![]() |
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi- Mawasiliano, Pascal Shelutete |
NA MWANDISHI MAALUM – ARUSHA
MAMLAKA ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), imeshinda tuzo ya
dhahabu ya kimataifa ya utoaji huduma bora kwa mwaka 2020 inayotolewa na
Taasisi ya European Society for Quality Research (ESQR).
Taarifa ya ushindi huo imetolewa leo na Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano, Pascal Shelutete ambaye ameeleza kuwa
tuzo hiyo itakabidhiwa kwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jesta Nyamanga,
wiki ijayo, jijini Brussels.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamishna
Shelutete ameeleza kuwa TANAPA imeibuka mshindi miongoni mwa washindani 51
kutoka nchi 39 duniani.
“Tuzo za ESQR za huduma bora hutolewa kila mwaka na Shirika
la ESQR kwa kutambua taasisi za serikali na zisizokuwa za kiserikali pamoja na
watu binafsi wanaotoa huduma za viwango ya juu. Washindi wa tuzo hii
huchaguliwa kwa kuzingatia matokeo ya kura zilizopigwa na taasisi zilizoshinda
tuzo hizo awali, maoni ya wateja na utafiti wa masoko.
“Mchakato wa upatikanaji wa washindi wa tuzo hii
unajumuisha utafiti wa taarifa mbalimbali kwa umma, machapisho, maoni chanya ya
wateja, miradi ya kijamii na vyuo vikuu pamoja na maonyesho,” inasomeka sehemu
ya taarifa ya Kamishna Shelutete.
Anaandika zaidi kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya mikakati
madhubuti ya TANAPA katika kuhifadhi rasilimali za hifadhi pamoja na mrejesho
chanya kutoka kwa wateja wa kitaifa na kimataifa.
“Utambuzi huu utakuwa chachu ya kuendelea kuongeza jitihada
za uhifadhi endelevu wa hifadhi zetu na kutangaza vivutio katika masoko
mbalimbali na kuendelea kuboresha huduma za utalii,” inasomeka.
Taarifa hiyo inahitimishwa na wito kwa umma, taasisi za
kitaifa na kimataifa na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano kaktika
kuhifadhi rasilimali za hifadhi ya taifa na kuunga mkono juhudi za kukuza
utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
No comments:
Post a Comment