banner

Friday, September 25, 2020

DMO MANYONI ASEMA UJENZI ZAHANATI YA NTOPE HAUJAKAMILIKA TANGU 2012

 

Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Ntope  kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida ambalo ujenzi wake ulianza 2013. Mradi huu unadaiwa kughubikwa na vitendo vya ufisadi

NA MWANDISHI WETU

MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Manyoni (DMO) Furaha Mwakafula amesema ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya  ya Manyoni mkoani Singida haujakamilika kwa miaka minane sasa kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwakafula ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na TANZANIA PANORAMA kuhusu kukwama kwa ujenzi wa zahanati hiyo na madai ya ufisadi dhidi ya fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi huo.

Amesema mbali na zahanati hiyo, ujenzi wa nyumba ya daktari wa kijiji ulikamilika na ilianza kutumiwa na mtumishi ambaye hakuwa wa kada ya afya aliyepewa na uongozi wa kijiji.

"Taarifa nilizonazo mimi ni kwamba ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2012, katika bajeti ya mwaka 2012/2013 zilitolewa sh milioni 20 zikatumika kujenga sehemu ya boma ambalo halikukamilika na tangu wakati huo haijatolewa fedha nyingine. Kwa hiyo ujenzi umekwama kwa miaka yote hiyo kwa sababu ya ukosefu wa fedha," alisema Mwakafula.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa zilitolewa sh milioni 60 ila zilizoelekezwa kwenye ujenzi ni sh milioni 20 huku sh milioni 40 zikihamishiwa kwenye fungu lisilojulikana na hazijapata kurejeshwa hadi sasa alisema hizo zinaweza kuwa hisia za watu au upotoshaji wa makusudi.

"Kuna mambo mawili hapo ambayo ni vizuri yaeleweke, moja ni kwamba kuna fungu la fedha kutengwa kwenye bajeti na kuna fungu la fedha husika kupelekwa na kupokelewa kwenye mradi. Sasa mimi nimethibitishiwa na wataalamu wa mipango kuwa fedha iliyotolewa na kutumika kwenye mradi huo ni sh milioni 20 tu," alisema Mwakafula.



Aidha mganga mkuu huyo alisema mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba ya daktari ulioanza sambamba na zahanati ya Ntope ulikamilika na uongozi wa Kijiji cha Ntope uliitoa nyumba hiyo itumiwe na mtumishi wa serikali ambaye hakuwa wa kada wa afya hadi ilipoharika paa.

"Kuhusu nyumba ya daktari yenyewe ilikamilika na uongozi wa kijiji uliitoa kwa mtumishi ambaye hakuwa wa kada ya afya. Huyo aliitumia hadi ilipoezuka paa lake. Hivi sasa ndiyo tunafikiria kuitengeza ili ianze kutumika kama zahanati ya kijiji," alisema.

Aidha, Mwakafula alisema taarifa kuwa zahanati ya Kijiji cha Ntope ambayo haijawahi kutoa huduma hupewa mgao wa dawa kutoka MSD ni za kweli na dawa hizo huwa zinaelekezwa zahanati za jirani ambazo zinawahudumia wananchi wa Kijiji cha Ntope.

" Hilo kweli fungu la fedha za dawa katika zahanati ya Ntope huwa linatoka kila mwaka lakini kwa sababu haipo fedha hizo huwa zinaelekezwa zahanati za jirani ambazo zinatoa huduma kwa wananchi wa Kijiji cha Ntope," alisema.

Daktari Mwakafula amefanya mahojiano na TANZANIA PANORAMA na kutoa ufafanuzi huo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Jackson kueleza kuanza kuwa anafuatilia madai ya ufisadi katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope.

No comments:

Post a Comment