WAZIRI MKUU, KASSIN MAJALIWA AKIWAHUTUBIA WANANCHI WA MUSOMA MJINI
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetumia shilingi bilioni 25 kujenga na
kukarabati barabarani na mitaa ya Manispaa ya Mji wa Musoma, Mkoa wa Mara.
Sambamba na hilo, Serikali pia imeweka taa za
barabarani urefu wa kilomita 14 kupitia programu ya uboreshaji wa Miji (ULGSP)
katika manispaa hiyo.
Hayo yameelezwa Septemba 21, 2020 na Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim
Majaliwa katika hotuba yake ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM,
Rais John Pombe Magufuli.
Katika hotuba yake hiyo kwa wakazi wa Mji wa
Musoma aliyoitoa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mara iliyo Kata
ya Nyamatare, Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu alisema hatua chanya zilizokwishachukuliwa
ya serikali tangu mwaka 2015 ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2015 -2020.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema ni lengo la serikali
kuifanya miji yote ya Tanzania ukiwemo wa Musoma, usiku uwe mchana na mchana
uendelee kuwa mchana.
"Shilingi bilioni 18.7 zimetumika kujenga
kilomita 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani
kupitia programu ya uboreshaji wa miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na
mradi umekamilika. Tunataka taa ziwake ili usiku uwe mchana na mchana uwe
mchana.
" Kupitia Road Fund maintenance, kiasi kingine
cha shilingi bilioni 6.6 kilitumika kwa ajili ya kufungua barabara mpya,
kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na miradi yote
imekamilika.
"Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura
Dk. John Pombe Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu
yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Akizungumzia miradi mingine iliyotekelezwa na
serikali katika uhai wa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano, Waziri Mkuu
Majaliwa alitaja uboreshaji wa huduma za upatikanaji maji katika Manispaa ya
Musoma.
"Ili kuboresha huduma ya upatikanaji maji
katika Manispaa ya Mji wa Musoma, shilingi bilioni 46 zilitolewa na serikali
kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi wa Manispaa ya Mji wa Musoma ambao
tayari umeanza kutoa huduma.
" Shilingi bilioni 18 zimetolewa kwa ajili ya
mradi wa kusambaza maji Manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya Musoma Vijijini
na Butiama. Kazi zinazofanywa sasa ni ujenzi wa tenki la Bharima lenye ujazo wa
lita milioni tatu, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na ulazaji bomba la
kusafirisha maji kwenda tenki la Bharima lenye kipenyo cha milimita 450 na
urefu wa kilomita 1.56, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alitaja kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji
wa bomba la kusafirisha maji kutoka tenki la Bharima kwenda kwenye kaya za
wananchi lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7,058, ufungaji wa
pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa, ununuzi wa
bomba za kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.
No comments:
Post a Comment