NA MWANDISHI MAALUM – ARUMERU
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (DC) Jerry Muro amemtaka
mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji katika Halmashauri ya Arusha kuukamilisha
ndani ya siku 30 ili kutotoka nje ya mkataba.
Akizungumza katika eneo linapojengwa tanki kubwa la
kuhifadhi maji alikofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake, DC Murro alisema
ameridhishwa na maendeleo yake lakini mkandarasi anapaswa kuhakikisha anaumaliza
ndani ya siku 30 zilizosalia kama inavyoelekezwa kwenye mkataba.
Amesema amefanya ziara hiyo baada ya kutokea changamoto ya
kupasuka kwa mabomba kila maji yanapofunguliwa kutoka kwenye tanki kubwa
lililopo juu, changamoto ambayo imepatiwa ufumbuzi katika ziara hiyo.
“Mradi huu una thamani ya zaidi ya shulingi bilioni tisa na
tangu umeanza kutekelezwa sasa tumebakiza siku 30 kwa ajili ya mradi huu
kukamilika lakini nimeona unaenda vizuri ndiyo maana nikasema tutembee ili
tuone wapi kuna changamoto ili tuweze kuzitatua kabla ya siku 30 hizi hazijafika
tukabidhi mradi.
“Mpaka sasa nataka niwahakikishie zaidi ya asilimia 50 ya
maji yameishaingia kwenye mzunguko lakini changamoto kubwa hapa ilikuwa
kupasuka kwa mabomba. Ukifungua maji kutoka juu yakishuka mabomba yanapasuka,
sasa nikaona hapana lazima nije mwenyewe nijue kwanini yanapasuka. Leo, tumalize
ule mzizi wa fitina tujue kwa nini mabomba yanapasuka.
“Sasa tuna habari njema, moja kati ya sababu zilizokuwa
zinasababisha mabomba kupasuka ni presha ya maji kutoka juu pale mlimani kwenye
tanki kubwa kwa sababu maji yanashuika kwa kasi kwa sababu yakishuka kwa kasi
yakikuta wewe hujafungua maji yanajaa yanapasua mabomba, lakini changamoto hii
leo tumeimaliza na hamtaiona tena katika maisha yenu. Sasa tunaendelea kuongeza
mlazo wa mabomba,”alisoma DC Murro.
Mradi huu mkubwa utahudumia vijiji vitano vilivyo katika Kata
ya Ngaramtoni, Lemanyata na Oludonywasi
vyenye wakazi zaidi ya 50,000 watanufaika na unatekelezwa kwa ushirikiano wa
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Water Aid.
Katika ziara hiyo, DC Murro aliambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Arusha, Mbunge wa Arumeru magharibi, Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Arusha, wawakilishi la Shirika la Water Aid na watendaji wengine
wa serikali na mamlaka za maji.
No comments:
Post a Comment