banner

Friday, November 20, 2020

MSAKO WA LABNA WA ST MARY'S WAIBUA MADUDU YA KUTISHA, SHAMBA LA BANGI LABAINIKA NYUMBANI KWA KAMISHNA

 


NA MWANDISHI WETU

TIMU ya maafisa wanne waandamizi wa serikali iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kumsaka mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's, aliyepotea tangu Oktoba 4, 2020 imebaini kuwa shule hiyo imepungukiwa sifa zinazostahili kisheria.

Afisa Elimu Sekondari ya Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere ameyasema hayo alipokuwa akielezea mwenendo wa msako na uchunguzi wa mazingira ya kutoweka kwa mwanafunzi Labna unaofanywa na timu iliyoundwa na Chongolo.



Kapere alisema katika uchunguzi huo ulioanza jana  kwa kumuhoji Mkuu wa Shule ambaye alieleza kuwa Labna aliwaambia walimu hataki shule na alitoroka akaenda kwa rafiki yake ya kiume wakawa wanaishi pamoja.

"Tunafanya uchunguzi kwa umakini sana. Tumeishamuhoji Mkuu wa Shule na yeye ametueleza kuwa huyo mtoto alikwishawambia walimu kuwa hataki shule na aliondoka shuleni kwa kutoroka.

"Mkuu wa Shule alituambia kuwa motto alitoroka shuleni kwa kuruka ukuta usiku akisaidiwa na wanafunzi wenzake wavulana wawili, akaenda kwa boy friend wake wakaanza kuishi pamoja huko,” Kapere alimkariri mkuu wa shule.

Alisema mkuu huyo wa shule aliipeleka timu ya serikali nyumba aliyokuwa akiishi Labna na mpenzi wake baada ya kutoroka shule lakini waliwakosa na badala yake walikuta wavulana saba wakiwa wanavuta bangi.

"Mkuu wa shule anapajua alipotorokea mtoto huyo na alitupeleka kwenye hiyo nyumba. Ni nyumba ya Kamishna Mstaafu wa Magereza ambayo wanaishi watoto wake wawili lakini hapo hatukumta Labna wala boy friend wake, tulikuta vijana saba waliokuwa wanavuta bangi na nyumba nzima ilikuwa imetapakaa misokoto ya bangi.

"Kwa kweli ni hali ya kutisha sana kwa vijana wetu. Walituambia ni kweli Labna alipotoroka shule alikuwa akiishi hapo na boy friend wake na alikuwa mama wa nyumbani kwani alikuwa akiwapikia na kufanya usafi wa nyumba lakini baada ya muda kidogo aliondoka.

"Boy friend wake naye hatukumkuta, wale vijana wavuta bangi walisema anasoma chuo CBE na anaishi hostel sasa tumepeleka makachero akakamatwe huko.

“Lakini hiyo nyumba baada ya kuichunguza kwa sababu ina uzio mkubwa sana tulikuta shamba la bangi humo ndani. Yaani bangi inalimwa humo humo nyumbani kwa Kamishna wa Magereza wanavuna wanavuta hao vijana.

"Basi wale vijana tuliwachukua hadi polisi wamelala huko kwa ajili ya uchunguzi zaidi na taratibu nyingine zitafuata," alisema Kapere.

Alipoulizwa iwapo timu hiyo imebaini ni kwanini Mkuu wa Shule baada ya kuambiwa na Labna kuwa hataki shule hakuwapa taarifa wazazi na hata alipotoroka uongozi wa shule ulikaa kimywa wala haukutoa ripoti polisi, alisema mwalimu huyo amekiri kuwa yeye na wenzake walikosea.

Tanzania PANORAMA lilimuuliza pia Kapere kama timu ya serikali imebaini ni kwanini Mkuu wa Shule baada ya kubaini mwanafunzi wake ametoroka na alikuwa akiishi na mwanaume nje ya shule hakuchukua hatua za kutoa taarifa kwa wazazi na polisi ili wote wawili wakamatwe kwa kuzingatia mwanafunzi huyo wazazi wake walimkabidhi kwa uongozi wa shule, Kapere alisema swali hilo ni zuri na watamuuliza Mkuu wa Shule.

"Timu yetu ina polisi, hata nyumba ya  kamishna tuliivamia tukiwa na polisi. Polisi waliizingira kisha wakaingia ndani ndiyo wakakuta lile shamba la bangi na ile misokoto. Lakini Mwalimu anajitetea yeye ni mgemi na tabia ya watoto kutoroka usiku wakarudi alfajili aliikuta. Lakini pia mkuu wa shule alituambia kuwa awali yeye, polisi na wajomba wa huyo wa mtoto walikwenda hadi kwenye hiyo nyumba kumsaka lakini polisi na wajombe hawakuingia ndani, waliishia nje.  

"Sasa hata Labna alipotoroka Mwalimu amesema mwenyewe alijua ndiyo kawaida yao atarudu lakini kwa bahati mbaya yeye hakurudi, akahamia kabisa kwa huyo boy friend wake.

"Uchunguzi wetu sasa pale shuleni imebaini kuwa ile shule haifai, imepungukiwa sifa stahiki za kuitwa shule. Kwanza ni chafu sana, haina walinzi wa kutosha na hata ukuta wake haufai," alisema Kapere.

Alisema anaamini mtoto huyo yupo hai na atapatikana katika msako unaoendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo alipoulizwa jana alisema yupo msibani hivyo hayupo katika nafasi kuzungumza.

Labna, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde Jijini Dar es Salaam alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 lakini tukio  la kutoweka kwake halikuripotiwa polisi na uongozi wa shule.

SERIKALI YAANZA MSAKO MKALI MWANAFUNZI ALIYEPOTEA ST MARY'S

 

NA MWANDISHI WETU

HATIMAYE serikali imeanzisha msako mkali wa mwanafunzi Labna Salim Said wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary's ambaye amepotea tangu Oktoba 4, 2020 akiwa shuleni.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimeeeza kuwa, msako huo umeanza jana baada ya kufanyika kwa kikao cha ulinzi na usalama cha Wilaya ya Kinondoni kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Daniel Chongolo.

Chongolo ameithibitishia Tanzania PANORAMA  kuitisha na kuongoza kikao hicho na kueleza kuwa serikali imeanza kuchunguza mazingira ya tukio la kupotea kwa mwanafunzi huyo akiwa shuleni kwa kuunda kikosi maalumu kinachojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama.

Hata hivyo, Chongolo alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kulizunguzia suala hilo kwa sababu kuhofia kuharibu mwenendo wa uchunguzi wa timu yake aliyoiunda.

Akizungumzia hatua hiyo ya serikali kujitosa rasmi kwenye sakata la kupotea kwa mwanafunz Labna, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere Chongolo aliitisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ofisini kwake jana mchana baada ya kupokea malalamiko ya wazazi wa mtoto huyo kupotea akiwa shuleni.

Kapere alisema katika kikao hicho kilichohudhuliwa pia na wazazi wa mtoto huyo, Chongolo aliunda kamati ya watu  wanne kumsaka mtoto Labna popote alipo na kuchunguza mwenendo mzima wa tukio la  kupotea kwake.

"Hili tukio ni la aina yake lakini tunasikitika kuwa limechelewa kutufikia, hata mkuu wa wilaya kafahamu jana baada ya wazazi kumfikishia kesi hiyo. Hizo shule zipo chini yangu mimi ndiyo nashughulika nazo.

"Sasa mkuu wa wilaya aliitisha kamati ya ulinzi ya usalama na ameteua kikosi cha watu wanne kumsaka mtoto huyo.

"Walioteuliwa kwenye kikosi hicho ni viongozi waandamizi wakiwemo kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ofisi ya Afisa Usalama wa Wilaya ya Kinondoni, mimi mwenyewe Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kinondoni," alisema Kapere.

Mwanafunzi msichana, Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s alitoroka shuleni usiku na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana.

Labna alitoroka Oktoba 4, 2020 akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kupotea kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.

Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kupotea kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.

 

Thursday, November 19, 2020

FISI MADOA MNYAMA ANAYEWEKA MIPAKA YA HIMAYA YAKE KWA KINYESI CHAKE


 NA ERNEST SITTA

MAISHA ya mnyama Fisi yana mengi ya kuvutia kuyajua ambayo yanamsaidia binadamu kutambua umuhimu wa mnyama huyu katika uso wa dunia.

Fisi wamegawanyika katika makundi manne ambayo ni Fisi Madoa, Fisi Miraba, Fisi Kahawia na Fisi Aardwolf na asili yao ni familia inayofahamika kwa jina la kitaalamu la Hyenidae.

Taungalie kwanza maisha ya Fisi Madoa, mnyama anayetokea kwenye familia ya Hyenidae.

Kwa kawaida Fisi wote ni wanyama wanatokea katika kundi la wanyama walao nyama.

Fisi madoa ana urefu wa sentimita 77 kutoka mkiani hadi kwenye mabega akiwa amesimama.

Uzito wake ni kilo 63 kwa dume na jike ni kilo 68, hivyo jike ni mkubwa kuliko dume.



Fisi madoa anabeba mimba kwa muda wa miezi mitatu na nusu na huzaa watoto kuanzia mmoja mpaka wanne. Umri wake wa kuishi ni miaka 50.

Aina hii ya wanyama wanapendelea kukaa kwenye mashimo au mapango katika familia inayoongozwa na mtawala ambaye ni jike na kufuatiwa na majike daraja mbalimbali za utawala katika familia.

Sehemu hizo za mapangoni hutumika kuishi na kulea watoto wa rika mbalimbali. Jinsia ya kike hukaa katika himaya waliyozaliwa maisha yao yote lakini Fisi madume baada ya kufikia miaka minne huanza kujiandaa kuondoka kwenye familia.

Fisi madume baada ya kutimiza miaka minne hutoka na kujiunga na familia nyingine.

Fisi hawa huweka mipaka ya himaya yake kwa kutumia utomvu wenye harufu kali kutoka kwenye tezi lililomo ndani ya sehemu ya kujisaidia haja kubwa.



Mnyama huyu ni mahiri wa kuwinda, ana uvumilivu na nguvu nyingi za shingo. Umbo la fuvu la kichwa lina meno makali yenye uwezo wa kutafuna hata mifupa.

Kinyesi cha Fisi Madoa kina rangi nyeupe kama chaki au chokaa.

 Jike mtawala pamoja na watoto wake humiliki himaya na chochote kilichopo ndani ya eneo kama ni mnyama wameshirikiana kuua ndani ya himaya wa kwanza kula ni jike mtawala pamoja watoto wake, wakishatosheka ndipo Fisi wengine watafuatia kwa kuzingatia daraja mbalimbali au rika.

Chakula kisipotosha familia nzima ya Fisi wawindaji au wavizia mizoga husafiri kwenda mbali muda wa siku moja au mbili kutafuta chakula kingine cha kutosheleza kundi zima na kurudi kuwatapikia watoto wao.



Watoto wa Fisi Madoa waliozaliwa na jike mtawala wanakuwa na bahati ya kuendelea kutawala, vivyo hivyo wanaozaliwa na mama ambaye yupo daraja la chini huendelea  kutawaliwa na hawapewi kipaumbele hasa katika masuala ya chakula.

Katika jamii zetu za kiafrika hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Fisi huhusishwa na imani za kishirikina na hasa wanaposikika kwa milio tofauti karibia na mazingira ya makazi ya watu.

Lakini kiuhalisia sauti za Fisi huashiria  kuomba msaada endapo mmoja ameona mawindo, mzoga au msaada kama kuna adui.

Fisi ni muhimu sana katika mapori tengefu na hifadhi za taifa. Mfano katika  mfumo wa kiikolojia wa Serengeti-Maasai Mara Kenya unajumuisha wanyama mbalimbali wakiwemo wanyama wahamiaji - Nyumbu zaidi ya milioni mbili ambao kila mwaka wanahama kutoka sehemu wanapozaa na kuenda sehemu wasipozaa kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa, kutafuta chakula, mazingira na maji.

Fisi Madoa na jamii nyingine za Fisi huitwa bwana afya katika hifadhi kwa sababu ya kula idadi kubwa ya mizoga ingawa kuna wanyama wengine kama Simba, Chui, Mbweha na ndege aina ya Tumbusi ambao nao hula mizoga hiyo.

Hivyo bila Fsi kula mizoga hiyo kwa idadi kubwa, hifadhi zingekuwa zinanuka na kukatisha wageni kuzitembelea jambo ambalo lingechangia kupoteza mapato yatokanayo na utalii.

ERNEST SITTA NI MTAALAMU WA ELIMU YA WANYAMA NA MIMEA AMBAYE AMEFANYA KAZI NA TAFITI MBALIMBALI KATIKA HIFADHI TOFAUTI TOFAUTI HAPA NCHINI KWA ZAIDI YA MIAKA 10

DSTV YAJA NA OFA KABAMBE YA MSIMU WA SIKUKUU

 



NA MWANDISHI MAALUM

KATIKA kunogesha zaidi msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka na mwaka mpya, Kampuni ya MultiChoice Tanzania imetangaza ofa kabambe kwa wateja wapya wa DStv yenye lengo la kuhakikisha Watanzania wengi wanapata huduma hiyo ili waweze kufurahia burudani, elimu na habari wao na familia zao msimu huu wa sikukuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya DStv ya msimu wa sikukuu iliyopewa jina la ‘Vibe la sikukuu na DStv kama DStv’, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania, Ronald Shelukindo amesema kama ilivyo ada kwa DStv, kila unapofika msimu wa sikukuu hutoa ofa maalum kwa wateja wake ili kuwapa uhakika wa kupata huduma za DStv kipindi cha sikukuu na watu wengi wakiwemo watoto huwa likizo hivyo kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa burudani nyumbani.

Akifafanua, Shelukindo amesema kampeni ya msimu wa sikukuu DStv hutoa ofa maalum kwa wateja wake.

“Kwa wale ambao bado hawajajiunga na DStv, huu ndio wakati muafaka kwani kuna ofa maalum ya kujiunga ambapo mteja ataunganishwa na DStv kwa Sh,79,000 tu na zawadi ya kifurushi cha Family mwezi mmoja bila malipo” alisema Shelukindo.

Alisema ofa hii inawapa uhakika wateja wapya kufurahia maudhui motomoto ndani ya DStv na itadumu hadi mwisho wa mwezi Desemba 2020.


Mkuu wa Mauzo wa MultiChoice Tanzania, Salum Salum akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msimu wa sikukuu ambapo DStv imetangaza ofa kabambe kwa wateja wake


Akifafanua zaidi kuhusu ofa hiyo alisema inapatikana nchi nzima kwa mawakala wa DStv hivyo mteja atapata ofa hii na huduma ya kufungiwa DStv popote alipo kwa urahisi na haraka.

“Tunafahamu kuwa kipindi hiki cha sikukuu watu wengi husafiri kuungana na familia zao maeneo mbalimbali mijini na vijijini na kwa kulitambua hili tumejipanga kuhakikisha huduma zetu zinapatikana kirahisi kila mahali”

Amewashauri wateja wote ambao wanahitaji huduma za DStv, mbali na kwenda kwenye vituo au mawakala wa DStv, wanaweza pia kupata huduma hiyo kwa kupiga simu 0659070707 au kwa kutembelea kurasa za DStv Tanzania za mitandao ya kijamii Instagram @dstvtanzania, Twitter @DStv_Tz na Facebook @DStv(tz) ambapo wanaweza kupata huduma mbalimbali za DStv kama vile kuunganishwa, kulipia vifurushi, kubadili kifurushi na huduma nyinginezo.

Kwa wateja wa DStv, Salum amesema wataendelea kupata maudhui kemkem kuanzia michezo, burudani, vipindi vya elimu, chaneli za watoto, sinema na tamthilia za ndani na nje bila kusahau chaneli za habari zitakazowahakikishia taarifa mbalimbali kutoka pande zote za dunia.

Kwa wale wanaosafiri, amewakumbusha kupakua App ya DStv Now inayowawezesha kuendelea kufurahia huduma za DStv kwenye vifaa mbalimbali kama simu janja bila gharama yaziada.

“Kwa wale wanaosafiri na wangehitaji kuendelea kuburudika na DStv, ni vyema wakatumua huduma yetu ya DStv Now kwa kupakua app yetu na hivyo kuweza kutumia akaunti zao katika vifaa zaidi ya vine popote walipo nchini bila kulazimika kulipia malipo yoyote ya ziada” alisisitiza Salum



Waigizaji maarufu katika tamthilia ya Karma Ford (kulia) na Misa (Katikati) wakiwa pamoja na maafisa wa DStv Tanzania – Mkuu wa Masoko Ronald Shelukindo (wa pili kulia), Mkuu wa Mauzo Salum Salum (wa pili kushoto) na Afisa Uhusiano wa kampuni hiyo Grace Mgaya (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msimu wa sikukuu

 Hafla ya kuzindua kampeni hiyo ya DStv ilihudhuriwa na baadhi ya wasanii maarufu wa Bongo Movie wanaoigiza katika tamthilia na filamu mbalimbali zinazoonyeshwa kwenye chaneli ya Maisha Magic Bongo ndani ya DStv akiwemo kinara wa tamthilia maarufu ya Karma Wema Sepetu.

 

 

Wednesday, November 18, 2020

WAFANYAKAZI MR CLEAN WAMLILIA JPM

 


NA MWANDISHI WETU

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya udobi ya Mr Clean ya jijini Dar es Salaam wamemuomba Rais John Magufuli atakapoteua Baraza la Mawaziri, amuelekeze Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira kutafuta suluhu ya kudumu kwa watanzania wanaofanyishwa kazi muda mrefu bila kupewa mikataba ya kazi.

Wakizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni kuhusu kutopatiwa mikataba ya kazi na mwajiri wao kwa muda mrefu, walisema wao ni sehemu tu ya watanzania wengi wanaonyanyasika sehemu za kazi na wameamua kupaza sauti zao ili Rais ambaye amekuwa akiwatetea wanyonge awasikie.

"Tunaamini Rais akisikia kilio chetu atatusidia kutatua hii kero yetu. Sisi tumefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa katika Kampuni ya Udobi ya Mr Clean lakini mwajiri wetu hajatupa mikataba ya kazi. Kila tukiomba anatishia kutufukuza kazi.

"Tunapenda kufanya kazi kwa sababu bila kazi kwa maisha ya sasa mtu unakufa njaa na tunafurahi wanapojitokeza wawekezaji na wafanyabiashara wenye makampuni wanaotoa nafasi za kazi lakini mazingira ya kazi ni magumu mno.

"Mtu unakuwa kibarua mwaka mzima, miaka miwili, kazi yenyewe ngumu maana tunafua nguo kwa madawa ambayo hatujui yana kemikali za aina gani. Matokeo yake ukiugua unaondolewa kazini.

"Hatuna pensheni ya aina yoyote, hatuna Bima ya Afya, tunafua nguo kwa kutumia madawa, tunalipwa mkononi kama vibarua serikali haipati kodi yoyote ambayo ingetokana na mishahara yetu. Tunaomba kilio chetu kimfikie rais atuletee waziri wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu wafanyakazi wa sekta binafsi," alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr Clean, Ravi Shankar kuhusu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema suala hilo aulizwe msemaji wa Kampuni yake aliyemtaja kwa jina la Morris Ngonyani.

 

Alipoulizwa Ngonyani alisema yeye siyo msemaji wa kampuni ya Mr Clean bali mwenye Kampuni akiwa na hisa asilimia 90 na huyo alielekeza aulizwe ni mfanyakazi wake ambaye hana ruhusa ya kuzungumza lolote kwa sababu amemuweka kiwandani hapo kama msimamizi wa wafanyakazi tu.

Akijibu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema walikuwa vibarua ambao kwa sasa wameishaondolewa kazini na kwamba Kampuni ya Mr Clean imebaki na wafanyakazi saba tu nchi nzima kutokana na mwenendo mgumu wa biashara.