banner

Saturday, October 3, 2020

VIBARUA ONE WORLD CO. LTD WALIA KUNYANYASWA, KUTISHIWA MAISHA


NA MWANDISHI WETU

VIBARUA wa Kampuni ya One World Company Limited ya jijijni Dar es Salaam wamelalamika kuwa wananyanyaswa na kutishiwa maisha na mwajiri wao.

Wamesema mwajiri wao anakiuka makubaliano waliyoingia kufanya kazi, kutowapa mikataba ya ajira, kuwapunja malipo ya kazi wanazofanya kwa kampuni anazowapeleka kufanya kazi anazoingia nazo mikataba ya kumkodishia vibarua na kutopeleka fedha za makato katika mifuko ya pensheni.

Malalamiko hayo wameyatoa mwishoni mwa  wiki jijini Dar es Salaam katika mahojiano yao na TANZANIA PANORAMA.

"Tumeamua kuwatafuta nyie watu wa TANZANIA PANORAMA baada ya kuona nyie mko tofauti na wengine kwa sababu mnagusa matatizo ya Watanzania na kuyaweka hadhani. Ukiangalia kwenye mitandao unaona mnaandika habari ambazo haziandikwi na wengine ambazo zinagusa maisha ya watu wanyonge moja kwa moja.

" Sasa sisi tuna malalamiko yetu, tunaomba yafike serikalini na tunaomba serikali ije itusikilize sisi wananchi wake. Tunaomba kwanza kuiambia serikali kuwa huyu mwajiri wetu Kampuni ya One World Company Limited anatunyanyasa na kututishia maisha kila tunapojaribu kudai hata kile kidogo anachotudhulumu.

"Huyu mwajiri wetu anatufanyisha kazi kwa saa nyingi kuliko tulivyokubaliana, baadhi yetu wana miaka mingi sana kwenye kampuni lakini kila wakiomba ajira anasema anayetaka ajira aache kazi. Sasa tunashagaa huyu bwana mbona anakiuka sheria kwa sababu sheria inaelekeza mtu akifanya kazi kwa kipindi fulani anapaswa kuajiriwa.

"Jambo jingine ni pensheni, hapeleki pesa yetu kwenye mifuko ya jamii, na huko mahakama ya kazi wamemshindwa maana amekataa kupokea barua za mahakama  baada ya wenzetu kumfungulia shauri kwenye mahakama hiyo lakini kinachotuuma zaidi, huyu ana mikataba ya siri na baadhi ya makampuni hapa nchini ambayo huwa anayatafutia vibarua anawapeleka kufanya kazi huko na hayo makampuni yanamlipa ili alipe vibarua aliowapeleka.

" Kibaya hapo ni kwamba zile pesa zetu huwa anatulipa kidogo sana kiasi kikubwa anachukua yeye bila kujali kampuni hizo zinakuwa zimeishamlipa hela yake ya udalali. Tukimlalamikia kuwa anatuonea anasema ambaye amechoka kuishi aendelee kuhoji na ole wake atakayebainika kutoa siri za kampuni nje," alisema mmoja wa vibarua hao ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu ya kulinda kibarua chake.

Akizungumzia malalamiko hayo. Mwanasheria wa vibarua hao, Saulo Kusakala alieleza kushangazwa na uongozi wa kampuni hiyo kwa kuonyesha kiburi hata kwa Mahakama.

"Kweli mimi ni mwanasheria wao, nimeamua kuwasaidia kwa sababu ukisikia mateso yao kwa kweli unawahurumia. Kama mwanasheria wao nilimuandikia barua huyo mwajiri ili nipate maelezo yake kuhusu malalamiko ya wafanyakazi wake alichojibu ni kwamba hawatambui. Yaani hana ushirikiano kabisa," alisema.

Alipoulizwa Mkurugenzi wa One World, Kelvin Tegwa kuhusu malalamiko hayo alisema hao waliokuja kwa waandishi wa habari wanajisumbua na alijigamba kuwa ana mkono mrefu hivyo atawabaini na atawashughulikia.

"Unasema wewe ni mwandishi wa habari, kwa hiyo wamekuja kwako ili utuchafue. Kwahiyo kwako ndiyo wanadhani watapata msaada? Labda nikuulize sasa wamekuja kalalamika kwako wewe utafanya nini? Wewe njoo tuongee ofisini hao waache niko nao mahakamani.

" Na ninakwambia tu mimi nafanya kazi na serikali, nina mkono mrefu hivyo hata hao waliokuja kwako nakuhakikishia ntajua na nitawashughulikia. Hii siyo kampuni ya kuchezea, alisema.

Muda mfupi baadaye TANZANIA PANORAMA lilipigiwa simu na mtu ambaye hakujitambulisha jina lakini uchunguzi wa namba aliyotumia umebaini kuwa imesajiliwa kwa jina la Dismas Damas ambaye alionya kuwa kitu chochote kinachohusu kampuni hiyo kisiandikwe.

Damas alisema iwapo maelekezo hayo yatakiukwa asiwepo wa kulalamika na kabla hajakata simu alisema yeye ni meneja wa Kampuni ya One World Company Ltd na milango yake ipo wazi kwa mazungumzo.

No comments:

Post a Comment