![]() |
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Aron Kigurumjuli |
NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Aron
Kigurumjuli amesema mkandarasi aliyepewa kandarasi ya kujenga soko jipya la
Tandale, Namis Corporation LTD ni mwizi mdogo mdogo ambaye akikamatwa hurejesha
alichoiba.
Kigurumjuli aliyasema hayo wiki iliyopita katika mahojiano
maalumu na Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyikia Kinondoni Dar es Salaam.
Alikuwa akijibu kuhusu madai kuwa, mkandarasi huyo alighushi
leseni yake ya biashara na alibainika kutenda kosa hilo wakati akisaka zabuni
ya ujenzi wa soko la Tandale.
Katika majibu yake, Kigurumjuli alisema Namis Corporation
LTD haikughushi leseni ya biashara isipokuwa ilifanya udanganyifu ulioiwezesha
kuwa inalipa pesa kidogo kinyume na hitaji la leseni yake na hivyo ikawa inaiibia
serikali pesa kidogo za tozo ya leseni.
Kigurumjuli alisema, wataalamu wake walibaini kuwepo kwa
dosari hiyo kwenye leseni ya Namis Corporation LTD wakati wa ukaguzi wa nyaraka
uliofanyika kabla ya kuzawadiwa zabuni ya ujenzi wa soko la Tandale.
"Unasema inadaiwa si ndiyo? sasa mimi nakwambia madai
hayo ni uongo. Namis hajaghushi leseni ya biashara, sema, acha nikusaidie yule
alikuwa akiiba kidogo hela za serikali. Ni mwizi mdogo mdogo tu lakini
tulimbaini tukambana, akakiri tukampiga faini, akalipa.
"Alikuwa anaibaje, sikiliza. Leseni za biashara zipo
za aina nyingi sana, zipo za mpaka Dola za Marekani 200,000. Huyu leseni yake
alipaswa alipie kiwango cha juu lakini yeye akakataka ya kiwango cha chini,
akawa analipa below ya kiwango anachopaswa kulipa. Kama sikosei kwa shughuli
zake za ukandarasi alipaswa kulipa 60,000 lakini yeye akawa analipa 30,000.
" Sasa wakati wa ukaguzi wa nyaraka zake alipokuwa
ameomba tenda ya soko la Tandale wataalamu wangu wakagundua huyu anatuibia,
anaiibia serikali. Wakambana, alibishabisha kidogo lakini alibanwa haswa
akakubali kulipa.
"Tulimpiga faini kubwa. Shilingi milioni nane ya miaka
mitano aliyokuwa amefanya ujanja wake. Sasa huyu huwezi kumpa kosa kubwa hilo
la kughushi, huyu ni mwizi mdogo mdogo tu na alibanwa akalipa. Hayo mengine
sasa kamuilize mwenyewe," alisema Kigurumjuli.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Mkurugenzi wa Namis Corporation
LTD, Thomas Uiso kuzungumzia suala hilo bila mafanikio kwani tongu aliposema
mambo yote yanayohusiana na kukwama kwa ujenzi wa soko jipya la Tandale ambalo
yeye ndiye mkandarasi aulizwe Mkurugenzi Kigurumjuli amekuwa hapokei simu wala
kujibu ujumbe wa maandishi.
Tanzania PANORAMA jana lilimpigia simu Uiso hakupokea na
lilimtumia ujumbe wa maandishi kumuuliza kuhusu jambo hilo hakuujibu licha
kuonyesha umemfikia na ameusoma.
Taarifa zilizolifikia Tanzania PANORAMA Blog zilieleza kuwa
kampuni hiyo ulighushi leseni ya biashara na ilipata kandarasi mbalimbali kwa
kutumia leseni hiyo ya kughushi.
No comments:
Post a Comment