NA MWANDISHI WETU
KWA mwaka wa pili sasa,
Watanzania wanalala usingizi ulioambatana na jonzi tatu.
Njozi hizo ni, mosi;
Wakala wa Barabara (TANROADS), pili; barabara ya juu iliyopo eneo la Tazara
inayofahamika zaidi kwa jina la Mfugale Flyover, na tatu; Mhandisi Patrick
Mfugale.
Walianza kuota njozi hizi
usiku wa kuamkia Septemba 16, 2018 baada ya kuanza kutumika kwa barabara ya juu
ya Mfugale iliyopo eneo la Tazara, Septemba 15, 2018.
Kabla ya hapo, Watanzania
hasa waliokuwa wakitumia barabara ya Julius Nyerere na Nelson Mandela, walikuwa
wanaota wamefukuzwa au kupewa barua ya karipio kali kwa kuchelewa kazini.
Wasafiri walikuwa wanaota
wameachwa na ndege au treni na wafanyabiashara waliota hasara na kupoteza saa
nyingi wakiwa katika foleni.
Ali Msafiri, mfanyabiashara
na mkazi wa eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ambaye alihudhuria
uzinduzi wa Mfugale Flyover alinukuriwa na vyombo vya habari akieleza hivi:
"Kuzinduliwa kwa
Mfugale Flyover kutaturahisishia usafiri wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na
hata wasiokuwa wakazi wanaofika katika jiji hili kubwa la kibiashara nchini
Tanzania.
"Wananchi tutakuwa
tumepata fursa na foleni na msongamano utabaki ndoto sasa. Lile tatizo sugu na
la miaka mingi la kwenda kazini sasa naona limeisha."
Watanzania wengi walikuwa
wakilala hoi kutokana na shida ya usafiri iliyokuwa ikisababishwa na foleni.
Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanaotumia barabara za Nyerere na Mandela
kwenda kazini na kurudi nyumbani walilazimika kulala kuanzia saa tano usiku na
kuamka saa 10 alfajili ili kuwahi kupambana na foleni.
Wasafiri wanaosafiri kwa
ndege au treni ya Tazara nao walilazimika kutenga muda wa hadi saa tatu za
kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam au pembezoni kwenda uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere au Stesheni ya Reli ya Tazara kwa sababu ya foleni
na msongamano wa magari.
Wafanyabiashara na
wasafirishaji wanaotumia barabara hizo walikuwa wakipoteza fedha na muda mwingi
kukabiliana na foleni na shughuli za kiuchumi kwa taifa na raia mmoja mmoja
zilikuwa zikikutana na changamoto kubwa kutokana na tatizo la foleni katika
barabara hizo.
Daniel Masanja, Dreva la
roli ambaye mara nyingi hutumia barabara ya Mandela kusafirisha mizigo
inayotoka bandarini ambaye naye alihudhuria uzinduzi huo, yeye alikaririwa
akisema hivi;
"Kulikuwa na shida
kubwa sana. Tulikuwa tunapoteza fedha nyingi sana kwa kukaa saa nyingi
barabarani, sasa tutasafirisha mizigo ya wateja na kuifikisha kwa wakati,
hakika tutaongeza tija. Tutalala tukiota njonzi njema za barabara ya juu ya
Mfugale."
Septemba 16, 2018,
wanafunzi, wafanyakazi, wafanyabiashara, wasafirishaji na wasafiri walitumia
barabara za Nyerere na Mandela kwa mara ya kwanza zikiwa hazina msongamano
baada ya kuzinduliwa kwa Mfugale Flyover.
Mfugale Flyover ni
barabara ya kwanza ya juu katika historia ya Tanzania inayounganisha sehemu kuu
za Jiji la Dar es Salaam na maeneo makuu ya kiuchumi kama Uwanja wa Ndege wa
Julius Nyerere, Bandari ya Dar es Salaam, machinjio ya Vingunguti na barabara
zinazoelekea viwandani.
Ni barabara inayojumuisha njia
kuu nne na daraja. Imetatua tatizo la msongamano na foleni na sasa imeongeza
muda wa watu kufanya kazi badala ya kutumia muda mwingi wakiwa wamekwama
barabarani kwenye foleni.
Kuanza kutumika kwa
Mfugale Flyover kumewafanya Watanzania na wageni wanaotumia barabara za Nyerere
na Mandela kulala usingizi mwororo huku wakiota ndoto ya kupita barabara ya juu
ya Mfugale kuwahi katika shughuli zao za kiuchumi, masomo na usafiri.
Hii ndiyo ndoto ya kwanza
ambayo Watanzania wanaota sasa kila walalapo usingizi.
Ndoto ya pili wanayoota
sasa Watanzania ni TANROADS. Watanzaia wanaiota TANROADS kuwa taasisi yao
iliyoshirikiana na kampuni kubwa ya ujenzi kutoka Japan ya Sumitomo Mitsui
Construction Co. LTD kujenga barabara ya kwanza ya juu iliyopewa jina la
Mhandisi Mfugale kwa mafanikio makubwa.
Wanaota maneno ya Rais wa
Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliyeitaka TANROADS kuitunza barabara hiyo na
sasa ikiwa imepita miaka miwili tangu kuzinduliwa kwake, ipo katika mwonekano
mzuri kutokana na uangalizi makini wa TANROADS.
Watanzania ambao sasa si
taifa masikini tena wanaota mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo uliosainiwa
Oktoba 15, 2015 kati ya Tanzania National Roads Agency (TANROADS) na Sumitomo
Mitsui Construction Co.,Ltd. (SMCC), lengo likiwa kuboresha makutano ya barabara
ya Nyerere na Mandela. Lengo ambalo limefikiwa.
Awali wengi walikuwa
wakiota kuwa ujenzi wa barabara za aina hiyo hautawezekana Tanzania kwa
sababu unagharimu matrilioni ya Dolla za Marekani ambayo Tanzania haina hivyo
ili kuwa na barabara ya aina hiyo ni sharti kuomba mkopo kwa wazungu.
Sasa ndoto hizo hazipo,
Watanzania wanaota shilingi bilioni 100 za kodi zao zinazokusanywa na Serikali
ya Awamu ya Tano kuwa zinaweza kujenga barabara ya juu ya kisasa kama zile
zilizoko Chicago na California nchini Marekani na wakiamka wanapita kwenye
barabara ya aina hiyo.
Ni ndoto iliyosubiriwa
tangu Aprili 16, 2016, siku ambayo Rais Magufuli alizindua ujenzi wa barabara
hiyo ya juu.
Ndoto ya tatu inamuhusu
Injinia Patrick Mfugale ambaye mchango wake katika ujenzi wa daraja hilo
utabaki kuwa kielelezo cha Mtanzania mzalendo aliyetumia vema elimu yake
kulinufaisha taifa lake.
Watu walio karibu pamoja
na wasaidizi wake wanaeleza kuwa Injinia Mfugale ni mkali kwa watu wanaomsifia
yeye binafsi hata kama anastahili kusifiwa. Anapenda sifa zinazomstahili
zielekezwe kwa serikali anayoitumikia, taifa na Watanzania.
Kwa sababu ya ukali wake
huo, Watanzania wamebaki kuuota uzalendo, utaalamu na uadilifu wake ndotoni.
Haina shaka sifa zake nyingi zitatolewa hadharani na bila kuogopa katazo lake
atakapokuwa hayupo.
Lakini kwa sababu katazo
lake hilo siyo sheria hivyo haliifungi Tanzania PANORAMA Blog kumtendea haki,
linafuata nyayo za Rais Magufuli ambaye kwa kuutambua mchango wake katika
ujenzi wa barabara hiyo na utumishi wake uliotukuka kwa taifa alimpa heshima ya
juu kwa kuiita kwa jina lake.
Dunia sasa inapaswa
kumtambua Mhandisi Patrick Mfugale kuwa mtaalamu wa kwanza wa fani ya uhandisi
duniani aliyetumia utaalamu wake kujenga sehemu kubwa ya miundombinu ya barabara
na madaraja ya taifa lake.
Kumbukumbu za kazi za
kihandisi zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog mpaka sasa zinaonyesha kuwa
rekodi ya Mhandisi Mfugale ya kusaidia kujenga madaraja 1400 katika nchi ya
baba na mama zake haijafikiwa na mhandisi mwingine yeyote duniani.
Rekodi zinamtaja pia
Mhandisi Mfugale kuwa mtaalamu wa kwanza wa fani ya uhandisi duniani ambaye
baada kupata elimu ya juu ya uhandisi nje ya nchi hakulikimbia taifa lake
kwenda kufanya kazi ughaibuni ambako wahandisi hulipwa mishahara minono, bali
alirejea kulijenga na mpaka sasa amebuni na kusimamia barabara za Taifa la
Tanzania zenye urefu wa zaidi ya kilomita 36,258.
Kwa mujibu wa rekodi za
kihandisi zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog, Mhandisi Mfugale ndiye pekee
duniani mpaka sasa aliyetoa mchango mkubwa kwa nchi yake katika ujenzi wa
miundombinu ya barabara.
Watanzania wanaoota
taswira ya Patrick Mfugale kila wanapopita juu ya Mfugale Flyover wanapaswa
kukumbuka maneno yake mbele ya Rais Magufuli siku ya ufunguzi wa barabara hiyo
ili yawajengee uzalendo, unyenyekevu katika utumishi na uwajibikaji, aliposema;
"Ukiwa waziri wa
ujenzi ulinituma Japan kwenda kuweka sahihi mkataba wa kazi hiyo, lakini
tulikuwa hatujapata mkandarasi na ulinielekeza kuwa nisirudi huku mpaka niwe
nimesaini mkataba.
"Na nilipoiambia
Japan nimeambiwa na nchi yangu nisirudi, wakasema viza yako imeisha, kwa hiyo
ni lazima urudi, nikasema ninaweza nikakaa hata railway stesheni, ili mradi
kama mkimbizi lakini tenda hii tutafute namna ya kufanya daraja hili lijengwe,"
Mtu huyu Mhandisi Patrick Mfugale
alizaliwa mkoani Iringa na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi
ya Consolata ya mjini Iringa na 1975 alihitimu elimu yake ya shule ya upili
katika shule ya upili mkoani Moshi.
Mwaka 1977, Mfugale
aliajiriwa Wizara ya Ujenzi kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Rocky nchini India
ambako alihitimu mwaka 1983 na kutunukiwa shahada yake ya kwanza ya
uhandisi kisha akarejea nchini kuja kulijenga taifa lake
Mwaka 1991 Mhandisi Mfugale alisajiliwa kama mhandisi
mtaalamu na mwaka 1992 aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa.
Mwaka 1994 hadi 1995 alikwenda ughaibuni kusoma katika Chuo
Kikuu cha Loughborough, Braunshweig nchini Uingereza ambako alihitimu ya
kutunukiwa shahada yake ya pili ya uhandisi na kisha akarejea tena nchini
kuendelea kulijenga taifa lake.
Mwaka 1995 aliteuliwa kuwa mhandisi mkuu wa madaraja
nchini Tanzania na wakati huo huo akiwa masomoni nchini Uingereza alitafiti na
kutengeneza mfumo wa madaraja nchini Tanzania.
Mhandisi Mfugale alibuni Daraja la Magarasi lenye mita 178
lililogharimu shilingi za Tanzania milioni 300 na pia, kwa uchache amejenga
Daraja la Mkapa Rufiji, Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbuji,
Daraja la Rusumo, Daraja la Kikwete na Daraja la Nyerere huko Kigamboni
No comments:
Post a Comment