NA MWANDISHI MAALUMU - OFISI YA WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama
vya ushirika wabadilike na wawe weledi ili warejesha heshima ya ushirika
nchini.
Akizungumza jana katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini
Dodoma na wakuu wa mikoa sita, makatibu wakuu, Mrajisi wa Ushirika Taifa,
warajisi wasaidizi wa mikoa, Menejimenti
ya Tume ya Ushirika, wajumbe wa Bodi za
NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd, SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi
ya Mkonge, Waziri Mkuu Majaliwa alisema viongozi wa vyama vya ushirika
wanapaswa kubadilika kwa sababu wamepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania
wanyonge.
"Viongozi wa ushirika ni lazima tubadilike. Nyie
mliopewa dhamana kwenye vyama vikuu hivi vitatu vya KNCU, NYANZA na SHIRECU
lazima mbadilike. Nyie mmepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wenzetu
wanyonge wanaolima ekari moja, mbili au tatu,” alisema.
Katika mkutano huo maalumu ambao Waziri Mkuu Majaliwa
alipokea taarifa ya ufuatiliaji wa mwenendo wa vyama vya ushirika vya NCU
(1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd na SHIRECU (1984) Ltd kutoka kwa timu maalumu ya
uchunguzi , alisema viongozi wa ushirika bado hawajabadilika kwa sababu hata
kazi ya usambazaji mbolea kwa wakulima bado ni changamoto.
Uwasilishwaji wa taarifa hiyo ulishuhudiwa na Wakuu wa
Mikoa ya Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Geita na Simiyu. Pia Makatibu
Wakuu wa Wizara za Fedha, Ardhi, Kilimo, Viwanda na Biashara.
Wengine walioshuhudia ni Mrajisi wa Ushirika Taifa,
Warajisi Wasaidizi wa Mikoa, Menejimenti ya Tume ya Ushirika, Wajumbe wa Bodi
za KNCU, NYANZA na SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge
Tanzania.
"Ninasema viongozi bado hatujabadilika kwa sababu hata
suala la usambazaji wa mbegu kwa wakulima ni changamoto. Wengine wamekuja
kujifunza ushirika hapa nchini na wamesonga mbele lakini sisi hatuendi mbali
kwa sababu ya kukosa weledi, uaminifu na uwajibikaji katika majukumu
tuliyowakabidhi.
"Nendeni mkasimamie ushirika ili heshima ya ushirika
wa zamani irejee, hali ya ushirika ule ambao uliacha mali za ushirika. Bado
kazi hizo mali haijakamilika. Tunataka tuzisimamie na tuwakabidhi kitu ambacho
kimekamilika," alisema.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema anasikitika kuona
makosa ya ushirika yanafanyika wakati warajisi wasaidizi wapo na hata kwenye halmashauri
kuna maafisa ushirika.
“Haya madudu yanafanyika lakini warajisi wa mikoa mpo na
nyie ndiyo wasimamizi wa ushirika. Je mnafanya nini?”
“Lazima uhakikishe vyama vya msingi vinasimamiwa na
vinakwenda kama ambavyo sheria yetu ya ushirika inasema. Warajisi wasaidizi
wapo kila mkoa na kila wilaya kuna afisa ushirika. Ni kwa nini mambo hayaendi?
"Hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu
anayehujumu mali za ushirika. Tulianza na tutaendelea kusimamia mali za
ushirika," alisema.
Mapema, akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu
Majaliwa, kiongozi wa timu hiyo maalumu, Asangye Bangu alisema imefanikiwa
kurejesha mali 60 za ushirika zenye thamani ya sh. bilioni 68.98.
“Mali hizo zinajumuisha majengo, viwanja, magari na mitambo
ya mashine, hazikuwa mikononi mwa vyama hivi vitatu lakini sasa zimerudishwa
kwenye vyama," alisema Bangu.
Alisema kati ya hizo, NYANZA ilikuwa na mali 37 zenye
thamani ya sh. bilioni 61.36, SHIRECU ilikuwa na mali saba zenye thamani ya sh.
bilioni 3.33, KNCU ilikuwa na mali 10 zenye thamani ya sh. bilioni 2.03 na
TCCCo ilikuwa na mali sita zenye thamani ya sh. bilioni 2.2.
Bangu alikabidhi taarifa hiyo ikiwa na mapendekezo kadhaa
kwa serikali.
No comments:
Post a Comment