NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI mbili za ujenzi za China, China Road and
Breadge Corporation (CRBC) na SCG Overseas Tanzania Company Limited zinadaiwa
kufanya biashara inayoziingia mabiilioni ya shilingi ambayo hayatozwi kodi.
Sambamba na biashara hiyo inayoyaingizia utajiri
mkubwa lakini unaofubaza fuko la fedha zikusanywazwo na Mamlaka ya Mapato (TRA)
kama kodi, Kampuni ya CRBC imekusanya na kutia kibindoni mamilioni ya fedha
ilizokuwa ikiwakata wafanyakazi wake kama malipo ya pensheni.
Taarifa za uhakika zilizoifikia TANZANIA PANORAMA
zimedai kuwa SCG Overseas Tanzania Company Limited ambayo iliingia nchini kwa
ajili ya kujishughulisha na ujenzi wa barabara na madaraja ilipewa
msamaha wa kodi wa vifaa vyake vya ujenzi.
Inadaiwa kampuni hiyo ambayo sasa imemaliza shughuli
zake hapa nchini, imekuwa ikikodisha vifaa ilivyokuwa ikitumia kwa shughuli
zake za ujenzi vikiwa na msamaha wa kodi kwa Kampuni ya CRBC ambayo
huilipa mamilioni ya fedha.
Taarifa zaidi zilizokusanywa na TANZANIA PANORAMA
zimeonyesha kuwa biiashara kati ya kampuni hizo mbili, licha ya kuwa yenye
thamani kubwa, risiti zinazotolewa kuthibitisha kufanyika kwa malipo
hazitambuliki kwenye mfumo rasmi wa kikodi wa hapa nchini.
"Hawa wachina wa hizo kampuni mbili wanafanya
biashara ya mabilioni kwa kukodishiana vifaa na mitambo ya ujenzi. Kiukweli
wanaoga fedha hapa Dar as Salaam," alisema mmoja wa watoa taarifa.
Wakati huo huo, CRBC inadaiwa kuweka katika fuko
lake ya fedha mamilioni ya shilingi waliyokuwa wakikatwa wafanyakazi wake kama
malipo ya pensheni.
Katika mahojiano kati ya badhi ya wafanyakazi wa
kampuni hiyo na TANZANIA PANORAMA huku wakiwa na nyaraka zao za malipo ya
mshahara mkononi (salary slip) wamedai kwa zaidi ya mwaka mmoja walikuwa
wakikatwa pesa katika mishahara yao kwa ajili ya pensheni lakini baada ya
mikataba yao ya kazi kuisha wamebaini kuwa fedha hizo zilikuwa haziwasilishwi
kwenye mifuko ya jamii.
Alipoulizwa Meneja Rasilimali Watu wa CRBC Alice
Charles kuhusu madai hayo alikubali kuzungumzia suala ya malipo ya pensheni
huku dai la kuwepo biashara baina ya CRBC na SCG alisema hilo kwake ni
zito na anayeweza kulisemea ni bosi wake aliyemtaja kwa jina moja la Zhang.
Alice alisema madai ya wafanyakazi kukatwa sehemu ya
mishahara yao kwa ajili ya pensheni ni ya kweli.
Aidha Alice alieza zaidi kuwa fedha hizo badala ya
kuwasilishwa kwenye mifuko ya kijamii zilikuwa zikiingizwa kwenye fuko Kuu la
kampuni hiyo kwa sababu wafanyakazi hao walikuwa siyo wanachama wa mifuko hiyo.
Alice aliahidi kuwasiliana na bosi wake Zhang ili
azungumzie madai ya kuwepo biashara baina ya CRBC na SCG na kwamba taarifa
rasmi angeitoa kwa TANZANIA PANORAMA lakini kwa zaidi ya wiki mbili ameshindwa
kutekeleza Ahadi yake hiyo.
Meneja wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo
alipotafutwa kuzungumzia iwapo taratibu za mamlaka hiyo zinaruhusu vifaa
vilivyoingizwa nchini vikiwa na msamaha wa kodi kutumiwa kibiashara, simu yake
iliita zaidi ya mara tano bila kupokelewa na hata alipotumiwa maswali kwa
ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani, aliyasoma lakini hakujibu chochote.
Jitihada za kumpata balozi wa China kuzungumzia hilo
hazikiweza kuzaa matunda baada ya simu kuwa inaita bila kupokelewa.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment