*Ampokea aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Kyerwa wamchague
Dk. John Pombe Magufuli kuwa rais kwa sababu anatoka katika chama ambacho kina
mikakati inayotokana na mawazo ya wananchi.
"Dk. Magufuli anatoka kwenye chama ambacho kina
utaratibu katika kuendesha nchi, chama ambacho kina ratibu kero za wananchi,
ambacho kinasikiliza wananchi mpaka ngazi ya chini," amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Septemba 29, 2020)
wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkwenda, akiwa njiani kuelekea Isingiro
wilayani Kyerwa, mkoani Kagera.
"Tumemjaribu na amefanya mambo makubwa katika
wizara alizoziongoza na ndiyo maana namleta kwenu Dk. Magufuli na kumuombea
miaka mingine mitano ili alete maendeleo zaidi," amesema.
Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura
mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi
mgombea ubunge wa Jimbo la Kyerwa, Innocent Bilakwate, mgombea udiwani wa Kata
ya Nkwenda, Edward Katunzi na wagombea wa CCM wa kata za jirani.
Amesema CCM ni chama kinachoongozwa na Ilani ya
Uchaguzi na kuna mambo yamethibitika katika ilani inayoishia 2020.
"Leo tunaleta kitabu kingine cha Ilani ya 2020
- 2025. Kama tuliweza kufanya makubwa ndani ya miaka mitano na kile kitabu
kidogo, je huko tuendako itakuwaje?" amesema.
Akiwa Isingiro kwenye mkutano wa hadhara,
Majaliwa amesema serikali ilibadilisha sheria tangu mwaka 2017 na ikazuia
uuzaji wa madini ya bati nje ya nchi kwa kutumia njia za panya.
"Sheria inatutaka tutenge ekari kadhaa kwa
ajili ya wachimbaji wadogo. Leo hii ekari 38,000 zimetolewa kwa wachimbaji
wadogo wa madini mbalimbali. Pia tumeanzisha masoko ya madini 26 na vituo
vidogo 28 vya kuuzia madini," amesema.
Akifafanua kuhusu vitambulisho vya Taifa,
Majaliwa amesema Tanzania ni nchi ya amani na wengi wanatamani kuja kuishi
nchini.
Amesema Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Missenyi ni za
mipakani kwa hiyo zina changamoto za uhamiaji na masuala ya kiraia.
"Ndiyo maana serikali inakuwa makini katika
uhakiki. Tutaimarisha usimamizi ili kila Mtanzania apate kitambulisho,"
amesema.
Pia amewaonya maafisa wanaohusika na utaoaji
vitambulisho vya uraia ambao wanapokea hongo na kuwapa vitambulisho hivyo watu
wasiostahili.
Wakati huohuo, Majaliwa amempokea
aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Karagwe kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Princepius Rwazo ambaye ameamua kurejea CCM.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rwazo amesema
alikuwa mgombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliopita na aliisumbua sana CCM
lakini sasa ameamua kurejea kwani ameona mazuri yanayofanywa na chama hicho.
"CCM imejibu kiu zetu, kimekuwa kama chama cha
upinzani, na wapinzani sasa wamelala. Nimerudi CCM, sihitaji cheo chochote,
shida yangu ni kujiunga na watu wanaochapa kazi. Nitamuunga mkono Dk. Magufuli
na ndugu yangu Bashungwa," amesema na kushangiliwa.
Majaliwa anaendelea za ziara yake katika Wilaya za
Karagwe na Missenyi.
No comments:
Post a Comment