NA MWANDISHI WETU
WAFANYAKAZI wa Kampuni ya udobi ya Mr Clean ya jijini Dar
es Salaam wamemuomba Rais John Magufuli atakapoteua Baraza la Mawaziri,
amuelekeze Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira kutafuta suluhu ya kudumu kwa
watanzania wanaofanyishwa kazi muda mrefu bila kupewa mikataba ya kazi.
Wakizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni kuhusu
kutopatiwa mikataba ya kazi na mwajiri wao kwa muda mrefu, walisema wao ni
sehemu tu ya watanzania wengi wanaonyanyasika sehemu za kazi na wameamua kupaza
sauti zao ili Rais ambaye amekuwa akiwatetea wanyonge awasikie.
"Tunaamini Rais akisikia kilio chetu atatusidia
kutatua hii kero yetu. Sisi tumefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa katika
Kampuni ya Udobi ya Mr Clean lakini mwajiri wetu hajatupa mikataba ya kazi.
Kila tukiomba anatishia kutufukuza kazi.
"Tunapenda kufanya kazi kwa sababu bila kazi kwa
maisha ya sasa mtu unakufa njaa na tunafurahi wanapojitokeza wawekezaji na
wafanyabiashara wenye makampuni wanaotoa nafasi za kazi lakini mazingira ya
kazi ni magumu mno.
"Mtu unakuwa kibarua mwaka mzima, miaka miwili, kazi
yenyewe ngumu maana tunafua nguo kwa madawa ambayo hatujui yana kemikali za
aina gani. Matokeo yake ukiugua unaondolewa kazini.
"Hatuna pensheni ya aina yoyote, hatuna Bima ya Afya,
tunafua nguo kwa kutumia madawa, tunalipwa mkononi kama vibarua serikali
haipati kodi yoyote ambayo ingetokana na mishahara yetu. Tunaomba kilio chetu
kimfikie rais atuletee waziri wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu wafanyakazi
wa sekta binafsi," alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr Clean, Ravi Shankar
kuhusu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema suala hilo aulizwe msemaji wa
Kampuni yake aliyemtaja kwa jina la Morris Ngonyani.
Alipoulizwa Ngonyani alisema yeye siyo msemaji wa kampuni
ya Mr Clean bali mwenye Kampuni akiwa na hisa asilimia 90 na huyo alielekeza
aulizwe ni mfanyakazi wake ambaye hana ruhusa ya kuzungumza lolote kwa sababu amemuweka
kiwandani hapo kama msimamizi wa wafanyakazi tu.
Akijibu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema walikuwa
vibarua ambao kwa sasa wameishaondolewa kazini na kwamba Kampuni ya Mr Clean
imebaki na wafanyakazi saba tu nchi nzima kutokana na mwenendo mgumu wa
biashara.
No comments:
Post a Comment