*Wamo Mwenyekiti wa Vijana wa Mkoa, Naibu Katibu
Mkuu Tanzania Bara,
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha
Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa leo amewapokea wanachama 20 kutoka Chama cha
Demokrasia (CHADEMA) ambao wameamua kurudi CCM.
Wanachama hao wameongozwa na Mwenyekiti wa Vijana wa
CHADEMA wa Mkoa wa Kagera, Francis Mutachunzibwa ambaye pia alimtambulisha
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa BAVICHA, Getrude Ndibalema ambaye alijiuzulu
uongozi tangu mwaka jana.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mutachunzibwa
amesema: “Ninaijua vizuri CHADEMA, nilipotea, nilitenda dhambi lakini sasa
nimeamua kurudi nyumbani, nipokeeni.
“Ninawaomba wana-Bukoba tumchague Dk. Magufuli,
mashine ya kusaga na kukoboa, jembe la nguvu. Kuanzia kesho, nitamnadi yeye na
Advocate Byabato hadi kieleweke," amesema.
Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba leo
jioni, waliojitokeza kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya
Bukoba, mkoani Kagera, Majaliwa aliwataka wakazi hao wajitafakari sana
wanapofikiria kumchangua mtu wa kuongoza nchi.
“Tunataka kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ili
umpate ni lazima umjue historia yake. Kuongoza nchi si lelemama, kiongozi wa
nchi ni Mkuu wa Nchi, tena ni Mkuu wa Majeshi," amesema Majaliwa.
Majaliwa ambaye ameanza ziara katika Mkoa wa Kagera
kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli,
ametumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Bukoba Mjini kwa
tiketi ya CCM, Wakili Steven Byabato, mgombea udiwani wa Kata ya Bilele, Tawfiq
Sharif Salum na madiwani wengine wa jimbo hilo.
Aliwasimamisha wazee wa Kagera wakiwemo aliyekuwa
Meya wa Bukoba, Dk. Anatoly Amani, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Balozi
Khamis Kagasheki ambao wote waliomba kura za Dk. Magufuli, Wakili Byabato na
madiwani wa jimbo hilo.
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Viwanda,
Charles Mwijage, amesema Muleba wana ajenda ya kuhakikisha kura zote zinaenda
kwa Dk. Magufuli na wabunge wa CCM na akawataka wana-Bukoba nao wafanye hivyo
ili kuhakikisha majimbo yote tisa yanabakia CCM na pia wanapata wabunge wanne
wa viti maalum.
No comments:
Post a Comment