NA PIUS NTIGA, MOSHI
WAFANYABIASHARA wadogo, maarufu kwa jina la Machinga
katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamesema vitambulisho wa
wajasiriamali wadogo vimewatua mzigo hivyo wanawashangaa baadhi ya wanasiasa
wanaopotosha kuhusu vitambulisho hivyo.
Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM
inayoangazia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
John Magufuli, wafanyabiashara hao wamesema utamu wa vitambulisho hivyo
wanaujua wao.
Wamesema awali walikuwa wanalipa shilingi 500 kwa
siku, sawa na shilingi 182,000 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa
ukilinganisha na shilingi 20,000 wanayolipa sasa kwa mwaka.
"Tulikua tukilipa shilingi 200 ya usafi kwa
siku, sawa na shilingi 73,000 kwa mwaka, ambapo sasa mateso kama hayo
hatuyapati. Tena tunashukuru sana Rais Magufuli kwa kutuona na tutampa zawadi
mwaka huu" wamesema Machinga.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao wadogo, mkombozi
wao ni Rais Magufuli ambaye amekuja na mpango wa sh 20,000 tu kwa mwaka
na sasa kero za mgambo kuwafukuza hazipo tena.
"Nikwambie tu kuwa mabenki nayo yamesema kwa
kuwa tuna vitambulisho, shughuli zetu zimerasimishwa hivyo tumeanza kupewa
mikopo huku vitambulisho vikiwa ni dhamana yetu". wamesema
Wamesema hivi sasa hawasumbuliwi tena na askari wa
jiji wala mgambo kama ilivyokuwa hapo awali.
"Vitambulisho vya wamachinga vimetusaidia sana,
tunanunua kwa ridhaa yetu, hatulazimishwi". wamesema Machinga.
Aidha, wamefafanua kuwa uwepo wa vitambulisho hivyo
umewaondolea kero na kwa sasa biashara yao imeimarika zaidi na kipato chao
kimeongezeka na wamefanikiwa kununua ardhi na kujenga nyumba.
Kutokana na mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, amesema tangu kuanza kwa utaratibu huo
zaidi ya asilimia 70 ya wamachinga wamepatiwa vitambulisho katika Manispaa ya
Moshi.
Mwandezi amesema fedha inayotokana na vitambulisho
hivyo inakwenda Hazina na kisha kurudishwa katika Manispaa kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawagusa moja kwa moja wananchi.
"Pia tumewasaidia hawa wajasiriamali kuwajengea
uwezo wa kimtaji ambapo sasa wanakopesheka kupitia vitambulisho, hivyo
vimewanufaisha kwa kukopa fedha benki," amesema Mkurugenzi huyo
Hivi karibuni baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipotosha kuhusu vitambulisho hivyo vya wamachinga kuwa haviwanufaishi na badala yake wanaibiwa, kauli ambayo Rais John Magufuli ambaye ni mgombea wa urais kupitia CCM, amewataka wafanyabiashara hao kuwapuuza wanasiasa na badala yake waunge juhudi za serikali za kuwakomboa Wamachinga.



No comments:
Post a Comment