Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Pili Mazowea akimkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoanza jana katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Katikati yao ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Pichana Ofisi ya Msajili wa Hazina)
NA MWANDISHI WETU - MOROGORO
KATIBU Mkuu Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro amesema kuanzishwa kwa mfumo wa kuhifadhi
taarifa za wajumbe wa bodi za taasisi na mashirika ya umma, kutasaidia kuondoa changamoto
ya ucheleweshaji wa uteuzi wa bodi mpya.
Kwa mujibu wake, serikali
ilitoa maelekezo kwa makatibu wakuu na watendaji wakuu wa taasisi za umma kuwasilisha
katika mamlaka za uteuzi taarifa za bodi ya taasisi kukaribia kumaliza muda
wake miezi sita kabla.
“Maelekezo hayo yalikuwa na
lengo la kuhakikisha ndani ya kipindi cha miezi sita, mchakato wa uteuzi wa Bodi
uwe umekamilika. Utekelezaji wa maelekezo hayo umekuwa ukisuasua na matokeo
yake bado kuna taasisi hazipati Bodi zaWakurugenzi kwa wakati.
Naamini kwa mfumo huu unaozinduliwa
leo(jana) utaisadia Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na mamlaka za uteuzi kufanyia
kazi changamoto hiyo na kuhakikisha Bodi zinateuliwa kwa wakati,” alisema Dk. Ndumbaro.
Katibu Mkuu Utumishi
aliyasema hayo wakati akizindua mafunzo ya matumizi ya mfumo mpya wa usimamizi wa
taarifa za wajumbe wa bodi katika wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma
yanayofanyika mjini hapa, na kuandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Hivyo basi, mfumo huu utakuwa
kitendeakazi muhimu cha ofisi yako na naamini hata makatibu wakuu wa wizara wataweza
kutumia mfumo huu kupata taarifa za hali ya Bodi zilizo chini ya wizara zao, na
kushauri mamlaka za uteuzi mapema iwezekanavyo na hivyo kuondoa changamoto zinazotokana
na uchelewaji wa teuzi za Bodi,” aliongeza.
Alieleza kuwa anafahamu
kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kuzikumbushia
mamlaka za uteuzi kuhusu kumalizika kwa muda wa Bodi za Wakurugenzi katika taasisi
za umma na mara nyingi amekuwa akipata na kalaza barua hizo.
“Aidha, taasisi nyingi za umma zimekuwa zikikaa muda mrefu
bila ya kuwa na Bodi zaWakurugenzi. Kutokuwepo kwa Bodi ya Wakurugenzi katika Taasisi
husababisha maamuzi mengi katika taasisi hiyo kukwama na kupelekea uchelewashaji
wa mambo mengi ya msingi kutofanyika kwa wakati.
“Athari za kutokuwepo na Bodi
ya wakurugenzi ni pamoja na kutopitishwa kwa hesabu zilizokaguliwa, watendaji kuendelea
kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu pamoja na kuchelewesha stahili mbalimbali za watumishi,”
alisema.
Aliongeza, “Hatua za kuimarisha
usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi ni za kupongezwa na zinahitajika kuwa endelevu
ili kufikia malengo ya kuwepo kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina. Nafahamu, ofisi yako
haikuwa na mfumo ambao ungeiwezesha kufuatilia uteuzi wa Bodi kwa mamlaka za uteuzi
pamoja na taarifa nyingine za utendaji wao.”
Alimpongeza Msajili wa Hazina,
Athumani Mbuttuka kwan iutekelezaji wa mfumo huu ni matokeo ya juhudi zinazofanywa
na ofisi yake katika kuimarisha usimamizi wa utendaji wa Bodi na Menejimenti za
wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
taasisi za Umma zinakuwa na Bodi za Wakurugenzi zilizo haina kupunguza watendaji
wakuu wanaokaimu kwa muda mrefu.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro akijibu maswali ya washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzinduliwa jana na Dkt Ndumbaro katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Morogoro. Kulia ni Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka na kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Neema Musomba. Mafunzo hayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi 236 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. (Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)
Aidha, aliwashukuru wadau wa
maendeleo wanaofadhili Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
(PFMRP) kwa kuwezesha kifedha ujengaji wa mfumo huo na kuendelea kufanya kazi kwa
ushirikiano na serikali katika kuimarisha maendeleo ya nchi.
“Aidha, nawapongeza kwa dhati
vijana wetu, Watanzania wenzetu, ndani ya serikali kwa weledi wao na jitihada zao
zilizosababisha kufanikisha kujengwa kwa mfumo huu,” alisema Dk Ndumbaro na kuongeza
kuwa amefurahi kwasababu mfumo huo utasaidia kuhakikisha bodi pamoja na watendaji
wakuu wanateuliwa kwa wakati.
Awali, akimkaribisha mgeni
rasmi, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema ofisi yake kwa kutumia wataalamu
wa ndani ikishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika mwaka wa fedha
2019/20 pamoja na washirika wa maendeleo ilianzisha Mradi wa Kusimika Mfumo wa Usimamizi
wa Taarifa za wajumbe wa Bodi za Taasisi za Umma.
Alisema mfumo huu utatumika
katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, mamlaka za uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi pamoja
na wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma katika usimamiaji wa masuala
yote yanayohusu bodi hizo.
Mbuttuka alieleza kuwa Mfumo
wa Usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi (BMIS) umejengwa na wataalamu wa ndani ili kuhifadhi
taarifa za uteuzi wa wajumbe wa bodi, wasifu wao, idadi ya taasisi wanazohudumu,
aina za ujumbe wao pamoja kurahisisha utolewaji wa taarifa za bodi kwa wakati.
Alifafanua kuwa mfumo utaisaidia
Ofisi ya Msajili wa Hazina na mamlaka za uteuzi kupata taarifa mapema kuhusu bodi
kumaliza muda wake, wajumbe wa bodi wanaohudumu katika bodi zaidi ya tatu.
“Uwepo wa mfumo huu utasaidia
kuimarisha usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi katika taasisi za umma kwa kuhakikisha
taasisi hizo zinakuwa na Bodi kwa wakati. Mfumo pia utasaidia upatikanaji wa taarifa
za uhakika za wajumbe wa Bodi na kwa wakati, ushiriki wao katika vikao na pia
itapunguza urasimu wa ufuatiliaji wa uteuzi wa Bodi pale Bodi inapomaliza muda
wake.
Inategemewa kuwa uwepo wa mfumo
huu utasaidia sana kuondoa changamoto ya taasisi kutokuwa na Bodi kwa muda mrefu,
baadhi ya wajumbe Bodi kuteuliwa katika Bodi zaidi ya tatu, watendaji wakuu kukaimu
muda mrefu, usahihi wa taarifa za taasisi kuhusu hali ya Bodi na watendaji wakuu,
kuongeza ufanisi wa utendaji wa Bodi na kuzifanya mamlaka za uteuzi kupata taarifa
kwa wakati kuhusu hali za Bodi katika taasisi za umma,” alielezaMbuttuka.
Mafunzo hayo yana washiriki
708 kutoka katika taasisi na mashirika ya umma 236, na watajengewa uwezo wa kutumia
mfumo huu.
Katibu Mkuu aliwaomba kila
mshiriki kuzingatia mafunzo haya kwa umakini na kuhakikisha anauelewa vizuri.
No comments:
Post a Comment