NA MWANDISHI WETU
IMEELEZWA kuwa vitendo vya kughushi nyaraka za
serikali vinafanywa na Watanzania wengi hapa nchini.
Akizungumza na TANZANIA PANORAMA jana, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba( TMDA), Akida Khea, alisema
siyo jambo jipya wala la kushtusha kwa nyaraka za serikali kughushiwa na kazi
ya serikali ni kupambana na uhalifu huo.
Khea alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwenendo wa
uchunguzi wa tuhuma kuhusu Kampuni ya Multvet Farm Ltd ya jijini Dar es Salaam
kuingiza nchini dawa za mifugo na kuzisambaza kwa matumizi kwa kutumia vibali
vyenye shaka vya TMDA.
Msemaji wa TMDA, Gaudensia Simwaza ambaye awali
alilieleza TANZANIA PANORAMA kuwa taasisi yake inaendelea na uchunguzi wa
nyaraka za kampuni hiyo hivyo ipewe muda wa kutosha, jana alipoulizwa alisema
mkurugenzi wake mkuu alitaka kwanza kuzungumza na TANZANIA PANORAMA.
Katika mazungumzo yake na TANZANIA PANORAMA, Khea aliomba
mkutano wa ana kwa ana kwa kuialika ofisini kwake Jumatatu, Oktoba 5, 2020 huku
akisisitiza kuwa anahitaji kupata msaada utakaosadia uchunguzi unaofanywa
taasisi yake.
Alisema, vitendo vya kughushi nyaraka za serikali
siyo vipya kwani vimekuwa vikifanywa na watu wengi hivyo vipo kila mara na
kwamba serikali imekuwa ikipambana navyo.
"Njoo ofisini tuzungumze, njoo utusaidie. Huyu
mtu siyo wa kwanza. Wapo wengi tu. Hivi vitendo vya watu kughushi nyaraka za
serikali vinafanywa na watu kila mara na serikali inapambana navyo
kikamalifu," alisema Khea.
Inadaiwa kuwa Kampuni ya Multvet Farm Ltd inayoagiza
dawa za mifugo kutoka nje ya nchi imekuwa ikitumia vibali vyenye shaka vya TMDA
huku akilipa kodi zote za serikali.
Kwamba kampuni hiyo imekuwa ikitumia vibali vyenye
shaka vya TMDA kwa zaidi ya miaka minne sasa na baadhi ya wataalamu wa afya ya
mifugo wameeleza kuwa dawa ambazo hazijathibitishwa na TMDA kutumika katika
mifugo zinaweza kuwa na athari mbaya katika ustawi wa mifugo na kuongeza kuwa
hilo linaweza kuwa moja ya mipango ovu ya kuangamiza mifugo hapa nchini.
Mmiliki wa Kampuni ya Multvet Farm Ltd, Dk. Henry
Ruhinguka alipoulizwa kuhusu kampuni yake kuelekezewa madai hayo kwanza
alikanusha kuwa yeye siyo msemaji wa kampuni hiyo na pia alikanusha kufahamu
lolote kuhusu madai hayo.
Hata hivyo uchunguzi wa TANZANIA PANORAMA umebaini
kuwa Dk. Henry ndiye mmiliki wa kampuni hiyo na amekuwa mzungumzaji wake mkuu.
Katika mahojiano hayo Dk. Henry baada ya kuelezwa
kuwa baadhi ya nyaraka zenye shaka za kampuni yake zilizotumika kuingiza dawa
hizo TANZANIA PANORAMA limeziona, alisema, hayo ni mambo ya zamani na hivi sasa
kampuni hiyo iliishaachana nayo.
Alisema ni kweli jambo hilo liliwahi kutokea na
alilipeleka Dodoma kwa wakubwa lakini hakufafanua alilipeleka kwa wakubwa
gani na maamuzi yaliyochukuliwa.
No comments:
Post a Comment