banner

Saturday, October 31, 2020

WAZIRI MKUU MAJALIWA APIGA KURA KIJIJINI KWAKE

 


*Asema ameridhishwa na shughuli inavyoendelea

 NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amepiga kura kijijini kwake Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge mteule wa jimbo la Ruangwa alipiga kura kwenye kituo cha Shule ya Msingi Nandagala Jumatano, Oktoba 28, 2020 akiwa na mkewe Mama Mary Majaliwa.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Waziri Mkuu alisema shughuli ya kupiga kura ni haki ya msingi na anamshukuru Mungu imeenda salama.

“Ninamshukru Mungu nimeweza kushiriki haki yangu ya msingi ya kumchagua kiongozi ninayempenda ili aweze kuliongoza taifa hili.

“Kwa hapa Nandagala, Mbunge na Diwani walishapita bila kupingwa, kwa hiyo leo nimepiga kura moja tu ya kumchagua Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwasili kituoni saa 4:20, na kujipanga foleni yeye na mkewe, alifuata taratibu kama wananchi wengine na alipiga kura saa 4:53. Aliondoka kituoni hapo saa 5:00 asubuhi.

Akielezea kuhusu utaratibu wa upigaji kura, Majaliwa alisema shughuli zima ilienda vizuri na aliwapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa sababu alikuta kuna utulivu na watu wamekaa kwenye foleni wakisubiri kuingia ndani.

“Nimekuta watu wanafuata utaratibu, wanapatiwa maelekezo, vitambulisho vinahakikiwa, ni jambo la kujivunia. Amani kwetu bado ni tunu ambayo hatutakiwi kuidondosha chini ikaharibika. Ninatoa wito kwa Watanzania tujitokeze tukapige kura ili tupate viongozi wa ngazi zote ambao watatuongoza. Ni nafasi muhimu, ukiikosa leo, hutaipata tena kwa miaka mitano ijayo,” alisema.

No comments:

Post a Comment