banner

Wednesday, September 23, 2020

RAIS MAGUFULI NI ALFA NA OMEGA - ;MAJALIWA

 



NA MWANDISHI WETU

RAIS John Pombe Magufuli ndiye mtu pekee  mwenye uwezo wa kiungozi kati ya wote waliojitokeza kugombea urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Hayo yameelezwa jana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Kata za Lubuga na Ilungu zilizopo Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.

Waziri Mkuu Majaliwa yupo katika ziara ya kisiasa ya nchi nzima ya kumnadi mgombea urais wa CCM, Rais Magufuli na amekuwa akitumia majukwaa ya kisiasa kuwanadi pia wagombea ubunge na udiwani wa CCM.

"Rais Magufuli anastahili kupewa nchi kwa sababu ana uwezo wa kuisimamia. Tanzania imekosa maendeleo ya haraka kwa sababu kulikuwa na tabia ya watu wachache ya kula rushwa na kuwaathiri wananchi wa chini wasipate mafanikio. Tunataka kiongozi wa nchi anayeweza kupambana na rushwa na mafisadi. Na huyo ndiye kiongozi tunayemtaka," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema chini ya uongozi wa Rais Magufuli, sera ya tiba kwa akinamama wajamzito na watoto na wazee ni bure. Huduma ya mama mjamzito kujifungua ni bure na kwamba Serikali ya Rais Magufuli imekwishatoa sh bilioni 10.8 kwa ajili ya huduma hizo.

" Tunayo Bima ya Afya ambayo tunataka tuiimarishe ili iwe ya kitaifa. Na leo tayari tunao muswada wa Bima ya Afya, tunataka tuunganishe wafanyakazi na wananchi wa kawaida ili watanzania wote wawe na Bima ya Afya.

"Si kila mara mtu anakuwa na pesa taslimu wakati anapopata mgonjwa kwenye familia  na ndiyo maana inasisitizwa Watanzania wote wawe na Bima ya Afya.

" Unapata kadi wewe na mkeo au mumeo na wategemezi wanne. Leo tuna watoto wanatoka Magu lakini wanasoma Chuo Kikuu cha Dodoma. Una mtoto yupo hapa lakini anasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, una mtoto mwingine anasoma Bwiru, akiugua huko na kuulizwa kitambulisho anatambulika kuwa ni mtoto wa fulani, anatibiwa.

"Haya yote niliyoyasema yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Dk Magufuli na ndiyo sababu leo namuombea kura ili awe Rais wa nchi hii," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aliongeza kuwa Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh bilioni 1.4 kwa Wilaya ya Magu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya .

Alisema kituo cha Afya cha Kahangara kimepata sh milioni 500 na ujenzi wake umekamilika, kituo cha Afya Lugeye kimepata sh milioni 500 na ujenzi wake umekamilika na Kituo cha Afya Kabila kimepata sh milioni 400 na ujenzi wake upo katika hatua za mwisho.

Akizungumza kuhusu fedha za ununuzi wa dawa, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh bilioni 10.1 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba kila mwezi Wilaya ya Magu inapokea wastani wa sh milioni 108.

Kuhusu ujenzi wa barabara, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali ya Rais Magufuli imetoa sh bilioni 10 kupitia TARURA na TANROADS kwa ujenzi, matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi na madaraja kwa barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami ya Magu mjini yenye urefu wa kilomita 5.7  ambayo tayari imekamilika ikiwa imegharimu sh bilioni 2.7

Alizitaja barabara nyingine kuwa ni Kisesa - Bujora yenye urefu wa kilomita 0.4 ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami, barabara ya Usagara - Kisesa yenye kilomita 16.14 kwa kiwango cha lami na usanifu wa kina wa barabara ya Magu - Ngudu - Hungumalwa yenye urefu wa kilomita 70.

DC MANYONI AFUATILIA TUHUMA ZA UFISADI ZAHANATI YA NTOPE

 


Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Ntope  kilichopo Kata ya Sanza, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida ambalo ujenzi wake ulianza 2013. Mradi huu unadaiwa kughubikwa na vitendo vya ufisadi


NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya Manyoni mkoani Singida, Rahabu Jackson amesema anafuatilia madai ya ufisadi katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ntope iliyopo Kata ya Sanza mkoani Singida.

Akizungumza na TANZANIA PANORAMA BLOG leo, Jackson amesema taarifa za kuwepo vitendo vya ufisadi katika mradi huo na hasa kufujwa kwa mamilioni ya fedha za ujenzi zilizotolewa na serikali zilikuwa hazimjamfikia hivyo ameanza kufuatilia.

"Ni Zahanati, sikuwa na taarifa ndiyo kwanza nazipata. Nipe muda nakutana na watu sasa hivi nikimalizana nao naanza kufuatilia madai ya tuhuma hizo," alisema Jackson.

Inadaiwa kuwa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Ntope ulianza mwaka 2003 lakini mpaka leo haujamalizika.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zimedai kuwa mwaka 2003 serikali ilitoa shilingi milioni 60 za ujenzi wa zahanati hiyo ambapo zilitumika sh milioni 20 kujenga msingi na kupandisha matofali machache kabla ya kudaiwa kuwa sh milioni 40 zimepotea.

Aidha, taarifa nyingine zimedai kuwa fedha hizo sh milioni 40 zilizokuwa zimesalia kwa ajili ya kukamilimisha ujenzi huo zilitolewa kwa mkopo zikawekwa kwenye mfuko mwingine wa kijiji lakini hazijarejeshwa hadi sasa hivyo kukamwisha ujenzi.

Imedaiwa zaidi kuwa licha ya zahanati hiyo kutokamilika kujengwa, imekuwa ikipatiwa mgawo wa dawa ambazo haijulikani zimekuwa zikipelekwa kwenye hospitali gani.

 

AJIRA ZAIDI YA 2,000 ZAPATIKANA WILAYA YA SIHA MKOANI KILIMANJARO



NA PIUS NTIGA, SIHA

 ZAIDI ya ajira 2,000 zimepatikana Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha miaka mitano.

 Nyingi kati ya ajira hizo zinahusisha miradi mbalimbali ukiwemo mradi mkubwa wa Shamba la Mwekezaji la Maparachichi unaojulikana kwa jina la Africado ambalo limetoa nafasi za kazi kwa wananchi wengi wilayani Siha.

 Sambamba na mradi huo mkubwa wa Africado uliopo Kijiji cha Kifufu, mradi mwingine mkubwa ulitoa ajira nyingi kwa wananchi wa Siha ni shamba la uzalishaji Mayai ya kisasa lenye ukubwa wa hekari 507 lililopo Kijiji cha Namwai ambalo mwekezaji wake ni Irvine Family. Miradi hii imezalisha ajira zaidi ya 700 Kati ya 2,000 za wananchi kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.

 Akizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM ikilenga kuainisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, 

Meneja Utawala wa Shamba la Africado, Berinda Meena amesema shamba hilo limesaidia kupatikana kwa ajira 500 za wananchi wa Siha zilizowawezesha kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.

 Amesema mbali ya kufanisha utoaji wa ajira kwa mamia ya wananchi wa Siha, shamba hilo la Africado lenye uwekezaji wa mabilioni ya shilingi linawasaidia wafanyakazi wake kuwajengewa uwezo wa ujuzi wa kilimo kwa kufunga vikonyo,  ambapo sehemu kubwa ya wafanyakazi wana mashamba yao binasfi.

 Meena amesema wafanyakazi pia wanapatiwa pembejeo bure na mwekezaji na mazao yao wanayauza kwa mwekezaji - Africado lengo likiwa kuwawezesha kuwa na soko la uhakika.

 po Mwekezaji wake ni James Pasoz raia wa Ujerumani.

 "Tangu Mwekezaji huyu, James Pasoz ambaye ni raia wa Ujerumani awekeze katika shamba hili sasa yapata miaka 10 anazalisha maparachichi na kuyauza Ulaya na Uarabuni.

 "Mwaka huu zaidi ya tani 3,600 zimezalishwa katika shamba hili na kuuzwa nje ya nchi.

 'Maandalizi ya shamba la Maparachichi ni miaka mitatu kuanzia hatua ya kupanda miche hadi kuvuna kwa kutumia mbegu ya hasi inayokuwa haraka" alisema Meena.

 Aidha, amesema serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa kutoa leseni kupitia EPZ na msamaha wa kodi na kuwezesha eneo kubwa kwa kuweka mtaji mkubwa na hivyo ameipongeza serikali kwa kusamehe kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vitu ambavyo mwekezaji ananunua kwa ajili ya shamba hilo.

 Meena alisifu uhusiano mzuri baina ya mwekezaji na serikali ambao umewezesha shughuli za uzalishaji kuwa kutokwama.

 "Mazingira ya uwekezaji sasa ni mazuri kwa kiasi kikubwa, yamekuwa mazingira yanayosaidia kampuni kukuwa kwa kiasi kikubwa.

 "Kwa sababu ya kuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji, mwekezaji sasa anatafuta maeneo mengine ya kuwekeza zaidi wilayani Siha.

 "Shamba hilo limekuwa na msaada mkubwa kwani kipato kinachopatikana  kimekuwa kikisaidia kukuza uchumi wa wananchi pamoja na kujenga shule ya msingi Karagoha na kutoa kampeni ya matibabu bure ya macho," amesema Meena.

 Wakati huo huo, Meneja Mwendeshaji wa Shamba la Mayai ya Kisasa la Joseph Kasegama, amesema shamba hilo limeondoa upungufu wa upatikanaji wa vifaranga vya Kuku na limesaidia upatikanaji wa ajira 120 kwa wananchi wa Siha na kuongeza pia mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha.

 "Shamba hilo la Irvine Family lenye hekari 507 lina Mabanda 507 yenye uwezo wa kuchukua kuku 9,000," amesema.

 Naye Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo katika wilaya hiyo ambazo zimewezesha kukarabati pia Hospitali ya Wilaya ya Siha.

 "Tumepata fedha, fedha hizo zimesaidia kukabarati  Hospitali ya Kibong'oto inayotibu wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB), shilingi bilioni saba zimepelekwa pale huku Hospitali ya Wilaya ya Siha ikipokea shilingi bilioni mbili zilizofanya ukarabati mkubwa," alisema.

 Aidha, amesema zaidi ya shilingi bilioni 50 zimetumika kujenga barabara za lami wilayani humo sanjari na kurahisisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

 "Mpango wa elimu bure umesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi na sekondari wakiwemo jamii ya wamasai.

 "Ni kwamba ukanda wa Kasikazini haujasaulika ni tofauti kabisa na ambavyo imekuwa ikisemwa kuwa ukanda huu umesahaurika kitu ambacho sio kweli," anasema Buswelu ambaye kauli yake inaungwa mkono Katibu Tawala wa Wilaya, Joseph Mabiti.

 Kuhusu uhusiano na wawekezaji amesema ni mzuri na hivyo kuwataka watu kupuuza kauli zinazotolewa kuwa hakuna uhusiano mzuri baina ya serikali na wawekezaji.

 


Akizungumzia Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea, Buswelu,  amewataka wanasiasa kunadi sera zao kwa utulivu na kuache mihemuko.

 Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutekeleza haki yao ya msingi kwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu wakachague viongozi watakaowaletea  maendeleo ya haraka.

 Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, Dk. Andrew Method, amesema hivi karibuni mashine ya X-ray itafungwa na hivyo kupunguza changamoto ya wanachi kwenda kutafuta huduma ya vipimo KCMC pamoja na Hospitali ya Mawenzi ya Mjini Moshi.

 Aidha Hospitali hiyo ndani ya wiki chache zijazo majengo ya huduma na mama na mtoto yataanza kutumika, ambapo katika Hospitali hiyo vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua hadi  kifo kimoja kwa mwaka.

 Aidha, Dk Method amesema hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kuwa na jengo la kisasa la kuhifadhi miili 20 ya marehemu kwa wakati mmoja.

 Pia amesema ndani ya miezi mitatu ijayo Hospitali hiyo ya Siha itapokea kiasi kikubwa cha dawa ambacho kitatoshereza hospitali hiyo na hata kuzidawa katika vituo vingine vya Afya nje ya Wilaya hiyo.

 Nao wananchi pamoja na watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, wamepongeza uboreshaji wa Hospitali hiyo ambayo inatoa huduma kubwa za kibingwa ambazo walikuwa wakizipata nje ya Wilaya hiyo ya Siha.

 Mwisho

RORYA YAMWANGIWA BILIONI 5.8 ZA ELIMU BILA MALIPO




NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imetoa shilingi bilioni 5.8 kwa shule 151 za Wilaya ya Rorya mkoani Mara kwa ajili ya kugharamia mpango wa elimu bila malipo unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarani mwaka 2015.

Fedha hizi zimenufaisha shule za sekondari 31 na za msingj 120.

Akizungumza na wananchi wa Shirati kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mpira Obwere, Kata ya Mkoma, Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara, Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema sh. bilioni 3.3 zilitolewa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli kwa ajili ya shule za msingi 120.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya ukarabati, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maafisa elimu kata na walimu wakuu.

Alisema kwa shule za sekondar 31, Serikali ya Rais Magufuli ilitoa sh bilioni 2.5 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali kupitia mpango wa lipa kutokana na matokeo (EP4R)  pia ilitoa sh bilioni 1.2 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule ambayo ni pamoja na ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za walimu kwa shule za msingi.

Alizitaja baadhi ya shule za msingi zilizonufaika na mpango huo kuwa ni Mori, Nyanduga, Buchuri, Kondo, Saye, Masonga, Kyaro, Kitembe, Bubombi, Oliyo B, Dagopa, Nyabi, Ratia, Kotwo, Muchirobi, Manyara, Ochuna na Nuamaguku.

" Kwa upande wa shule za sekondari zimetumika sh milioni 777.8 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo maabara, madarasa, mabweni na vyoo kwa shule za Bukama, Mirage, Ngasaro, Nyamunga, Buturi, Goribe, Nyathorogo, Nyamtinga na Waningo.

Waziri Mkuu Majaliwa yupo Mkoa wa Mara akifanya kampeni za kumuombea kura mgombea urais wa CCM, Rais John Pombe Magufuli na aliitumia fursa ya mkutano huo kuwaombea kura mgombea ubunge wa Jumbo la Rorya, Jafari Chege, mgombea udiwani wa Kata ya Mkoma, Ayoi Mussa Sonde na madiwani wengine wa wilaya hiyo.

SERIKALI YATUMIA BILIONI 25 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA MANISPAA MUSOMA

 


WAZIRI MKUU, KASSIN MAJALIWA AKIWAHUTUBIA WANANCHI WA MUSOMA MJINI

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imetumia shilingi bilioni 25 kujenga na kukarabati barabarani na mitaa ya Manispaa ya Mji wa Musoma, Mkoa wa Mara.

Sambamba na hilo, Serikali pia imeweka taa za barabarani urefu wa kilomita 14 kupitia programu ya uboreshaji wa Miji (ULGSP) katika manispaa hiyo.

Hayo yameelezwa Septemba 21, 2020 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa katika hotuba yake ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais John Pombe Magufuli.

Katika hotuba yake hiyo kwa wakazi wa Mji wa Musoma  aliyoitoa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mara iliyo Kata ya Nyamatare, Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu alisema hatua chanya zilizokwishachukuliwa ya serikali tangu mwaka 2015 ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema ni lengo la serikali kuifanya miji yote ya Tanzania ukiwemo wa Musoma, usiku uwe mchana na mchana uendelee kuwa mchana.

"Shilingi bilioni 18.7 zimetumika kujenga kilomita 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani kupitia programu ya uboreshaji wa miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na mradi umekamilika. Tunataka taa ziwake ili usiku uwe mchana na mchana uwe mchana.

" Kupitia Road Fund maintenance, kiasi kingine cha shilingi bilioni 6.6 kilitumika kwa ajili ya kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na miradi yote imekamilika.

"Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura Dk. John Pombe Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia miradi mingine iliyotekelezwa na serikali katika uhai wa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano, Waziri Mkuu Majaliwa alitaja uboreshaji wa huduma za upatikanaji maji katika Manispaa ya Musoma.

"Ili kuboresha huduma ya upatikanaji maji katika Manispaa ya Mji wa Musoma, shilingi bilioni 46 zilitolewa na serikali kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi wa Manispaa ya Mji wa Musoma ambao tayari umeanza kutoa huduma.

" Shilingi bilioni 18 zimetolewa kwa ajili ya mradi wa kusambaza maji Manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya Musoma Vijijini na Butiama. Kazi zinazofanywa sasa ni ujenzi wa tenki la Bharima lenye ujazo wa lita milioni tatu, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na ulazaji bomba la kusafirisha maji kwenda tenki la Bharima lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 1.56, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alitaja kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka tenki la Bharima kwenda kwenye kaya za wananchi lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7,058, ufungaji wa pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa, ununuzi  wa bomba za kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.