NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama Cha Mapunduzi (CCM), Kassim Majaliwa jana amemuuza mgombea urais wa chama
hicho, Dk. John Pombe Magufuli kwa rekodi yake ya kupigiwa mfano ya utendaji
kazi.
Majaliwa ameutangazia umma wa Watanzania kuwa
mgombea hiyo wa CCM ana rekodi ya kutukuka ya utendaji kazi katika kipindi cha
miaka 20 alipokuwa Waziri katika wizara mbalimbali.
Akiwahutubia wakazi wa Ushirombo, Okotoba Mosi
katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe mkoani
Geita, amesema Dt. Magufuli ana rekodi nzuri ya utendaji kazi.
"Dk. Magufuli tunamjua. Alikuwa Waziri katika
nchi hii kwa miaka 20. Alikuwa Waziri wa Ujenzi akajenga barabara ambazo sote
leo tunaziona. Alipoenda Wizara ya Ardhi, akapiga marufuku watumishi wa wizara
hiyo kujilimbikizia viwanja vinne vinne.
"Nimekuja kuwaomba kura zenu. Ni lazima tumpe
kura mtu ambaye tunaijua historia yake ya kwamba aliwahi kuwa kiongozi na
ameweka historia," amesema.
Majaliwa amewataka wananchi wamchague kiongozi
ambaye anaweza kuisimamia Serikali yake.
"Usipokuwa makini unaweza kumpa mtu
nchi halafu akashindwa kuisimamia. Kiongozi anayefaa, mwenye uwezo wa
kuratibu rasilimali zetu na kuzisimamia, si mwingine bali ni Dk.
Magufuli," amesema.
Amehimiza watanzania wawachague wagombea wa CCM ili
waweze kuzungumza lugha moja. "Ni muhimu tuwe na madiwani ili waunde
baraza lao la madiwani, waongee lugha moja na wapeleke hoja zao kwa mbunge
wao," amesema.
Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya kumuombea kura
mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi
mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko na mgombea udiwani wa Kata ya
Igulwa, Richard Mabenga.
"Dk. Magufuli amekuwa rais kwa miaka mitano,
aliyoyafanya katika kipindi kifupi tunayaona. Dk. Magufuli huyu, wala rushwa
ndiye kiboko yao. Leo niko mbele yako, bila kujali chama chako cha siasa,
ninakuomba umpigie kura Dk. Magufuli. Niko mbele yenu, ninawaomba kura za
wagombea wa CCM," amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema
Wilaya ya Mbogwe imetengewa sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi
za Makao Makuu ya Wilaya hiyo.
Akielezea kuhusu sekta ya maji, amesema serikali
imetoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa
maji Kabanga – Nhomolwa ambao ulipatiwa sh. bilioni 1.2. “Fedha nyingine
zilizotolewa ni shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji
Mbogwe ambao utanufaisha maeneo ya Kasosobe, Bwelwa na Iboya.”
Amesema upanuzi wa mradi wa maji Nyakafuru umepatiwa
sh. milioni 633 ambao utanufaisha maeneo ya Lulembela na Nyakafuru, Shinyanga A
& B pamoja na usimikaji wa nguzo za umeme huko Nyakafuru, Shenda na
Masumbwe.
Majaliwa amemaliza ziara yake mkoani Geita na
anaendelea kutafuta kura katika Mkoa wa Shinyanga.
No comments:
Post a Comment