![]() |
Labna Said |
NA MWANDISHI WETU
LABNA Salim Said, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Bweni ya St. Mary’s iliyopo Mbezi Makonde ambaye alipotea tangu Oktoba 4, 2020,
amepatikana.
Mwanafunzi huyo alipatikana Disembe 12, 2020, eno la Banana
Relini akiwa amewekwa kinyumba na mwanaume ambaye jina lake halikufahamika mara
moja baada ya kufanikiwa kuwakimbia polisi waliokwenda kuwakamata.
Taarifa za kupatikana kwa Labna zilithibitishwa na Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC) Ramadhani Kingai katika mahojiano
mafupi kwa njia ya simu ambaye alisema, taarifa za kupatikana kwa mwanafunzi
huyo anazo lakini hawezi kuongea zaidi kwa sababu yupo kwenye kikao.
Mama mzazi wa Labna anayefahamika kwa jina la Rabia Swedan
alisema walipata taarifa za kuwepo kwa mtoto wao eneo Banana Relini usiku na
walifika eneo hilo wakiwa wameambatana na polisi wawili na kumkuta akiwa
amelala chini pamoja na aliyemtorosha.
“Inasikitisha, tulipata taarifa za huyu mtoto kuwepo Banana
Relini usiku, tukaenda Kituo cha Polisi Stakishari kuomba polisi, tukapewa
wawili tukaambatana nao mpaka kwenye hiyo nyumba tukawakuta wamelala chini.
Yule bwana aliyekuwa naye alipotuona na polisi akakurupuka akakimbia, sasa kwa
sababu polisi walikuwa wawili hawakuweza kumfukuza.
“Mtoto alikuwa hoi, tulimpeleka Stakishari polisi huo usiku
wa saa saba akakaa hapo wakimuhoji mpaka saa 12.00 asubuhi, kwa jinsi alivyokuwa
wakatuambia tumpeleke hospitali.
“Tukampeleka Hospitali ya Amana na baada ya matibabu
tukamchukua hadi Kituo cha Polisi Goba kwa sababu ndiko kesi yake
inakopelelezwa, nao wakamuhoji wakaturudishia tuendelee kumtibu ila akiwa
na nafuu tutampeleka tena polisi,” alisema Swedan.
Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya
St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na
kutokomea kusikojulikana hadi alipopatikana Disemba 12.
Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini
taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra
aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.
Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari
ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na
badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.
No comments:
Post a Comment