NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya uwakili ya IMMMA imemfukuza mwanahisa
wake, Fatuma Karume.
Barua ya kufukuzwa kwa Fatuma Karume, maarufu kwa
jina la shangazi, ya Septemba 16, 2020 ambayo TANZANIA PANORAMA BLOG imeiona
imesainiwa na Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya IMMMA, Sadock Magai ikiwa
na maelekezo yanayomtaka wakili huyo kufungasha virago vyake ndani ya mwezi
mmoja.
Barua ya kufukuzwa kwa Fatuma aliisambaza yeye
mwenyewe kwenye mitandao ya kijamii akiambatanisha na ujumbe kuwa kila kitu
kina mwanzo na mwisho.
Katika andishi lake hilo Fatuma anaandika kuwa
amefukuzwa kwenye ofisi aliyosaidia kuijenga na kosa lake ni uanaharakati.
Wakili na mwanaharakati Fatuma amefukuzwa na
washirika wake wa muda mrefu katika fani ya sheria baada ya kujihusisha na
mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa
serikali.
Aidha, Fatuma amepata kushambuliwa hadharani na
mmoja wa wazazi wake kutokana na mwenendo wake wa kuwashambulia kwa lugha isiyokuwa
na staha viongozi wakuu wa kitaifa na bila kujali kuwa baba yake mzazi amepata
kuwa kiongozi mkuu wa Zanzibar.
Katika barua yake ya kumfukuza Fatuma, Magai
anaandika kuwa mwanaharakati huyo anaondolewa kwenye umiliki wa kampuni na
akusanye vilivyo vyake katika ofisi hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Magai anaandika zaidi akielekeza kuwa Fatuma
anapaswa kurudisha kila kitu alichonacho ambacho ni mali ya Kampuni ya IMMMA na
pia kesi alizokuwa anazisimamia
azikabidhi na hasa kesi ya Kampuni ya Shivacom na Vodacom.
Andiko la Magai linaeleza pia kuwa Fatuma atalipwa
stahiki zake kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment