banner

Wednesday, September 30, 2020

MAJALIWA: MCHANGUENI DK. MAGUFULI, ANATOKA CHAMA KINACHOJALI WANANCHI

 


*Ampokea aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Kyerwa wamchague Dk. John Pombe Magufuli kuwa rais kwa sababu anatoka katika chama ambacho kina mikakati inayotokana na mawazo ya wananchi.

"Dk. Magufuli anatoka kwenye chama ambacho kina utaratibu katika kuendesha nchi, chama ambacho kina ratibu kero za wananchi, ambacho kinasikiliza wananchi mpaka ngazi ya chini," amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Septemba 29, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkwenda, akiwa njiani kuelekea Isingiro wilayani Kyerwa, mkoani Kagera.

"Tumemjaribu na amefanya mambo makubwa katika wizara alizoziongoza na ndiyo maana namleta kwenu Dk. Magufuli na kumuombea miaka mingine mitano ili alete maendeleo zaidi," amesema.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Kyerwa, Innocent Bilakwate, mgombea udiwani wa Kata ya Nkwenda, Edward Katunzi na wagombea wa CCM wa kata za jirani.

Amesema CCM ni chama kinachoongozwa na Ilani ya Uchaguzi na kuna mambo yamethibitika katika ilani inayoishia 2020.

"Leo tunaleta kitabu kingine cha Ilani ya 2020 - 2025. Kama tuliweza kufanya makubwa ndani ya miaka mitano na kile kitabu kidogo, je huko tuendako itakuwaje?"  amesema.

Akiwa Isingiro kwenye mkutano wa hadhara, Majaliwa amesema serikali ilibadilisha sheria tangu mwaka 2017 na ikazuia uuzaji wa madini ya bati nje ya nchi kwa kutumia njia za panya.

"Sheria inatutaka tutenge ekari kadhaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Leo hii ekari 38,000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini mbalimbali. Pia tumeanzisha masoko ya madini 26 na vituo vidogo 28 vya kuuzia madini," amesema.

 Akifafanua kuhusu vitambulisho vya Taifa, Majaliwa amesema Tanzania ni nchi ya amani na wengi wanatamani kuja kuishi nchini.

Amesema Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Missenyi ni za mipakani kwa hiyo zina changamoto za uhamiaji na masuala ya kiraia.

"Ndiyo maana serikali inakuwa makini katika uhakiki. Tutaimarisha usimamizi ili kila Mtanzania apate kitambulisho," amesema.

Pia amewaonya maafisa wanaohusika na utaoaji vitambulisho vya uraia ambao wanapokea hongo na kuwapa vitambulisho hivyo watu wasiostahili.

Wakati huohuo, Majaliwa amempokea aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Karagwe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Princepius Rwazo ambaye ameamua kurejea CCM. 

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rwazo amesema alikuwa mgombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliopita na aliisumbua sana CCM lakini sasa ameamua kurejea kwani ameona mazuri yanayofanywa na chama hicho.

"CCM imejibu kiu zetu, kimekuwa kama chama cha upinzani, na wapinzani sasa wamelala. Nimerudi CCM, sihitaji cheo chochote, shida yangu ni kujiunga na watu wanaochapa kazi. Nitamuunga mkono Dk. Magufuli na ndugu yangu Bashungwa," amesema na kushangiliwa.

Majaliwa anaendelea za ziara yake katika Wilaya za Karagwe na Missenyi.

MAJALIWA: SERIKALI YATEKELEZA MIRADI 1,423 YA MAJI

 


Kayanga ni miongoni mwa miji 28 iliyonufaika na sh. tril. 1.2 za miradi hiyo

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa amesema Serikali imetekeleza miradi ya maji 1,423 ikiwemo mradi wa kupeleka maji kwenye miji 28 inayotekelezwa kwa sh. trilioni 1.2.

“Kayanga imepata sh. bilioni 58, ni miongoni mwa miji 28 iliyopata fedha za mradi wa maji kitaifa ambao unajumuisha mikoa mingi,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 29, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Kayanga, katika mikutano uliofanyika kwenye uwanja wa Changarawe, wilayani Karagwe, mkoani Kagera.

Mikoa inayohusika na mradi huo miji yake kwenye mabano ni Tanga (Handeni/Korogwe, Muheza na Pangani); Njombe (Njombe, Wanging’ombe na Makambako); Kagera (Kayanga); Mtwara (Nanyumbu na Makonde) na Singida (Manyoni).

Pia Ruvuma (Songea); Tabora (Sikonge, Urambo-Kaliua); Mbeya (Rujewa na Chunya); Kigoma (Kasulu); Lindi (Kilwa Masoko); Mara (Mugumu, Rorya/Tarime); Geita (Geita na Chato); Singida (Singida Mjini na Kiomboi); Katavi (Mpanda); Dodoma (Chamwino na Chemba); Iringa (Mafinga); na Morogoro (Ifakara).

Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, mgombea udiwani wa Kata ya Kayanga, na wagombea wa CCM wa kata za wilaya hiyo.

Amesema miradi mingine ya maji inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo imetumia sh. bilioni 5.2 kwa ajili ya uboreshaji wa miradi ya maji. Ameitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa maji Kijiji cha Nyaishozi ambao umetumia sh. milioni 706, umekamilika na unatoa huduma.

“Shilingi bilioni 1.6 zilitumika kwa ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha Chamchuzi, mradi umekamilika na unatoa huduma, shilingi milioni 805 zilitumika kwa ujenzi wa mradi wa maji Chanika, mradi umekamilika na unatoa huduma," amesema.

Amesema sh. milioni 63 zilitumika kwa uchimbaji wa visima vinne na ufungaji wa pampu katika vijiji vya Okakajinja na Chonyonyo, mradi ambao umekamilika na unatoa huduma. 

Amesema fedha nyingine zilizotumika ni sh. milioni 120 kwa ajili ya mradi wa maji uchimbaji wa visima vinne na ufungaji wa pampu katika vijiji vya Mulamba na Nyarugando, ambao pia umekamilika na unatoa huduma.

Amesema sh. bilioni 2.4 zilitumika kwa ajili ya mradi wa maji Nyakakika, ambao uko katika hatua za umaliziaji na sh. milioni 251 zilitumika kwa ajili ya mradi wa maji Rugu, ambao nao upo kwenye hatua za majaribio.

CHADEMA CHANYOOSHEWA KIDOLE KWA MAUAJI YA KIKATILI

 


NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshutumiwa kuhusika moja kwa moja na tukio la mauaji ya kinyama ya kijana Bryan Mollel.

Kwa mujibu wa taarifa ya kulaani mauaji hayo liyotolewa na Katibu Msaidizi wa Taasisi ya Amani na Maendeleo (TAMA), Mkoa wa Songwe, Jackson Eliabu inawataja waliohusika na mauaji ya kikatili ya kijana Mollel kuwa ni viongozi wa Chadema ambao walimpondaponda kwa mawe hadi alipokufa.

Taarifa ya Eliabu  inawataja wagombea udiwani wa Chadema wa Mkoa wa Songwe kuongoza mauaji hayo kwa sababu ya kulazimisha wapewe fomu nyingine baada ya kuharibu waliyokuwa nayo.

Sehemu ya taarifa hiyo inasomeka hivi; 'Tumepokea kwa masikitiko mauaji yaliyofanywa na kuongozwa na wagombea wa udiwani wa Chadema mkoani Songwe waliyoyafanya hivi karibuni kisa kulazimisha kupewa fomu nyingine baada ya kuharibu fomu ya awali.

'Taarifa zinaeleza kijana Bryan Mollel aliuawa na wafuasi na viongozi wa Chadema baada ya juhudi zao za kuhonga hela ili waruhusiwe kuendelea kugombea kushindikana.'

Taarifa ya Eliabu inaeleza zaidi kuwa mbali ya kutekeleza mauaji hayo ya kinyama ya Mollel, pia walitaka kumuua kijana mwingine ambaye aliokolewa na polisi akiwa ameikwishambuliwa na sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

'Mbali na kumpondaponda kwa mawe pia walitaka kumuua kijana mwingine kabla hajaokolewa na polisi na sasa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya akiwa na hali mbaya.' inasomeka taarifa hiyo.

Taarifa hii ya Eliabu ni mwendelezo ya madai ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakikihusisha Chadema na baadhi ya makada wake na mauaji wakiwemo viongozi wa juu.

Freeman Mbowe alipata kunyooshewa kidole  akihusishwa na kifo cha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Chacha Zakayo Wangwe kilichotokea eneo la Pandambili mkoani Dodoma na alinusurika kushambuliwa na wananchi wa Tarime alipokwenda kuhudhuria mazishi yake.

Aidha,  Chadema kimekuwa kikihusishwa na matukio mbalimbali ya mauaji katika shughuli zake za kisiasa ikiwemo mikutano na maandamano


MAJALIWA APOKEA WANACHAMA 20 WA CHADEMA BUKOBA MJINI

 


*Wamo Mwenyekiti wa Vijana wa Mkoa, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara,

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa leo amewapokea wanachama 20 kutoka Chama cha Demokrasia (CHADEMA) ambao wameamua kurudi CCM. 

Wanachama hao wameongozwa na Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera, Francis Mutachunzibwa ambaye pia alimtambulisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa BAVICHA, Getrude Ndibalema ambaye alijiuzulu uongozi tangu mwaka jana.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mutachunzibwa amesema: “Ninaijua vizuri CHADEMA, nilipotea, nilitenda dhambi lakini sasa nimeamua kurudi nyumbani, nipokeeni.

“Ninawaomba wana-Bukoba tumchague Dk. Magufuli, mashine ya kusaga na kukoboa, jembe la nguvu. Kuanzia kesho, nitamnadi yeye na Advocate Byabato hadi kieleweke," amesema.

Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba leo jioni, waliojitokeza kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Majaliwa aliwataka wakazi hao wajitafakari sana wanapofikiria kumchangua mtu wa kuongoza nchi.

“Tunataka kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ili umpate ni lazima umjue historia yake. Kuongoza nchi si lelemama, kiongozi wa nchi ni Mkuu wa Nchi, tena ni Mkuu wa Majeshi," amesema Majaliwa.

Majaliwa ambaye ameanza ziara katika Mkoa wa Kagera kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli, ametumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Wakili Steven Byabato, mgombea udiwani wa Kata ya Bilele, Tawfiq Sharif Salum na madiwani wengine wa jimbo hilo.

Aliwasimamisha wazee wa Kagera wakiwemo aliyekuwa Meya wa Bukoba, Dk. Anatoly Amani, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki ambao wote waliomba kura za Dk. Magufuli, Wakili Byabato na madiwani wa jimbo hilo.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Charles Mwijage, amesema Muleba wana ajenda ya kuhakikisha kura zote zinaenda kwa Dk. Magufuli na wabunge wa CCM na akawataka wana-Bukoba nao wafanye hivyo ili kuhakikisha majimbo yote tisa yanabakia CCM na pia wanapata wabunge wanne wa viti maalum.

MSIDANGANYIKE KUHUSU BEI YA KAHAWA - MAJALIWA

 



NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema serikali imedhamiria kuhakikisha kilimo kinamnufaisha mkulima wa Tanzania. 

"Watu wasije kuwadanganya kwamba serikali haiwajali, siyo kweli. Kuna sababu zilizochangia kuyumba kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia."

Ametoa kauli hiyo leo mchana alipokuwa  akizungumza na wakazi wa Rubale Latina mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Rubale, wilayani Bukoba, mkoani Kagera.

"Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, iliazimia kufufua mazao matano ya kimkakati ambayo ni kahawa, pamba, korosho, chai na tumbaku. Mazao haya bei ilishuka na si katika zao la kahawa tu.

"Kuyumba kwa bei haikuwa katika zao la kahawa tu bali katika mazao mengine kama pamba na korosho. Kahawa bei yake iliathirika kwa sababu ya ugonjwa wa Corona. Korosho bei ilishuka kutoka sh.3,300 hadi sh. 1,900. Pamba pia ilishuka bei," amesema. 

Amesema Kenya ndiko mnada wa kahawa huwa unafanyika lakini hadi sasa bado wanasumbuliwa na ugonjwa wa Corona kwa hiyo haikuwa rahisi kufanya biashara katika kipindi chote hicho.

Majaliwa ambaye ameanza ziara katika Mkoa wa Kagera kumuombea kura mgombea irais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli ametumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Jason Rweikiza, mgombea udiwani wa kata ya Rubale, Rwegasira Renatus Rwechungura na madiwani wengine wa jimbo hilo.

Kuhusu maji, amesema sh. bilioni 4.09 zilitolewa ili kuboresha miradi ya maji katika vijiji kadhaa ambayo yote imekamilika. Almevitaja vijiji hivyo kuwa ni  Ibwera, Kasharu, Kitahya, Katale, Itongo, Bituntu, Kibona, Katoro, Mikoni, Kibirizi Ngarama, Ruhoko na Ruhunga.

Saturday, September 26, 2020

KISIWA CHA GANA KUPATIWA KIVUKO KIPYA


NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa kivuko kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.

Ahadi hiyo imetolewa jana (Ijumaa, Septemba 25, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika kitongoji cha Gana.

Katika mkutano huo, Majaliwa alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Ukerewe kupitia tiketi ya CCM, Joseph Mkundi na madiwani. Pia Majaliwa aliwataka wananchi wa Gana wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao wa urais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akitoa ahadi hiyo mbele ya wananchi wa kisiwa cha Gana, Majaliwa alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 yenye kurasa 303. Kivuko hicho kitatoa huduma kati ya Kakuru na Gana.

Alisema Ilani ya CCM imetoa maelekezo kwa Serikali ijayo itekeleze idadi kubwa ya miradi ya kimkakati ikiwemo kuboresha usafiri wa majini ili kuwandolea adha wananchi wanaoishi katika maeneo ya visiwani.  

Majaliwa alisema wananchi zaidi ya 3000 wa Gana, wanahitaji kivuko bora ambacho kitatoa fursa kwao kufanya shughuli za uvuvi na biashara ili kujipatia kipato.

"Hapa Gana tutaleta kivuko, hiki kisiwa ni kikubwa kina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma bora ya usafiri wa majini. Serikali yenu imeweka mipango mizuri kwa ajili yenu," alisema Majaliwa.

Alisema chama kitaendelea kutekeleza Ilani yake kwa vitendo kwa kuboresha huduma za wananchi katika visiwa vyote nchini ikiwemo wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza yenye visiwa 38.

Mbali na kutoa ahadi ya kivuko, Majaliwa alisema Serikali ijayo itapeleka boti za doria kulinda usalama wa wavuvi ambao wakati mwingine wanafanya shughuli zao kwa mashaka wakihofia uvamizi wa majambazi wanaotoka nchi jirani.

Kwa upande wake, Mkundi alisema kipaumbele cha kwanza baada ya kuingia bungeni ni kuhakikisha Serikali ijayo inaboresha huduma ya afya kwa kujenga idadi kubwa ya zahanati ndani ya kisiwa hicho.

"Gana tuna changamoto ya zahanati, umeme na maji. Nitakuwa daraja zuri kati yenu na Serikali ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia kwa haraka naomba mumchague Rais Magufuli ili mambo yetu yaende vizuri," alisema Mkundi.

Paschal Bukuru ambaye ni mfanyabiashara ya duka, alisema ujio wa kivuko utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Gana, kwa kuwa muda mrefu wamekuwa wakitumia mitumbwi kwenda Nansio kufuata mahitaji.

Bukuru alisema wafanyabiashara wamekuwa wakipata changamoto ya kuleta bidhaa zao wakitokea Nansio kwa kuwa hawana usafiri wa uhakika, hivyo ujio wa kivuko hicho utakuwa na manufaa makubwa kwao.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM imeahidi kuboresha vivuko ikiwemo ujenzi wa kivuko cha Rugezi-Kisorya (Mwanza). Pia ujenzi wa vivuko vipya vinane utaanza ambao ni Ijinga-Kahangala (Mwanza), Musoma-Kinesi (Mara), Nyamisati-Mafia (Pwani), Msangamkuu-Msemo (Mtwara), Nyakalilo-Kome (Mwanza), Bwiro-Bukondo (Ukerewe), Irugwa-Murutanga (Ukerewe) na Kakuru – Ghana (Ukerewe).

 

KIWANDA CHA TANGAWIZI SAME KUANZA UZALISHAJI NOVEMBA

 






NA PIUS NTIGA, SAME

KIWANDA cha kuchakata zao la Tangawizi kilichopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kitaanza kuchakata zao Novemba mwaka huu baada ya kupata mwekezaji.

Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2012 kikimilikiwa na Chama cha Ushirika cha Tangawizi Mamba, Miamba lakini kiliharibika muda mfupi baadaye na hivyo kusikitisha shughuli zake.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa (PSSSF), Fortunatus Magambo ambao ndiyo mwekezaji mpya wa kiwanda hicho jana amekabidhi kwa menejimenti mashine za kuchakata Tangawizi zilizotolewa na mfuko huo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule

Katika mkutano na wananchi wa Mamba, Miamba ambao ulihudhuriwa pia na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM kijijini hapo, Magambo amesema mashine hizo za kisasa zimenunuliwa nchini China kwa gharama ya sh bilioni 1.83  na zinafanya kazi bila kutoa sauti.

Kwa mujibu wa ubia huo, PSSSF ina hisa ya asilimia 60 huku 40 zikiwa za wananchi wa Wilaya ya Same ambao zao lao kuu la Biashara ukiachia Mkonge ni Tangawizi.

Aidha, amesema kiasi cha sh milioni 800 zitatumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya kiwanda, ofisi, hospitali, Karakana na miundombinu pamoja na matumizi ya awali ya kiwanda hicho.

"Tunataka kuona mradi huu unakamilika na kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Same na utakamilika kwa wakati

"Wataalamu kutoka China wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kufunga mashine hizi tayari kwa kuanza uzalishaji," alsema Magambo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, amewaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa serikali ya awamu tano imejipambanua kuwa ni ya Tanzania ya viwanda, hivyo uwepo wa kiwanda hicho utachochea kukuza vipato vyao na taifa kwa ujumla.

Amesema tani 5,000 kwa mwaka zinahitajika kiwandani hapo, hivyo akawataka wakulima kuongeza uzalishaji wa Tangawizi ambayo itakuwa inasindikwa hapa hapa nchini kwa matumizi ya hapa nchini na nje ya nchi.

Aidha, DC Rosemary amesema soko la Tangawizi litakuwa kubwa baada ya uzalishaji kuanza.

Pia amewataka wananchi kuwapuuza Wanasiasa wakiwemo wa upinzani wanaojipitisha kwao wakidai kuwa mashine za kiwanda hicho wamezileta wao wakati zimeletwa na serikali ya awamu ya tano.

"Wananchi wangu wa Same hasa hapa Mamba,  Miamba, Corona ilichelewesha ufungaji wa  mashine hizo lakini sasa zipo hapa na nyie leo mmeshuhudia, hivyo muda wowote zitaanza kufanya kazi, endeleeni kuiunga mkono serikali yenu" alisema DC Rosemary

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM, baadhi ya wananchi akiwemo Mzee Ndimangwa Manento, aliyetoa shamba lake kwa ajili ya kujengwa kiwanda hicho cha Tangawizi, wameishukuru serikali kwa kusikiliza kilio chao cha kuleta mashine za kisasa zisizo na sauti na akawaomba wananchi wenzake mwaka huu wasifanye makosa katika uchaguzi mkuu wakampigie kura nyingi Rais Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM.

Wakati huo huo, zaidi ya sh milioni 400 zimetumika kujenga majengo mapya ya kituo cha afya cha Ndungu ikiwemo maabara, chumba cha kuhifadhi maiti, jengo la upasuaji, pamoja na wodi ya akina mama wajawazito. 

Hayo yamesema na Afisa Mipango wa Halmashauri ya Same,  Simion Mzee wakati akizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM.

Nao baadhi ya wananchi wa Ndungu akiwemo Hatibu Mlindoko, wamepongeza serikali kwa kuwajengea kituo hicho cha afya na wakaiomba kupandisha hadhi kituo hicho ili kiwe  Hospitali.

Kaimu Mganga Mkuu kituo hicho, Hamis Waziri Juma amesema kabla ya majengo hayo walikuwa wanatoka rufaa nyingi kwenda Hospitali ya Wilaya ya Same kwa ajili ya matibabu lakini sasa wajawazito wanajifungua katika kituo hichi na hivyo kupunguza gharama ya wanachi kuwapeleka Same.

Katika hatua nyingine, zaidi ya sh milioni 60 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa shule Kongwe ya Sekondari ya Same katika miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.

Mkuu wa Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 Mwalimu Hoza Mgonja, amesema  Majengo 24 yamekarabatiwa yakiwemo Mabweni, Jiko,  Madarasa, Maabara, Zahanati, Ofisi na kujenga Tenki la Maji kwa ajili ya matumizi ya Shule hiyo ambayo sasa ni ya Kidato cha Tano na Sita.

Wakizungumzia mafanikio hayo baadhi ya Wanafunzi wamesema Shule hiyo sasa imekuwa ya kisasa baada ya Majengo ya zamani kubadilishwa na kujengwa mapya imesaidia pia kuongeza ufaulu na walimu kufundisha katika mazingira mazuri na wameipongeza Serikali.

Aidha, shilingi Milioni-25 zimepelekwa na serikali kukarabati na kujenga  Ofisi na Madarasa Mawili katika Shule ya Sekondari Mamba, iliyopo Kata ya Mamba, Miamba Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.

Kiasi hicho cha fedha kimetajwa na Mkuu wa Shule hiyo Elizabet Irira, ambaye pia ameipongeza serikali kwa kupeleka kiasi hicho cha fedha Shuleni hapo, hatua ambayo pia imepongezwa na Wanafunzi wa Shule hiyo iliyopo Milimani Kilometa 90 kutoka Mjini Same hadi Mamba, Miamba.

Friday, September 25, 2020

SABUNI ILIYO PIGWA MNADA NA TRA SIYO SALAMA




NA MWANDISHI WETU

SABUNI ya Unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha lakini imeuzwa kwa njia ya mnada na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) siyo salama hivyo haifai kutumiwa.

Tahadhari hiyo imetolewa jana na afisa mwandamizi wa Shirika la Viwango (TBS), jina lake tunalihifadhi wakati akizungumza na TANZANIA PANORAMA kuhusu madhara yanayoweza kuwapata watu watakaotumia bidhaa hiyo.

Akijibu hilo, amesema ni kosa kuuza au kusambaza bidhaa ambayo muda wake wa matumizi umeisha na siyo salama kuitumia ingawa matatizo ya kiafya yanayoweza kumpata mtumiaji ni suala la kitabibu na inategemea kemikali zilizotumika kuitengeneza.

"Matatizo ya kiafya ni suala la kitabibu na inategemea kemikali gani kwa sababu sabuni zinatofautiana 'composition' ya kemikali lakini itoshe tu kusema tu bidhaa yoyote iliyo'expire' haifai na siyo salama kwa matumizi na anayeuza hatendi haki," alisema afisa huyo.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema wanaoweza kulizungumzia ni TBS.

Mapema mwezi huu TRA imeuza kwa njia ya mnada shehena ya sabuni ya unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha.

Shehena hiyo ya sabuni isiyofaa kutumika baada ya muda wake kuisha iliingizwa nchini kutoka nje na kukaa bandarini bila kulipiwa ushuru kwa muda mrefu kabla TRA haijaamua kuiuza.

Habari za uhakika zilizokusanywa na TANZANIA PANORAMA zimeonyesha kuwa shehena hiyo ni ya mifuko 1,800' ya sabuni ya unga aina ya AKO na imeuzwa kwa njia ya mnada na maafisa wa TRA huku wakijua kuwa wanatenda kosa linaloweza kuwa na athari mbaya kwa watakaoitumia sabuni hiyo.

Thamani ya sabuni hiyo ni sh milioni 300 na kabla ya kunadiwa ilikuwa imehifadhiwa katika bandari kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alithibitisha kuuzwa kwa shehena hiyo ingawa kabla ya kuthibitisha alikanusha na kutaka atumiwe ushahidi.

Katika majibu yake, Kayombo alisema "Sasa bwana ni hivi. Ni kweli huo mzigo unaousema ni kweli ulikuwepo TRA. Ni kweli kabisa. Na mnada wake wa kwanza ulikuwa Agosti 24, 2020 lakini aliyeshinda hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndiyo ukauzika

" Ni kama kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zikiushindania kwa sababu yule mnunuzi wa kwanza hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndipo shehena ile ikachukuliwa kwa sh. milioni 21.5."

DK. TULIA- SAFARI HII TUNALALA TUNAPOKULA

 



NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Tulia Ackson jana amepiga hodi katika Kata ya Sinde kuomba kura huku akiwa amebeba ujumbe unawaotaka wananchi wa jimbo hilo kulala wanapokula.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi, Dk Tulia amesema watu waliozowea kula kwa dada na kulala kusikojulikana waanze kujiandaa kwenda kulala wanakokula.

Dk Tulia amewaomba wananchi wa Kata ya Sinde kukipa ridhaa ya uongozi CCM kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kumchagua Rais John Pombe Magufuli kuwa Rais, kumchagua yeye kuwa Mbunge na pia kuwachagua madiwani wa CCM.

Amesema  wananchi wa Kata ya Sinde wana kila sababu ya kumchagua Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu ili apate fursa ya kukamilisha kazi kubwa na ya kutukuka anayolifanyia taifa.

"Ninapokuja hapa kwenu ndugu zangu mimi siyo mgeni, kuna watu wanasikika huko wakisema kwamba tunakula kwa dada halafu tutalala sijui wapi… safari hii tunalala tulipokula. Kura yetu safari hii tutaipeleka kwenye maendeleo na maendeleo safari hii hapa Mbeya ni CCM tu.

“Mpaka hapa ninapozungumza na nyie baada ya kushuhudia mafuriko ya watu waliojitokeza kuungana nasi katika maeneo ya Kata za Nzovwe, Isyesye, Igawilo, Sinde na mahali kwengineko mimi mbunge wa kujiongeza nilishafanya 'connection'.

"Hapa ninapozungumza, mipango kazi ipo tayari, watu wanafanya usanifu ili miundombinu yetu ikae sawa.

“Watu wa Mbeya safari hii tunaenda kwa kasi ya kujiongeza na kasi hii inatoka Chama Cha Mapinduzi pekee, pigieni kura zote CCM mjionee maendeleo yatakavyoinuka kwa kasi ya ajabu. Mtu akija kwenu kuwapiga propaganda muulizeni umetufanyia nini kabla ya kuja hapa kuomba kura?” Dk. Tulia.

IRUGWA KUPATA KITUO CHA AFYA

 



NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itajenga kituo kipya cha afya katika Kata ya Irugwa, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu wananchi wa kata hiyo kufuata huduma za kitabibu

Akizungumza leo na wakazi wa Kata ya Irugwa wakati wa mkutano wa kumuombea kura mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais John Magufuli, amesema uamuzi huo unakwenda sambamba na ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020 - 2025.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amesema  katika ilani ya uchaguzi ya 2020-2025, ukurasa wa 186 unasomeka, "hadi  kufikia 2025 serikali itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asimilia 20 ya vituo 8,446 vilivyopo sasa; vipaumbele vitawekwa  katika ujenzi wa vituo vya afya na ukamilishwaji wa maboma kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia, idadi ya watu na wingi wa wagonjwa."

Amesema Serikali ya Rais Magufuli imekwishatoa sh milioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo moja la kujifungilia  katika zahanati Irugwa.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi, alisema ilani imeweka mipango imara ya kushughulikia upatikanaji wa maji vijijini kama hatua ya kutekeleza azma ya Rais Magufuli  ya kumtua mama ndoo kichwani.

Kuhusu usafiri wa majini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ya CCM ikiingia madarakani inakusudia kujenga vivuko mbalimbali kikiwemo kivuko cha Irugwa, Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi Kisorya.

" Kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya CCM, ukurasa wa 83 hadi 84, Chama Cha Mapinduzi kimeielekeza serikali ikamilishe ujenzi wa vivuko vipya nane kikiwemo cha Irugwa - Murutanga wilayani Ukerewe.

"Pia ilani imeelekeza serikali ianze kutekeleza mradi wa ujenzi wa maegesho ya Lugezi - Kisorya mkoani Mwanza, Kome na Nyakalilo mkoani Mwanza, Utete huko Pwani, Chato- Nkome huko Geita, Iramba na Majita mkoani Mwanza na Irugwa," alisema.

 

DMO MANYONI ASEMA UJENZI ZAHANATI YA NTOPE HAUJAKAMILIKA TANGU 2012

 

Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Ntope  kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida ambalo ujenzi wake ulianza 2013. Mradi huu unadaiwa kughubikwa na vitendo vya ufisadi

NA MWANDISHI WETU

MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Manyoni (DMO) Furaha Mwakafula amesema ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya  ya Manyoni mkoani Singida haujakamilika kwa miaka minane sasa kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwakafula ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na TANZANIA PANORAMA kuhusu kukwama kwa ujenzi wa zahanati hiyo na madai ya ufisadi dhidi ya fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi huo.

Amesema mbali na zahanati hiyo, ujenzi wa nyumba ya daktari wa kijiji ulikamilika na ilianza kutumiwa na mtumishi ambaye hakuwa wa kada ya afya aliyepewa na uongozi wa kijiji.

"Taarifa nilizonazo mimi ni kwamba ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2012, katika bajeti ya mwaka 2012/2013 zilitolewa sh milioni 20 zikatumika kujenga sehemu ya boma ambalo halikukamilika na tangu wakati huo haijatolewa fedha nyingine. Kwa hiyo ujenzi umekwama kwa miaka yote hiyo kwa sababu ya ukosefu wa fedha," alisema Mwakafula.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa zilitolewa sh milioni 60 ila zilizoelekezwa kwenye ujenzi ni sh milioni 20 huku sh milioni 40 zikihamishiwa kwenye fungu lisilojulikana na hazijapata kurejeshwa hadi sasa alisema hizo zinaweza kuwa hisia za watu au upotoshaji wa makusudi.

"Kuna mambo mawili hapo ambayo ni vizuri yaeleweke, moja ni kwamba kuna fungu la fedha kutengwa kwenye bajeti na kuna fungu la fedha husika kupelekwa na kupokelewa kwenye mradi. Sasa mimi nimethibitishiwa na wataalamu wa mipango kuwa fedha iliyotolewa na kutumika kwenye mradi huo ni sh milioni 20 tu," alisema Mwakafula.



Aidha mganga mkuu huyo alisema mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba ya daktari ulioanza sambamba na zahanati ya Ntope ulikamilika na uongozi wa Kijiji cha Ntope uliitoa nyumba hiyo itumiwe na mtumishi wa serikali ambaye hakuwa wa kada wa afya hadi ilipoharika paa.

"Kuhusu nyumba ya daktari yenyewe ilikamilika na uongozi wa kijiji uliitoa kwa mtumishi ambaye hakuwa wa kada ya afya. Huyo aliitumia hadi ilipoezuka paa lake. Hivi sasa ndiyo tunafikiria kuitengeza ili ianze kutumika kama zahanati ya kijiji," alisema.

Aidha, Mwakafula alisema taarifa kuwa zahanati ya Kijiji cha Ntope ambayo haijawahi kutoa huduma hupewa mgao wa dawa kutoka MSD ni za kweli na dawa hizo huwa zinaelekezwa zahanati za jirani ambazo zinawahudumia wananchi wa Kijiji cha Ntope.

" Hilo kweli fungu la fedha za dawa katika zahanati ya Ntope huwa linatoka kila mwaka lakini kwa sababu haipo fedha hizo huwa zinaelekezwa zahanati za jirani ambazo zinatoa huduma kwa wananchi wa Kijiji cha Ntope," alisema.

Daktari Mwakafula amefanya mahojiano na TANZANIA PANORAMA na kutoa ufafanuzi huo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Jackson kueleza kuanza kuwa anafuatilia madai ya ufisadi katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope.

SERIKALI YATUMIA BIL 3.29 KUKARABATI SHULE ZA MSINGI


 

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imetumia shilingi bilioni 3.29 kukarabati na kugharamia shughuli za utawala, michezo, mitihani na posho kwa maafisa elimu kata na walimu wakuu kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2019/2020.

Fedha hizo zimetolewa na serikali kupitia mpango wa elimu bila malipo unaotekelezwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ambao hadi sasa umezinufaisha pia shule za sekondari 23.

Hayo yameelezwa jana na Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majukwaa ya kisiasa wilayani Ukerewe ambako amefika akiwa katika mfululizo wa ziara zake nchi nzima za kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema katika utekelezaji wa mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa lipa kutokana matokeo (EP4R) ulioanza kutekelezwa 2015 hadi 2020, sh milioni 309 zilitolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na ofisi kwa shule mbalimbali zikiwemo Kalandero, Murutunguru na Kakerege.

Alisema kiasi kingine cha sh milioni 873 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule za sekondari mbalimbali nchini zikiwemo Bukongo, Pius Msekwa, Bwisya, Muruti na Lugongo.

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa ilimfikisha katika Kisiwa cha Bwisya kilichoko Kisiwa cha Ukara ambako alitembelea Kituo cha Afya cha Bwisya na kukagua wodi ya wanaume na ya Wazazi.

Kabla ya kukagua kituo hicho, Waziri Mkuu Majaliwa alifika kwenye mnara wa kumbukumbu ya watu waliokufa kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere, Septemba 20, 201  ilikofanyika ibada fupi ya kuwaombea marehemu ikiongozwa na Padre Peter Paul wa Parokia ya Nyamwaga, Ukere na Sheikh Mudhakiru Maguza wa Msikiti wa Bwisya

ACT WAZALENDO CHAMKINGIA KIFUA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD

 



NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kimemwandikia barua msajili wa vyama vya siasa, kikijibu barua yake iliyotaka kujieleza kwa kukiuka masharti ya kifungu cha 11 A cha sheria ya vyama vya siasa kikimtaka arejee na kufahamu tafasiri sahihi ya kifungu hicho.

Barua hiyo ya Septemba 24, 2020 yenye kumbukumbu namba ACT/HQ/MSJ/023/Vol.III/248 inamtaka msajili afahamu maana,  tafasiri sahihi na tofauti ya vyama kuungana chini ya kifungu hicho na mgombea mmoja kuonyesha imani yake kwa mgombea mwingine katika uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo imesainiwa na Jaran Bashange kwa niaba ya katibu mkuu, mgombea mmoja kuonyesha imani kwa mgombea mwingine ni jambo la kupigiwa mfano kwa siasa za Tanzania kuwa licha ya ushindani wa kisiasa, umoja na mshikamano kama Watanzania unadumishwa.

Sehemu ya barua hiyo ambayo TANZANIA PANORAMA imeoina inasomeka; 'nakiri kupokea barua yako ya tarehe 22 Septemba, 2020 yenye kumbukumbu namba HA.322/362/21/90 inayotutaka tuwasilishe maelezo juu ya mgombea wetu wa urais wa Zanzibar, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad kumuombea kura mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tundu Antipas Lissu

'Katika barua yako umetukumbusha uwepo wa kifungu cha 11 A cha sheria ya vyama vya siasa kinachoweka utaratibu wa vyama "kushirikiana" na ukaenda mbali kuwa  kwa vyama kushirikiana bila kufuata utaratibu uliowekwa ni kukiuka sheria.



'Tunapenda kueleza kuwa mgombea wetu wa urais wa Zanzibar, mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad hajakiuka kifungu cha 11 A cha sheria ya vyama kinachoweka utaratibu wa vyama kuungana au vinavyokusudia kuungana kabla au baada ya uchaguzi.

'Aidha, mheshimiwa Seif Sharif Hamad hakumuombea kura ndugu Tundu Antipas Lissu kama inavyodaiwa na ofisi yako. Video clip uliyotutumia haina maneno hayo na nikuombe urejee kuisikiliza upya kwa makini .

'Alichokisema mgombea wetu ni imani yake kuwa ndugu Tundu Antipas Lissu atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo ambalo liko wazi sana kutokana na mwelekeo wake wa kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.

'Hii inathibitishwa na namna wananchi wengi na kwa hamasa kubwa wanavyojitokeza katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea. Hilo si kosa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.

'Kauli na imani hiyo haina tafasiri ya kuungana kwa vyama vyetu vya Alliance for Change and Transparent (ACT Wazalendo) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ila chama chetu kina Imani kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chama Cha Mapinduzi, Ndugu John Pomne Magufuli hatakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi wa tarehe 28 Oktoba, 2020.'

Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilikiandikia ACT ikikitaka kitoe Maelezo kuhusu hatua ya Maalim Seif kumuombea kura mgombea urais wa Chadema, Lissu.

 

"VITAMBULISHO VYA WAMACHINGA VIMETUTUA MZIGO"



NA PIUS NTIGA, MOSHI

WAFANYABIASHARA wadogo, maarufu kwa jina la Machinga katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamesema vitambulisho wa wajasiriamali wadogo vimewatua mzigo hivyo wanawashangaa baadhi ya wanasiasa wanaopotosha kuhusu vitambulisho hivyo.

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM inayoangazia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, wafanyabiashara hao wamesema utamu wa vitambulisho hivyo wanaujua wao.

Wamesema awali walikuwa wanalipa shilingi 500 kwa siku, sawa na shilingi 182,000 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na shilingi 20,000 wanayolipa sasa kwa mwaka.



"Tulikua tukilipa shilingi 200 ya usafi kwa siku, sawa na shilingi 73,000 kwa mwaka, ambapo sasa mateso kama hayo hatuyapati. Tena tunashukuru sana Rais Magufuli kwa kutuona na tutampa zawadi mwaka huu" wamesema Machinga.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao wadogo, mkombozi wao ni Rais Magufuli ambaye amekuja na mpango wa sh  20,000 tu kwa mwaka na sasa kero za mgambo kuwafukuza hazipo tena.

"Nikwambie tu kuwa mabenki nayo yamesema kwa kuwa tuna vitambulisho, shughuli zetu zimerasimishwa hivyo tumeanza kupewa mikopo huku vitambulisho vikiwa ni dhamana yetu". wamesema

Wamesema hivi sasa hawasumbuliwi tena na askari wa jiji wala mgambo kama ilivyokuwa hapo awali.

"Vitambulisho vya wamachinga vimetusaidia sana, tunanunua kwa ridhaa yetu, hatulazimishwi". wamesema Machinga.

Aidha, wamefafanua kuwa uwepo wa vitambulisho hivyo umewaondolea kero na kwa sasa biashara yao imeimarika zaidi na kipato chao kimeongezeka na wamefanikiwa kununua ardhi na kujenga nyumba.

Kutokana na mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, amesema tangu kuanza kwa utaratibu huo zaidi ya asilimia 70 ya wamachinga wamepatiwa vitambulisho katika Manispaa ya Moshi.

Mwandezi amesema fedha inayotokana na vitambulisho hivyo inakwenda Hazina na kisha kurudishwa katika Manispaa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawagusa moja kwa moja wananchi.



"Pia tumewasaidia hawa wajasiriamali kuwajengea uwezo wa kimtaji ambapo sasa wanakopesheka kupitia vitambulisho, hivyo vimewanufaisha kwa kukopa fedha benki," amesema Mkurugenzi huyo

Hivi karibuni baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipotosha kuhusu vitambulisho hivyo vya wamachinga kuwa haviwanufaishi na badala yake wanaibiwa, kauli ambayo Rais John Magufuli ambaye ni mgombea wa urais kupitia CCM, amewataka wafanyabiashara hao kuwapuuza wanasiasa na badala yake waunge juhudi za serikali za kuwakomboa Wamachinga. 

MAJALIWA AAHIDI MAPITIO MAPYA TOZO SEKTA YA UVUVI


 

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa aseme serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero Watanzania wanaojishughulisha na uvuvi.

Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mji wa Nansio Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli.

Amesema katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, serikali iliondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio.

"Pia tumepunguza ada ya leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji baridi. Serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero wavuvi.

" Tumeweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa vifaa bora vya uvuvi, kuzuia uingizaji na uzalishaji wa zana haramu za uvuvi na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa zana na vyakula vya samaki," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.


TRA YAUZA SHEHENA YA SABUNI ISIYOFAA

 



NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)  imeuza kwa njia ya mnada shehena ya sabuni ya unga ambayo muda wake wa matumizi umeisha.

Shehena hiyo ya sabuni isiyofaa kutumika baada ya muda wake kuisha iliingizwa nchini kutoka nje na kukaa bandarini bila kulipiwa ushuru kwa muda mrefu kabla TRA haijaamua kuiuza.

Habari za uhakika zilizokusanywa na TANZANIA PANORAMA zimeonyesha kuwa shehena hiyo ilikuwa na mifuko 1,800' ya sabuni ya unga aina AKO na imeuzwa kwa njia ya mnada na maafisa wa TRA huku wakijua kuwa wanatenda kosa linaloweza kuwa na athari mbaya kwa watakaoitumia sabuni hiyo.

TANZANIA PANORAMA limedokezwa na vyanzo vyake vya habari kuwa shehena hiyo ambayo thamani yake ni sh milioni 300, ili kuwa imehifadhiwa katika bandari kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam na imepigwa mnada mapema mwezi huu kwa sh milioni 20

"Watanzania tunaumizana wenyewe kwa wenyewe. Sabuni iliyopigwa mnada na TRA imekwisha muda wake wa matumizi na TRA walilijua hilo. Sasa wameiingiza mtaani bila kujali kama itasababisha magonjwa kwa watakaoitumia,  wewe waulize uone kama watajibu, watababaisha tu maana wanajua siku hizi hakuna watu wa kichumbua mambo," alisema mmoja wa watoa habari wa TANZANIA PANORAMA.

Alipoulizwa juzi, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo  haraka haraka alikanusha kuwa taarifa hizo hazina ukweli na kutaka atumiwe ushahidi wa uwepo wa shehena hiyo na alipotumiwa sehemu ndogo ya ushahidi aliotaka aliomba apewe muda kidogo afuatilie.

Hadi juzi jioni Kayombo alishindwa kutoa majibu kwani kila alipopigiwa alisema maafisa wanaohusika na minada na wale wa forodha wote wametoka ofisini hivyo anaendelea kuwasubiri na alipoombwa namba zao za simu alikataa kutoa.

Jana asubuhi,  TANZANIA PANORAMA lilimtafuta tena Kayombo ili kuzungumzia tuhuma hizo lakini hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya kiganjani akikumbushwa ahadi yake ya kutoa kauli kuhusu tuhuma hizo na pia kutimiza wajibu wake alijibu kuwa kuna taarifa moja anaisubiri kutoka kwa wahusika wa mnada.

TANZANIA PANORAMA lilimtumia ujumbe mwingine likimshauri awe anapokea simu yake na kutoa taarifa hata kama hajafanikiwa kupata majibu husika na yeye alijibu kuwa akiwa kwenye kikao huwa hapokei simu kwa sababu siyo nidhami nzuri.

Baadaye mchana, Kayombo alitafutwa tena lakini hakujibu chochote na majira ya jioni alipiga simu na kueleza kuwa ni kweli shehena hiyo ya sabuni ilikuwepo TRA na imeishauzwa lakini haweza kusema kama muda wake wa matumizi umeishaisha au bado.



"Sasa bwana ni hivi. Ni kweli huo mzigo unaousema ni kweli ulikuwepo TRA. Ni kweli kabisa. Na mnada wake wa kwanza ulikuwa Agosti 24, 2020 lakini aliyeshinda hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndiyo ukauzika

" Ni kama kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zikiushindania kwa sababu yule mnunuzi wa kwanza hakuja kulipa hivyo ikabidi ufanyike mnada mwingine ndipo shehena ile ikachukuliwa kwa sh. milioni 21.5 ," alisema Kayombo.

Alipoulizwa mnada wa pili uliofanyika lini na kukumbushwa kujibu swali aliloulizwa kuwa TRA inadaiwa kuuza shehena ya sabuni iliyokwisha muda wa matumizi huku ikijua kuwa inaweza kuwa na athari mbaya kwa watumiaji alisema maswali hayo hawezi kuyajibu.

"Hivi unaandikia chombo gani siku hizi........  Sasa hayo maswali mengine mimi siwezi kuyajibu we fahamu tu mnada umefanyika mara mbili," alisema Kayombo.

Thursday, September 24, 2020

SERIKALI YATUMIA BILIONI 58 KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI UKEREWE

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imekamilisha ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika Wilaya ya Nansio mkoani Mwanza kwa gharama ya sh bilioni 58.

Hayo yameelezwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa Nansio jana katika uwanja wa Getrude Mongela.

Majaliwa ambaye yuko katika ziara ya kisiasa nchi nzima ya kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais John Pombe Magufuli, amesema kati ya fedha hizo, sh bilioni 13 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji ikiwemo sh bilioni 10.9 za uboreshaji wa huduma ya maji safi mjini Nansio utakaonufaisha wananchi 108,653.

Amesema sh bilioni 2.1 zimetumika kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafi wa mazingira  mjini Nansio.

Ameitaja miradi mingine ya maji iliyokamilishwa na Serikali ya Rais Magufuli kwa gharama ya sh bilioni 1.3 kuwa ni ukarabati wa mradi wa maji wa Irugwa,  mradi wa maji ya bomba ya Nansore, mradi wa maji wa Muriti/ Ihebo, upanuzi wa mradi wa maji wa Chabilungo na upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Kazilankanda.

TANZANIA YASIFIWA KWA SERA BORA ZA UWEKEZAJI

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajab Kundya (mwenye suti nyeusi) akifanya mahoajino na waandishi wa Uhuru FM - Amsha Amsha 2020, Suti katika Shamba la Maua la Mwekezaji raia wa Uholanzi.

NA PIUS NTIGA, MOSHI

TANZANIA imesifiwa kuwa ina sera nzuri ya uwekezaji ambayo imekuwa kichocheo cha upatikanaji wa ajira na ukuaji wa uchumi.

Hayo yameelezwa leo na mwekezaji Fons Nijenhuis katika mahojiano na Amzha Amsha 2020 ya Uhuru FM shambani kwake Dakau, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ameema zaidi ya ekari 250 zinatumika katika uwekezaji wa sh bilioni 6  tangu mwaka 2003 na kufanikiwa kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 1,000 katika shamba la maua la Vasso.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka  2015/2020 iliyoahidi kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kama njia moja wapo ya kuongeza ajira kwa Watanzania

Fons Nijenhuis, amesema uwekezaji huo umetoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na pia umesaidia kuchangamsha eneo hilo kibiashara na hivyo kuinua Uchumi.



Aidha, amesema amefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi wanozunguka shamba hilo ambao miongoni mwao wameanzisha kilimo cha maua wanayoyauza kwake.

"Ngoja nikwambie hapa mimi nimefanikiwa kufundisha ujuzi wananchi wapo kama 40 hivi hawa wote wana mashamba hapo nje na maua yao huwa wananiuzia mimi na huwalipa kiasi cha shilingi milioni kama moja hivi kila wiki wanaponiuzia" anasema Mwekezaji.

Kwa mujibu wa mwekezaji huyo kila wiki husafirisha zaidi ya tani 250 za miche ya maua nje ya nchi na sehemu ya fedha zake hutumika pia kufanya ukarabati wa huduma katika vijiji vitatu vinavyozunguka shamba hilo.

Amesema katika shamba hilo anatumia tani 500 za udongo ambazo huziagiza kutoka nchini Uholanzi na kwamba udongo wa hapa nchini hautoshelezi.



Aidha, amesema anaendelea kufanya mazungumzo na serikali ili kuangalia uwezekano wa kuwa anatumia udongo wa hapa nchini ambao unapatikana Wilaya ya Pangani, Mkoa waTanga ili pesa anayotumia kuagiza nje udongo ibaki hapa hapa nchini.

"Sehemu kubwa ya wateja wangu wapo nchini China na Uholanzi ambako huuza hii Miche ya Maua," alisema

Kwa upande wake, Afisa Kilimo Halmashauri ya Moshi Vijijini, Mercy Urio amesema uwekezaji huo umeleta manufaa makubwa kwa jamii na Halmashauri ya Moshi vijijini na wananchi kwa ujumla wanajivunia uwepo wa mwekezaji huyo.

Nao wanufaika wa uwekezaji huo, Agnes Shofa, Justina Mushi pamoja na Benard Erasto wamesema kwa sasa maisha yao yamebadilika ukilinganisha na awali walivyokuwa kwani wamefanikiwa kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba mpya.

Naye meneja wa shamba hilo, Alany Njau, amevitaja vijiji vitatu vinavyonufaika na uwekezaji huo kuwa ni pamoja na kijiji cha Umbwe, Ucharo pamoja na Dakau na wamekuwa wakifundisha ujuzi kwa wananchi wa namna ya kupandikiza pia Vikonyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaj Rajab Kundya, aliambatana na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru Fm, katika shamba hilo amesema mafanikio yote yamepatikana kutoka na uongozi thabiti wa Rais Dk. John Magufuli na kusisitiza kuwa chanda chema huvikwa Pete.


Aidha, mkuu huyo wa Wilaya ya Moshi, amesema shamba hilo la maua ni moja ya mashamba 11 yaliyopo katika wilaya hiyo na  yameendelezwa vizuri kupitia vyama vya ushirika.

"Kuna changamoto kadhaa ambazo hujitokeza kwa mwekezaji huyo lakini tumekuwa tukikaa pamoja kuzitafutia ufumbuzi wa kina"Amesema DC wa Moshi.

Amesema wanafarijika kuona maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha kutumia mvua kinapitwa na wakati na serikali inahakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa vizuri ili kuleta chachu katika kilimo cha Umwagiliaji.

Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020 /2025 imeahidi kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika kilimo cha Kisasa cha biashara hususani ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji.

Kutokana na mafanikio hayo na ahadi zinazotolewa na CCM, Amsha Amsha kazi yake kubwa ni kumkumbusha  mtanzania  Oktoba 28 mwaka huu asifanye makosa akachaguze viongozi wakaowaletea maendeleo ya haraka wanaotokana na CCM.