NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limewaua watu
wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya wizi toka maungoni, kuvunja
nyumba na maduka usiku na kuiba, unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa
pikipiki.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai,
imeeleza kuwa watuhumiwa hao wa uhalifu waliuawa wiki iliyopita katika eneo la Mbezi
Luis wakati wakipambana kwa risasi na polisi wa kikosi maalumu cha kupambna na
majambazi cha Mkoa wa Kinondoni.
Katika taarifa yake hiyo, RPC Kingai alieleza kuwa X.F.
407. CLP Bundala Said Kimenya na X.F. 1205 CLP
Muhidin Sadick Mhina, ambao ni askari waliofukuzwa jeshini kutokana na
matendo yao kihalifu waliuawa baada ya kukurupushwa na polisi wakijiandaa
kufanya tukio la kihalifu.
“Mnamo tarehe 26/11/2020 majira ya saa 12 jioni huko maeneo ya Kimara Luguruni, Jeshi la Polisi
Mkoa wa Kinondoni lilikuwa na taarifa fiche kuwa kuna majambazi wamepanga
kufanya uhalifu kwa kutumia silaha katika eneo la Kiluvya.
“Kikosi maalumu cha kupambana na majambazi Mkoa wa
Kinondoni kiliweka mtego eneo la Luguruni eneo la Sheli iitwayo hapa kazi tu
karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, ambapo majambazi hayo yalikuwa
yakitokea Kimara kulekea Kiluvya kupitia Morogoro Road.
“Walipofika eneo hilo wakiwa gari T 889 DKG, Toyota Brevis,
rangi ya Silver walisimamishwa na askari
polisi lakini hawakusimama, waligeuza gari yao kwa kasi kurudi walikotoka,
ndipo askari walipoanza kuwakimbiza majambazi hao ambao wakaanza kufyatua
risasi hovyo.
“Walipofika eneo la Mbezi Luis karibu na Shule ya St Anne Pr
& Sec School, askari walifanikiwa kupiga tairi risasi ambapo gari
lilipoteza mwelekeo na kuingia mtarano, jambazi mmoja aliuawa pale pale na
watatu walikimbia huku mmoja akiwa amejeruhiwa mguu,’ inasomeka sehemu ya
taarifa ya RPC Kingai.
Aidha, inaendelea kuwa baadaye polisi wakiwa katika
ufuatiliaji walijulishwa kuwepo kwa jambazi eneo la standi ya Kibo aliyekuwa
akitaka kupanda gari huku akiwa amejeruhiwa mguu ambapo askari walifika haraka
kumtia mbaroni akiwa na silaha.
Tatarifa inaeleza zaidi kuwa Mhina na Kimenya ni askari
waliofukuzwa kazi kabla ya kuuawa kutokana na matendo yao ya kihalifu na kwamba
watuhumiwa wengine wawili wanaendelea kutafutwa.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili Mloganzila.
No comments:
Post a Comment