania
pia).
Hapa wangeweza kuendeleza ili kuifanya hiyo habari
kuwa chanya kiujumla kwa Afrika Mashariki kwa kueleza namna shughuli za malori
mpakani mwa Tanzania na Kenya zinavyoweza kupunguza kuyumba kwa uchumi katika
eneo hili la Afrika Mashariki baada ya Corona.
Mzungu angepata stori yake hasi lakini na wao
waafrika wenzetu wangekuwa wana stori yao chanya kututia moyo huku nyumbani.
Badala yake tukapelekwa Zimbabwe kuelezewa pia namna
"LOCKDOWN" inavyoonyesha kuwatesa wazimbabwe. Sasa waafrika tufanyeje
jamani?. Waliokaa bila lockdown wamekosea, waliokaa lockdown wamekosa
pia.
Ipo haja kwa serikali za Afrika kuwasomesha
waandishi wenzetu darasa la propaganda, uzalendo na mengineyo kama hayo au
kwenda full force kama mataifa kadhaa ya Asia kwa kuweka majasusi kabisa kuwa
ndiyo watangazaji na waandishi wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya
mataifa ya magharibi.
No comments:
Post a Comment