![]() |
Katibu Mkuu Akwilapo |
NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu wa Wazara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Leonard Akwilapo amesema wajibu wa kumtafuta mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya
St Mary's, Labna Said Salim aliyepotea akiwa chini ya uangalizi wa shule ni wa
Jeshi la Polisi
Ameyasema hayo jana katika
mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilimuuliza mchango wa wizara
kumtafuta mwanafunzi huyo aliyepotea Oktoba 4, 2020.
"Hilo jambo wenye wajibu
ni polisi na ndiyo maana sisi halijafika kwetu na hata kama lingekuwa limefika
tungelipeleka polisi kwa sababu wao ndiyo wenye wajibu wa mambo kama
hayo," alisema Akwilapo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kipolisi Kinondoni, Ramandani Kingai alipoulizwa jana kuhusu hatua waliyofikia
katika msako huo alisema mpasa sasa hawafikiwa kumpata mwanafunzi huyo
Alipoulizwa kuhusu vijana saba
waliokamatwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza
ambaye jina lake limehifadhiwa, Kamanda Kingai alisema vijana hao ambao ni wanafunzi
bado wanafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne hivyo wanasubiriwa mpaka
watakapomaliza ndipo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Taarifa ya uchunguzi wa awali
wa kupotea kwa mwanafunzi huyo iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya
ya Kinondoni, Joseph Kapere ambaye ni mjumbe wa timu iliyoundwa na Serikali ya
Wilaya ya Kinondoni kuchunguza kupotea kwa mtoto huyo, mahali alipo sasa na
mazingira ya kutoweka kwake ilieleza kuwa timu hiyo ilithibitisha pasipo shaka
kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s Mbezi Makonde imepungukiwa sifa
zinazostahili kutoa elimu kwa mwanafunzi.
Wajumbe wengine katika timu
hiyo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ufisa Usalama na
Mdhibiti wa Ubora wa Elimu Kanda.
Kapere alisema tayari Mkuu wa
Shule ya St. Mary's, Recca Ntipoo amehojiwa na kuungama kutenda makosa katika
baadhi ya mambo kwenye sakata hilo na kwamba aliipeleka timu hiyo mahali
alikodai Labna alikwenda kuishi na mpenzi wake baada ya kutoroka shule.
Alisema timu ilibaini shule
hiyo ilifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto na pia
kukaa kimya siku nne bila kutoa taarifa
kwa wazazi kuhusu kutoweka kwake wala kuwajulisha kuwa amewaeleza walimu hataki
shule.
Katika maelezo yake Kapere
alisema, Ntipoo aliungama kufahamu vitendo vya mwanafunzi kutoka shule kwa
kuruka ukuta usiku na kwenda maeneo hatarishi kwao jambo ambalo Mwalimu huyo
aliliona kuwa la kawaida kwa sababu
alikuta likifanyika shuleni hapo.
Aidha, Kapere alisema timu
ilibaini shule hiyo kuwa na mazingira machafu, kukosa ulinzi wa kutosha na
kutokuwa na ukuta imara.
Alisema mambo mengine
yaliyogundulika katika uchunguzi wa timu hiyo ni kubainika kwa nyumba ya
Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Magereza ambayo ina shamba la bangi ambamo walikutwa wavulana saba, wanafunzi wa Shule
ya Sekondari ya St Mary's waliokuwa wakivuta pamoja.
Labna alitoweka akiwa chini ya
uangalizi wa shule lakini taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020
na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama
ameishafika nyumbani.
Katika hatua ya kushangaza,
uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu
kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la
mtoto wao kupotea akiwa shuleni.
No comments:
Post a Comment