banner

Thursday, October 15, 2020

TANROAD DAR ES SALAAM WALALAMIKA SHERIA ZA BARABARA KUPUUZWA

 

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Wakala wa Barabara (Tanroad) Mkoa wa Dar es Salaam, umesema maagizo ya kisiasa yanayotolewa na wanasiasa kuhusu matumizi na utunzaji wa miundombinu ya barabara yamekuwa yakikinzana na sheria na miongozo ya utunzaji barabara.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Mipango Tanroad Mkoa wa Dar es Salaam, Elisony Mweladzi alipofanya mahojiano na TANZANIA PANORAMA wiki iliyopita kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara wa eneo la Kimara Mwisho kupangishwa vibanda vya biashara vilivyo katika eneo la Tanroad kwa bei kubwa.

Katika majibu yake, Mweladzi alisema sheria na miongozo iliyopo hairuhusu mtu yeyote kufanya biashara pembeni ya barabara hivyo Tanroad haijakodisha eneo lolote lililo pembezoni mwa barabara isipokuwa wafanyabiashara wamekuwa wakivamia maeneo yaliyo wazi na kuyatumia  kibiashara kwa kufuata maagizo ya kisiasa yanayotolewa na wanasiasa.

"Kwanza nataka ieleweke hakuna mwekezaji eneo la Kimara mwisho bali kuna wafanyabiashara pale. Kweli lile ni eneo la Tanroad na imelitoa kwa wafanyabiashara wapatao sita, Wanne upande wa kulia na wawili wapo upande wa kushoto wa barabara.

"Hawa tumewakodisha maeneo hayo na wanalipa kwa dola (fedha za marekani) lakini kwa ajili ya maegesho ya magari na siyo kuweka vibanda vidogo vidogo vya wafanyabiashara wa bidhaa za vyakula na nyinginezo.

" Sasa sisi tunatoa vibali vya kuegesha magari tu lakini hatuhusiki hata kidogo na vibali vya wafanyabiashara wadogo ndani ya hifadhi ya barabara. Na tulishachukua hatua hapo awali na kama wapo wengine basi tutawashughulikia.

"Tatizo linalotukwamisha kusimamia ipasavyo jambo hili ni matamko ya kisiasa yanayotolewa na viongozi wa kisiasa kwa sababu hawazingatia sheria, wanawaruhusu kufanya biashara pembezoni mwa barabara jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria. Nadhani hata wewe mwandishi unaujua ugumu wa kusimamia sheria panapokuwa na upinzani kutoka kwa wanasiasa," alisema  Mweladzi.

Awali wafanyabiashara wadogo wa eneo Kimara Mwisho waliiambia TANZANIA PANORAMA kuwa mwekezaji aliyepewa eneo la pembezoni mwa barabara na Tanroad anawatoza fedha nyingi za kukodi vibanda vya biashara na hata wasiokuwa na vibanda nao wanatozwa bila kujali wana vitambulisho vya wamachinga.

Walisema vibanda vya mbogamboga na mama lishe vinatozwa kuanzia sh 50,000 hadi 300,000 na wapiga kiwi viatu ambao kikawaida hawana vibanda wao wanalipia eneo wanaloweka meza sh 45,000 hadi 50,000.

Akijibu hilo, Mweladzi alisema malalamiko hayo yanashagaza kwa sababu wafanyabiashara hao walipata kufika ofisini kwake wakimsifia na kumshukuru mfanyabiashara aliyewapa eneo hilo na kuwaruhusu kufanya biashara bila kuwatoza chochote na waliomba Tanroads inamruhusu awajengee choo.

TANZANIA PANORAMA lilifika ofisini kwa mfanyabiashara huyo eneo la Kimara Mwisho na kukutana na wasaidizi wake walioeleza kuwa bosi wao hayupo hivyo wapewe muda wawasiliane naye kabla ya kujibu maswali waliyoulizwa.

Wakijibu kwa niaba ya bosi wao walisema, Biashara yote inayoendelea katika eneo hilo la pembezoni mwa barabara inatambuliwa na kusimamiwa na Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Dar es Salaam hivyo kuna jambo lolote linalohitaji ufafanuzi basi aulizwe yeye.

No comments:

Post a Comment