MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema serikali ijayo ya CCM
itaanzisha maabara na kliniki za kutibu mifugo katika wilaya zote za wafugaji
nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wakazi
wa Kata ya Orgosorok, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, katika mkutano
uliofanyika kwenye uwanja wa Waziri Mkuu, mji mdogo wa Loliondo.
"Tumeanza kuwatumikia na kuwahudumia wafugaji
kwa kuhakikisha kuwa wana maeneo mazuri ya malisho, na sasa tumeamua
kuwachimbia mabwawa ya kunywesha mifugo.
"Bado tutaendelea kubaini maeneo ya wafugaji na
kuwachimbia mabwawa na majosho. Na sasa, tunaanzisha maabara kwa ajili ya
kupima magonjwa ya mifugo. Tunajenga kliniki kwa ajili ya kutibu mifugo kwenye
wilaya zote zinazofuga na pia tunatoa dawa ya ruzuku kwa ajili ya mifugo,"
amesema.
Amesema Serikali ya CCM itaendelea kuweka mazingira
mazuri ya kuhudumia mifugo na hivyo, wafugaji waendelee kufuga kwa uhakika ili
Watanzania wanufaike na sekta ya mifugo.
Kuhusu barabara, Majaliwa amesema Serikali ijayo ya
CCM itajenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa km. 300 kutoka Mto wa
Mbu hadi Ngorongoro.
Majaliwa amewaomba wananchi wa Ngorongoro wamchangue
tena Dk. John Magufuli ili aendelee kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ameonyesha uwezo
mkubwa katika kukusanya mapato ya Serikali na kusimamia matumizi yake.
Amesema: “Kazi ya Urais ni kazi nzito na haina
nafasi ya kufanyiwa majaribio na mtu ambaye hana historia na uongozi wa nchi,”
na kusisitiza kuwa: “Amani ya nchi inategemea kwa kiwango kikubwa na kiongozi
aliyeko madarakani, kwani akiwa kiongozi mahiri ataisimamia amani iliyopo, na
akiwa kiongozi legelege amani itayumba.”
Wakati huohuo, Mama Mary Majaliwa amewaomba
wakazi wa Ngorongoro wampe kura zote za ndiyo Dk. John Pombe Magufuli, mgombea
ubunge wa Jimbo la Ngorongoro William Ole Nasha na wagombea udiwani wote kwa
tiketi ya CCM.
Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kwa
tiketi ya CCM, William Tate Ole Nasha amesema maendeleo yaliyopatikana katika
kipindi cha awamu ya kwanza ya miaka mitano ya Dk. Magufuli ni makubwa na
hakika historia ya maendeleo imeandikwa katika Wilaya ya Ngorongoro.
“Kwa mara ya kwanza, Chuo cha Ufundi VETA kinajengwa
Ngorongoro na Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa chuo
hicho katika eneo la Samunge, Loliondo," amesema.
Ole Nasha amesema Serikali imetoa shilingi bilioni
2.2 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na hivyo kurahisisha upatikanaji
wa huduma za afya kwani wananchi wa Ngorongoro hawatalazimika kwenda Arusha au
nchi jirani ili kupata matibabu.
Majaliwa yuko mkoani Arusha kumuombea kura mgombea
urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa Jimbo la
Ngorongoro, William Ole Nasha na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM.
No comments:
Post a Comment