NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Zanzibar wamchague
Dk. John Pombe Magufuli kuwa rais kwa sababu ndiye mgombea pekee mwenye
uwezo wa kudumisha Muungano.
"Nawaletea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, amefanya makubwa kwenye uongozi wake uliopita. Hata kwenye wizara
alizowahi kuongoza, pia amefanya makubwa. Ndiye mgombea pekee mwenye uwezo wa
kutuunganisha Wazanzibari na Watanzania Bara,” alisema.
Wito huo aliutoa Jumatatu, Oktoba 12, 2020 wakati
akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mkutano uliofanyika
kwenye uwanja wa mpira wa Kairo, Kiwengwa, Wilaya ya Kaskazini B.
Alisema wako baadhi ya wagombea wanaotangaza
kuuvunja muungano pindi wakichaguliwa na amewataka wananchi wa Zanzibar wawaepuke.
Alisisitiza kuwa kazi ya rais si ya mchezo na
inataka mtu makini, kwa hiyo akawaomba wakazi hao wamchangue mtu ambaye ana
uwezo wa kupambana na wala rushwa.
Majaliwa yuko Zanzibar kuwaombea kura mgombea urais
kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM,
Dk. Hussein Mwinyi, wagombea ubunge wa majimbo, wawakilishi na wagombea
udiwani.
Akimuombea kura Dk. Mwinyi, Majaliwa alisema Chama
Cha Mapinduzi kina benki ya kutosha ya makada wenye uwezo wa kuongoza. “Chama
Cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za uongozi na katika nafasi hii ya kuongoza
Zanzibar, tumemleta Dk. Hussein Mwinyi.”
Alisema yapo mambo mengi mazuri yamefanywa na Dk.
Ali Mohammed Shein na yaliyobakia yatakamilishwa na Dk. Mwinyi. “Masuala yote
ya kipaumbele yamewekwa kwenye ilani ya uchaguzi yenye kurasa 303. Pia kitabu
hiki kimesambazwa hadi kwenye shehia zenu. Kitafuteni mkisome ili muone mambo
yaliyopangwa kufanyika kwa ajili ya Zanzibar.
“Maendeleo ya mifugo yamo humu, maendeleo ya uvuvi
yamo humu, maendeleo ya ajira yamo, kuwezesha sekta binafsi yamo humu,
kuwezesha viwanda yamo humu, kuwezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa
nayo pia yamo humu,” alieleza.
Mapema, akinadi sera zake, Dk. Mwinyi
alisema serikali yake itaimarisha uvuvi wa bahari kuu pamoja na bandari za
uvuvi pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki ili kuongeza ajira na
masoko kwa bidhaa za baharini.
Alisema ataimarisha ufugaji wa samaki ikiwa ni njia
mojawapo ya kulinda mazingira. “Nitasimamia hilo la ufugaji wa samaki hasa
kwenye maeneo ya mikoko kwa sababu tutakuwa pia tunalinda mazingira yetu,”
alisema.
Alisisitiza kuwa atashughulikia tatizo la mmomonyoko
wa maadili na hasa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji wa
wanawake na watoto. “Ninawaomba mtoe ushirikiano kwa sababu wanaofanya hivi
vitendo mnawajua. Tusaidieni ili tuweze kudhibiti hivi vitendo vya
udhalilishaji na dawa za kulevya,” alisema.
Akielezea kuhusu sekta ya maji, Dk. Mwinyi alisema
upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 72 na kwamba asilimia 28
iliyobakia ni ya kutoa maji kutoka barabara kuu hadi kwenye makazi ya watu.
“Serikali yetu itakamilisha hiyo sehemu ndogo iliyobakia,” alisema.
Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuomba kura za Dk.
Magufuli, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa CCM.
No comments:
Post a Comment