![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Murro |
NA MWANDISHI MAALUMU- ARUMERU
FURAHA ilipotea ya wananchi wa Kijiji
cha Manyire, Kata ya Mlangarini, Halmashauri ya Arusha waliokuwa
wamenyang'anywa ardhi yao na mtu aliyefahamika kwa jina moja la William, mapema
wiki hii ilirejea upya baada ya Serikali ya Wilaya ya Arumeru kuwarejea ardhi
hiyo.
Shangwe zilizoambatana na vigelegele
vya akina mama ziliibuka katika eneo ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kutatua
mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji hicho na William, baada ya Mkuu wa
Wilaya ya Arumeru (DC), Jerry Muro kutangaza kuwa ardhi iliyokuwa imetwaliwa na
Wiliam kutoka kwa wananchi hao imerejeshwa rasmi kwao na serikali.
Katika mkutano huo uliofanyika mapema
wiki hii kijiji hapo, William alitakiwa na DC Muro kuwasilisha nyaraka zake
zote zilizokuwa zikimpa uhalali wa umiliki wa ardhi lakini baada kukaguliwa na
wataalamu wa ardhi wa serikali ilibainika kuwa hakukuwa na nyraka yoyote kati
ya alizowasilisha iliyokuwa ikimpa uhalali huo.
"Nimekuja hapa ili tumalize hili
tatizo lililodumu kwa miaka mingi! Hii ni serikali makini na Rais John Pombe
Magufuli ametutuma tuje tusikilize kero zenu wananchi.
" Nimekuja, nimekagua, nimezunguka
eneo ambalo kuna mgogoro wa ardhi uliosababisha nyumba kuchomwa moto.
Tumeangalia vielelezo na nyaraka zote za maeneo ambayo Mzee William anasema ni
mali yake.
"Hakuna nyaraka hata moja
imethibitisha maeneo hayo ni mali ya Mzee William. Jinsi alivyopata hana
vielelezo na hana nyaraka yoyote inayosema maeneo hayo ni mali yake.
" Hivyo serikali imejiridhisha na
tunatamka maeneo yale ambayo wananchi walinyang'anywa na Mzee William
tumewarudishia," alisema DC Muro.
Kutolewa kwa kauli hiyo na DC Muro
kuliibua shangwe kutoka kwa wananchi na baadhi yao waliishukuru serikali ya
wilaya kwa kuumaliza mgogoro huo wa ardhi uliokuwa ukihatarisha hali ya amani
katika Kijiji cha Manyire.
DC Muro alifika kijijini hapo mapema
wiki hii akiwa amefuatana na baadhi ya wataalamu wa ardhi kukagua uharibifu
uliotokea kwenye nyumba iliyochomwa moto kwa sababu ya mgogoro wa ardhi.
Akiwa kijijini hapo DC Muro alifanya
kikao na wananchi pamoja na boma la Mzee William ambapo watalaamu wa
ardhi walipitia upya vielelezo vya umiliki wa ardhi vya kila upande na
kubaini upungufu mkubwa katika nyaraka za William.
No comments:
Post a Comment