NA PIUS NTIGA, MOSHI
TANZANIA imesifiwa kuwa ina sera nzuri ya uwekezaji
ambayo imekuwa kichocheo cha upatikanaji wa ajira na ukuaji wa uchumi.
Hayo yameelezwa leo na mwekezaji Fons Nijenhuis
katika mahojiano na Amzha Amsha 2020 ya Uhuru FM shambani kwake Dakau, Wilaya
ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ameema zaidi ya ekari 250 zinatumika katika
uwekezaji wa sh bilioni 6 tangu mwaka 2003 na kufanikiwa kutoa ajira kwa
Watanzania zaidi ya 1,000 katika shamba la maua la Vasso.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya Mwaka 2015/2020 iliyoahidi kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji
kama njia moja wapo ya kuongeza ajira kwa Watanzania
Fons Nijenhuis, amesema uwekezaji huo umetoa ajira
kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na pia umesaidia kuchangamsha eneo hilo
kibiashara na hivyo kuinua Uchumi.
Aidha, amesema amefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi
wanozunguka shamba hilo ambao miongoni mwao wameanzisha kilimo cha maua
wanayoyauza kwake.
"Ngoja nikwambie hapa mimi nimefanikiwa
kufundisha ujuzi wananchi wapo kama 40 hivi hawa wote wana mashamba hapo nje na
maua yao huwa wananiuzia mimi na huwalipa kiasi cha shilingi milioni kama moja
hivi kila wiki wanaponiuzia" anasema Mwekezaji.
Kwa mujibu wa mwekezaji huyo kila wiki husafirisha
zaidi ya tani 250 za miche ya maua nje ya nchi na sehemu ya fedha zake hutumika
pia kufanya ukarabati wa huduma katika vijiji vitatu vinavyozunguka shamba
hilo.
Amesema katika shamba hilo anatumia tani 500 za
udongo ambazo huziagiza kutoka nchini Uholanzi na kwamba udongo wa hapa nchini
hautoshelezi.
Aidha, amesema anaendelea kufanya mazungumzo na
serikali ili kuangalia uwezekano wa kuwa anatumia udongo wa hapa nchini ambao
unapatikana Wilaya ya Pangani, Mkoa waTanga ili pesa anayotumia kuagiza nje
udongo ibaki hapa hapa nchini.
"Sehemu kubwa ya wateja wangu wapo nchini China
na Uholanzi ambako huuza hii Miche ya Maua," alisema
Kwa upande wake, Afisa Kilimo Halmashauri ya Moshi
Vijijini, Mercy Urio amesema uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa kwa jamii na
Halmashauri ya Moshi vijijini na wananchi kwa ujumla wanajivunia uwepo wa
mwekezaji huyo.
Nao wanufaika wa uwekezaji huo, Agnes Shofa, Justina
Mushi pamoja na Benard Erasto wamesema kwa sasa maisha yao yamebadilika
ukilinganisha na awali walivyokuwa kwani wamefanikiwa kuboresha makazi yao kwa
kujenga nyumba mpya.
Naye meneja wa shamba hilo, Alany Njau, amevitaja
vijiji vitatu vinavyonufaika na uwekezaji huo kuwa ni pamoja na kijiji cha
Umbwe, Ucharo pamoja na Dakau na wamekuwa wakifundisha ujuzi kwa wananchi wa
namna ya kupandikiza pia Vikonyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaj
Rajab Kundya, aliambatana na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru Fm, katika shamba hilo
amesema mafanikio yote yamepatikana kutoka na uongozi thabiti wa Rais Dk. John
Magufuli na kusisitiza kuwa chanda chema huvikwa Pete.
Aidha, mkuu huyo wa Wilaya ya Moshi, amesema shamba
hilo la maua ni moja ya mashamba 11 yaliyopo katika wilaya hiyo na
yameendelezwa vizuri kupitia vyama vya ushirika.
"Kuna changamoto kadhaa ambazo hujitokeza kwa
mwekezaji huyo lakini tumekuwa tukikaa pamoja kuzitafutia ufumbuzi wa
kina"Amesema DC wa Moshi.
Amesema wanafarijika kuona maendeleo ya kilimo cha
umwagiliaji na kilimo cha kutumia mvua kinapitwa na wakati na serikali
inahakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa vizuri ili kuleta chachu katika
kilimo cha Umwagiliaji.
Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya
mwaka 2020 /2025 imeahidi kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika kilimo cha
Kisasa cha biashara hususani ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji.
No comments:
Post a Comment