SIMBA WANAJITEKENYA WENYEWE- BUMBULI
NA MWANDISHI WETU
AFISA habari wa timu ya Yanga, Hassan Bumbuli
amesema baadhi ya wanazi wa timu ya Simba wanajitekenya wenyewe kwa kusambaza
taarifa zisizokuwa sahihi katika mitandao ya kijamii.
Amesema taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya
kijamii zikidai kuwa Shirikisho la Soka (TFF) limempa siku mbili kulipa
faini ya shilingi milioni tano aliyotozwa na bodi ya ligi kwa kuingilia uamuzi
wa bodi hiyo kuhusu sakata la mchezaji Benard Morrison ni uzushi mtupu.
Bumbuli ameyasema hayo leo baada ya kuulizwa na
TANZANIA PANORAMA Blog kuhusu kusambaa kwa taarifa za kumtaka kulipa faini hiyo
ndani ya siku mbili ambayo imeibua mjadala mkali mitandaoni.
Amesema yeye hana tabia za kukurupuka kama wengine
hivyo anasubiri taarifa ya maandishi kutoka TFF ambayo pamoja na mambo mengine
itaeleza fedha hizo analizipa kwa mfumo gani na kwa muda gani.
"Uzushi wa wana Simba huo. Wanajitekenya
wenyewe. Taarifa ya uongo hiyo, sijapewa muda mimi na sijapata barua yoyote
kutoka TFF.
" Hukumu lazima iandikwe na niletewe kwa
maandishi. Niambiwe nalipa kwa muda gani na kwa mfumo gani. Simba wameona ndugu
yao kakurupuka kakimbia kaenda kulipa wanadhani na mimi ni mkurupukaji kama
huyo ndugu yao.
"Mimi nafuata taratibu, siyo sifa kama huyo
jamaa yao, unaambiwa lipa unakurupuka mbio kwenda kulipa hata hujui unapaswa
kulipa wapi hizo fedha. Na nikiletewa hukumu kwa maandishi nitaangalia kama nakata
rufaa au sikati maana hukumu inatoa nafasi ya kukata rufaa," alisema
Bumbuli.
No comments:
Post a Comment