NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa kivuko
kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.
Ahadi hiyo imetolewa jana (Ijumaa, Septemba 25,
2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa
katika mkutano wa kampeni uliofanyika kitongoji cha Gana.
Katika mkutano huo, Majaliwa alimnadi mgombea ubunge
wa Jimbo la Ukerewe kupitia tiketi ya CCM, Joseph Mkundi na madiwani. Pia
Majaliwa aliwataka wananchi wa Gana wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM,
Dk. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao wa urais, wabunge na madiwani
utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Akitoa ahadi hiyo mbele ya wananchi wa kisiwa cha
Gana, Majaliwa alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2020-2025 yenye kurasa 303. Kivuko hicho kitatoa huduma kati ya Kakuru na
Gana.
Alisema Ilani ya CCM imetoa maelekezo kwa Serikali
ijayo itekeleze idadi kubwa ya miradi ya kimkakati ikiwemo kuboresha usafiri wa
majini ili kuwandolea adha wananchi wanaoishi katika maeneo ya
visiwani.
Majaliwa alisema wananchi zaidi ya 3000 wa Gana, wanahitaji
kivuko bora ambacho kitatoa fursa kwao kufanya shughuli za uvuvi na biashara
ili kujipatia kipato.
"Hapa Gana tutaleta kivuko, hiki kisiwa ni
kikubwa kina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma bora ya usafiri wa
majini. Serikali yenu imeweka mipango mizuri kwa ajili yenu," alisema
Majaliwa.
Alisema chama kitaendelea kutekeleza Ilani yake kwa
vitendo kwa kuboresha huduma za wananchi katika visiwa vyote nchini ikiwemo
wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza yenye visiwa 38.
Mbali na kutoa ahadi ya kivuko, Majaliwa alisema
Serikali ijayo itapeleka boti za doria kulinda usalama wa wavuvi ambao wakati
mwingine wanafanya shughuli zao kwa mashaka wakihofia uvamizi wa majambazi
wanaotoka nchi jirani.
Kwa upande wake, Mkundi alisema kipaumbele cha
kwanza baada ya kuingia bungeni ni kuhakikisha Serikali ijayo inaboresha huduma
ya afya kwa kujenga idadi kubwa ya zahanati ndani ya kisiwa hicho.
"Gana tuna changamoto ya zahanati, umeme na
maji. Nitakuwa daraja zuri kati yenu na Serikali ili kuhakikisha huduma hizi
zinawafikia kwa haraka naomba mumchague Rais Magufuli ili mambo yetu yaende
vizuri," alisema Mkundi.
Paschal Bukuru ambaye ni mfanyabiashara ya duka,
alisema ujio wa kivuko utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Gana, kwa kuwa muda
mrefu wamekuwa wakitumia mitumbwi kwenda Nansio kufuata mahitaji.
Bukuru alisema wafanyabiashara wamekuwa wakipata
changamoto ya kuleta bidhaa zao wakitokea Nansio kwa kuwa hawana usafiri wa
uhakika, hivyo ujio wa kivuko hicho utakuwa na manufaa makubwa kwao.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM imeahidi
kuboresha vivuko ikiwemo ujenzi wa kivuko cha Rugezi-Kisorya (Mwanza). Pia
ujenzi wa vivuko vipya vinane utaanza ambao ni Ijinga-Kahangala (Mwanza),
Musoma-Kinesi (Mara), Nyamisati-Mafia (Pwani), Msangamkuu-Msemo (Mtwara), Nyakalilo-Kome
(Mwanza), Bwiro-Bukondo (Ukerewe), Irugwa-Murutanga (Ukerewe) na Kakuru – Ghana
(Ukerewe).

No comments:
Post a Comment