SHILINGI bilioni 5.26 zimetolewa kupitia
Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya ujenzi
na matengenezo ya barabara katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.
“Kati ya hizo, shilingi bilioni 1.1
zimetengeneza barabara kwa kiwango cha lami kilomita 4.5 katika makao makuu ya
wilaya hii.”
WHayo yamesemwa leo (Jumatano, Septemba 30, 2020) na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Rulenge, katika
mikutano uliofanyika kwenye stendi ya Rulenge.
Amesema kiasi kingine cha shilingi
bilioni 4.16 zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi na
matengenezo ya barabara ikiwemo barabara za Muhweza – Mukarehe, Keza –
Nyanzovu, Mukalinzi – Mulonzi, Kibuba – Gwenzaza, Murugwanza -
Runzenze (Airstrip), Chivu - Ntobeye – Nyakiziba,Buhororo – Mukididili, Ngara –
Kumutana na Buhororo - Ruganzo (Airstrip)
Majaliwa ambaye leo anamalizia ziara yake mkoani
Kagera ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe
Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Ngara,
Ndayisaba George Ruhoro na mgombea udiwani wa CCM wa kata ya Rulenge, John Niyonzima.
Mapema, akiwa njiani kuelekea Ngara akitokea
Bukoba mjini, Majaliwa alisimamishwa na wakazi wa kata za Nyaishozi (Karagwe)
na Kasulo Benaco (Ngara) ambako pia aliwanadi madiwani wa kata hizo. Pia
aliwaeleza kwamba barabara ya kutoka Omurushaka hadi Benaco itajengwa kwa
kiwango cha lami.
“Kwenye Ilani ya uchaguzi iliyopita ambayo inaisha
sasa, barabara hii ilielezwa kwamba itakamilishwa kufanyiwa upembuzi yakinifu,
na sasa inaenda kujengwa kwa lami kwa sababu kazi imeshafanyika.”
Pia aliitaja barabara nyingine ya kutoka Bugene –
Kasulo (BENACO) yenye urefu wa km. 124 ambayo inatajwa kwenye uk. 75 wa Ilani
ya Uchaguzi ya CCM kwamba ni miongoni mwa barabara zitakazoanza kujengwa upya
kwa kiwango cha lami.

No comments:
Post a Comment