banner

Thursday, December 10, 2020

BOSI AIRTEL ALIVYOKWAPUA MAMILIONI BILA KUBAINIKA

 



NA MWANDISHI WETU

IMEBAINIKA kuwa, mmoja wa waliokuwa maofisa wa juu wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, alichota mamilioni ya shilingi za kampuni hiyo kwa kufanya nayo biashara hewa.

Ili kufanikisha uchotaji wa mamilioni hayo, kigogo huyo ambaye jina lake tunalifadhi kwa sasa, alifungua kampuni iliyokuwa ikitoa huduma kwenye minara ya simu ya Aitel na kuweka mtu wa kuisimamia ili kuficha uhusika wake.

Uchunguzi wa awali kuhusu ufisadi wa mali za umma uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog kwa Kampuni ya Aitel umeonyesha kuwa, Airtel baada ya kubadilishwa jina kutoka Zain, kigogo huyo aliyekuwa amekwishachota pesa nyingi kwa kufanya biashara za udanganyifu, alifungua kampuni ambayo haraka haraka ilianza kupewa zabuni za Airtel.

Kwa mujibu wa uchunguzi, kampuni iliyofunguliwa ( jina tunalo) iliwekwa chini ya usimamizi wa mtu mwingine ambaye alikuwa akiripoti moja kwa moja kwa kigogo huyo na yeye alikuwa akifika kukagua mwenendo wake siku za mwisho wa wiki ambazo wafanyakazi hawakuwa kazini.

Uchunguzi umeonyesha kuwa kigogo huyo alitumia nafasi yake katika Airtel kutazama mianya ya kuiwezesha kampuni yake kupata zabuni hewa zenye thamani ya mamilioni ya fedha, jambo ambalo lingefanikiwa kampuni hiyo ingefungwa au kubadilishwa jina na iwapo ingetiliwa shaka na kuanza kufuatiliwa na mamlaka serikali, kigogo huyo angeacha kazi na kukimbilia nje ya nchi; na hiyo ingetegemea na hali halisi ya wakati ambao ingegundulika.

Tanzania PANORAMA Blog katika uchunguzi wake imebaini kuwa kigogo huyo baada ya kufanikiwa kuchomeka jina la kampuni yake kwenye menejimenti ya Airtel kama moja ya kampuni zenye sifa ya kufanya biashari kubwa, kwa kutumia wadhfa wake alianza kushawishi zabuni zenye thamani kubwa ipewe kampuni yake.

Uchunguzi umebaini kuwa haraka haraka bosi huyo aliwasilisha kwa menejimenti pendekezo la kununuliwa kwa jenereta mbili kubwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuendesha minara ya Airtel.

Pendekezo hilo liliainisha bei ya jenereta hizo kuwa; moja gharama yake ni Dola za Marekani 240,000 na ya pili Dola za Marekani 480,000 ambazo zingekaa makao makuu tayari kufanya kazi wakati wa dharura.

Mchakato wa ununuzi wa jenereta hizo ulifanyika haraka na malipo yalifanyika kwa mikupuo mitatu. Mkupuo wa kwanza ulihusisha malipo ya Dola za Marekani 480,000 ambazo zililipwa kwa invoice mbili na Dola za Marekani 240,000 invoice moja.

Hata hivyo Tanzania PANORAMA Blog inaripoti kwa uhakika kuwa manunuzi ya jenereta hizo hayakufanyika bali pesa hizo ziliwekwa kibindoni na bosi huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati akiandaa mpango mwingine wa kuchota zaidi ya Dola za Marekani 500,000 Serikali ya Awamu Tano ilianza kufuatilia mwenendo wa kampuni hiyo ili kuinusuru isife kutokana na hali mbaya iliyokuwa nayo.

"Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kufuatilia mwenendo wa kampuni kwa karibu, bosi alijua sasa atakuwa hatarini akaamua kuacha kazi mara moja kabla hajafanikisha mipango yake mingine.

"Wakaguzi wa serikali walipokuja waligundua kuwa manunuzi ya hizo jenereta yalikuwa hewa kwani hakukuwa na hizo jenereta bali hela za Airtel zilikwapuliwa zikawekwa mfukoni lakini hawakuweza kumnasa bosi kwa sababu alikuwa ameishaacha kazi.

"Na ilikuwa ngumu kumnasa kwa sababu yeye alikuwa nyuma ya ile kampuni ambayo aliweka mtu wake, huyo ndiyo akawa bosi. Huyo ndiyo alipata msukosuko kidogo lakini sasa yupo huru.

"Kwa sababu serikali ilishindwa kumbaini hakukimbilia nje ya nchi bali alikwenda nje kidogo ya jiji akajenga shule yake kubwa huko akaanzisha na biashara zake nyingine. Mke wake ambaye alikuwa mtumishi wa NSSF aliyeaacha kazi ili kusaidiana na yule bwana aliyemuweka kuendesha hiyo kampuni ya wizi sasa ndiyo anatokeza zaidi kwenye biashara zake, " kilieleza chanzo cha ndani cha taarifa.

Tanzania PANORAMA Blog itaripoti ufisadi huu kwa kina mara baada ya kukamilisha uchunguzi wake.

 

No comments:

Post a Comment