WAKALA wa Ufundi na Umeme (TEMESA), itaanza kulipa sehemu
ya madeni ya shilingi bilioni nne wanayodai wazabuni kutokana na fedha
zilizolipwa na wizara na idara za serikali zilizotokana na agizo la Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa.
Wazabuni mbalimbali wanaidai TEMESA fedha za kusambaza
vipuli na vilainishi pamoja na kutengeneza magari ya wizara na idara za
serikali, madeni yanayofikia shilingi bilioni nne ya tangu 2012.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Mtendaji Mkuu wa
TEMESA, Dk. Stephen Massele alisema baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka
kwa wazabuni, sasa wataanza kulipa baada
ya kukamilisha upitiaji wa madeni kwa kila mzabuni.
Dk. Massele alisema baadhi ya wazabuni ikiwemo kampuni ya
Planet mawakili wao, wamekwishapewa
taarifa kwamba TEMESA inafanya mapitio ya madeni na itaanza kulipa baada ya wiki moja.
Alisema fedha zitakazolipwa zimetokana na madeni wanayodai
wizara na idara za serikali zilizopata huduma ya wazabuni hao na zitalipwa kama
ilivyoagizwa na Waziri Mkuu mapema mwanzoni mwa mwaka huu.
Dk. Masele alisema madeni mengine ya wazabuni hao,
yataendelea kulipwa kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadeni wao. TEMESA
inazidai wizara na idara za serikali kiasi cha shilingi bilioni tano.
"Baadhi ya wazabuni tumewapa maelekezo kupitia
mawakili wao, wapo waliotuelewa kuwa
tunakamilisha 'Reconciliation' ya fedha zilizolipwa kwa agizo la Waziri Mkuu
nani ana fedha ya madeni yake na ndani ya wiki moja tutakamilisha malipo yake,
" alisema Dk. Massele na kuongeza.
"Ambayo hayajalipwa hiyo watapewa taarifa na mameneja
husika mengine yatasubiri kadiri tunavyolipwa. "
Kauli hiyo ya Dk. Masele imetolewa baada ya kuwepo
malalamiko ya muda mrefu ya wazabuni kupitia viongozi wao wa Umoja wa Gereji
Tanzania (UGETA).
Akizungumza na Tanzania PANORAMA, Mwenyekiti wa Umoja wa
Gereji Tanzania (UGETA), Lumona Mkala, alisema wanachama wake wanaidai TEMESA
MT Depot zaidi ya shilingi Bilioni nne za kusambaza vipuli na vilainishi vya
mafuta ya magari.
Alitaja wazabuni wanaodai ni Beka investment shilingi 250,563,150, Moroturbo shilingi 80,256,197,
Planet Busines link shilingi 175,312,570 na Ndeken shilingi 194,801,393
Wengine ni Kigustar Enterprisess, Leonardo Automotive Garage, Nedea
Enterprisess, RaaR Investment, Kigoma Garage, Adam Motor na Point A.
No comments:
Post a Comment