NA MWANDISHI WETU
RAIS John Pombe Magufuli ndiye mtu pekee
mwenye uwezo wa kiungozi kati ya wote waliojitokeza kugombea urais katika
uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Hayo yameelezwa jana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Kata za Lubuga
na Ilungu zilizopo Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.
Waziri Mkuu Majaliwa yupo katika ziara ya kisiasa ya
nchi nzima ya kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais Magufuli na amekuwa akitumia
majukwaa ya kisiasa kuwanadi pia wagombea ubunge na udiwani wa CCM.
"Rais Magufuli anastahili kupewa nchi kwa
sababu ana uwezo wa kuisimamia. Tanzania imekosa maendeleo ya haraka kwa sababu
kulikuwa na tabia ya watu wachache ya kula rushwa na kuwaathiri wananchi wa
chini wasipate mafanikio. Tunataka kiongozi wa nchi anayeweza kupambana na
rushwa na mafisadi. Na huyo ndiye kiongozi tunayemtaka," alisema Waziri
Mkuu Majaliwa.
Alisema chini ya uongozi wa Rais Magufuli, sera ya
tiba kwa akinamama wajamzito na watoto na wazee ni bure. Huduma ya mama
mjamzito kujifungua ni bure na kwamba Serikali ya Rais Magufuli imekwishatoa sh
bilioni 10.8 kwa ajili ya huduma hizo.
" Tunayo Bima ya Afya ambayo tunataka
tuiimarishe ili iwe ya kitaifa. Na leo tayari tunao muswada wa Bima ya Afya,
tunataka tuunganishe wafanyakazi na wananchi wa kawaida ili watanzania wote
wawe na Bima ya Afya.
"Si kila mara mtu anakuwa na pesa taslimu
wakati anapopata mgonjwa kwenye familia na ndiyo maana inasisitizwa
Watanzania wote wawe na Bima ya Afya.
" Unapata kadi wewe na mkeo au mumeo na
wategemezi wanne. Leo tuna watoto wanatoka Magu lakini wanasoma Chuo Kikuu cha
Dodoma. Una mtoto yupo hapa lakini anasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, una mtoto
mwingine anasoma Bwiru, akiugua huko na kuulizwa kitambulisho anatambulika kuwa
ni mtoto wa fulani, anatibiwa.
"Haya yote niliyoyasema yamefanyika katika
kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Dk Magufuli na ndiyo sababu leo
namuombea kura ili awe Rais wa nchi hii," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aliongeza kuwa Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh
bilioni 1.4 kwa Wilaya ya Magu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya .
Alisema kituo cha Afya cha Kahangara kimepata sh
milioni 500 na ujenzi wake umekamilika, kituo cha Afya Lugeye kimepata sh
milioni 500 na ujenzi wake umekamilika na Kituo cha Afya Kabila kimepata sh
milioni 400 na ujenzi wake upo katika hatua za mwisho.
Akizungumza kuhusu fedha za ununuzi wa dawa, Waziri
Mkuu Majaliwa alisema Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh bilioni 10.1 kwa
ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba kila mwezi Wilaya ya Magu
inapokea wastani wa sh milioni 108.
Kuhusu ujenzi wa barabara, Waziri Mkuu Majaliwa
alisema Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh bilioni 10 kupitia TARURA na
TANROADS kwa ujenzi, matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi na
madaraja kwa barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwemo ujenzi wa
barabara ya lami ya Magu mjini yenye urefu wa kilomita 5.7 ambayo tayari
imekamilika ikiwa imegharimu sh bilioni 2.7
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni Kisesa - Bujora
yenye urefu wa kilomita 0.4 ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami, barabara ya
Usagara - Kisesa yenye kilomita 16.14 kwa kiwango cha lami na usanifu wa kina
wa barabara ya Magu - Ngudu - Hungumalwa yenye urefu wa kilomita 70.
No comments:
Post a Comment