NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeuza kwa njia
ya mnada shehena ya sabuni ya unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha.
Shehena hiyo ya sabuni isiyofaa kutumika baada ya
muda wake kuisha iliingizwa nchini kutoka nje na kukaa bandarini bila kulipiwa
ushuru kwa muda mrefu kabla TRA haijaamua kuiuza.
Habari za uhakika zilizokusanywa na TANZANIA
PANORAMA zimeonyesha kuwa shehena hiyo ilikuwa na mifuko 1,800' ya sabuni ya
unga aina AKO na imeuzwa kwa njia ya mnada na maafisa wa TRA huku wakijua kuwa
wanatenda kosa linaloweza kuwa na athari mbaya kwa watakaoitumia sabuni hiyo.
TANZANIA PANORAMA limedokezwa na vyanzo vyake vya
habari kuwa shehena hiyo ambayo thamani yake ni sh milioni 300, ili kuwa
imehifadhiwa katika bandari kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam na imepigwa mnada
mapema mwezi huu kwa sh milioni 20
"Watanzania tunaumizana wenyewe kwa wenyewe.
Sabuni iliyopigwa mnada na TRA imekwisha muda wake wa matumizi na TRA walilijua
hilo. Sasa wameiingiza mtaani bila kujali kama itasababisha magonjwa kwa
watakaoitumia, wewe waulize uone kama watajibu, watababaisha tu maana
wanajua siku hizi hakuna watu wa kichumbua mambo," alisema mmoja wa watoa
habari wa TANZANIA PANORAMA.
Alipoulizwa juzi, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi
wa TRA, Richard Kayombo haraka haraka alikanusha kuwa taarifa hizo hazina
ukweli na kutaka atumiwe ushahidi wa uwepo wa shehena hiyo na alipotumiwa
sehemu ndogo ya ushahidi aliotaka aliomba apewe muda kidogo afuatilie.
Hadi juzi jioni Kayombo alishindwa kutoa majibu
kwani kila alipopigiwa alisema maafisa wanaohusika na minada na wale wa forodha
wote wametoka ofisini hivyo anaendelea kuwasubiri na alipoombwa namba zao za
simu alikataa kutoa.
Jana asubuhi, TANZANIA PANORAMA lilimtafuta
tena Kayombo ili kuzungumzia tuhuma hizo lakini hakupokea simu na alipotumiwa
ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani akikumbushwa ahadi yake ya kutoa
kauli kuhusu tuhuma hizo na pia kutimiza wajibu wake alijibu kuwa kuna taarifa
moja anaisubiri kutoka kwa wahusika wa mnada.
TANZANIA PANORAMA lilimtumia ujumbe mwingine
likimshauri awe anapokea simu yake na kutoa taarifa hata kama hajafanikiwa
kupata majibu husika na yeye alijibu kuwa akiwa kwenye kikao huwa hapokei simu
kwa sababu siyo nidhami nzuri.
Baadaye mchana, Kayombo alitafutwa tena lakini
hakujibu chochote na majira ya jioni alipiga simu na kueleza kuwa ni kweli
shehena hiyo ya sabuni ilikuwepo TRA na imeishauzwa lakini haweza kusema kama
muda wake wa matumizi umeishaisha au bado.
"Sasa bwana ni hivi. Ni kweli huo mzigo
unaousema ni kweli ulikuwepo TRA. Ni kweli kabisa. Na mnada wake wa kwanza
ulikuwa Agosti 24, 2020 lakini aliyeshinda hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike
mnada mwingine ndiyo ukauzika
" Ni kama kulikuwa na pande mbili zilizokuwa
zikiushindania kwa sababu yule mnunuzi wa kwanza hakuja kulipa hivyo ikabidi
ufanyike mnada mwingine ndipo shehena ile ikachukuliwa kwa sh. milioni 21.5
," alisema Kayombo.
Alipoulizwa mnada wa pili uliofanyika lini na
kukumbushwa kujibu swali aliloulizwa kuwa TRA inadaiwa kuuza shehena ya sabuni
iliyokwisha muda wa matumizi huku ikijua kuwa inaweza kuwa na athari mbaya kwa
watumiaji alisema maswali hayo hawezi kuyajibu.
"Hivi unaandikia chombo gani siku
hizi........ Sasa hayo maswali mengine mimi siwezi kuyajibu we fahamu tu
mnada umefanyika mara mbili," alisema Kayombo.


No comments:
Post a Comment