NA CHARLES MULLINDA
WANAFUNZI wasichana wa Shule ya Sekondari ya St.
Mary’s iliyoko Mbezi Makonde Jijini Dar es Salaam wametoroka shuleni usiku
kwenda mahali kusikojulikana huku mmoja akitoweka moja kwa moja.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA
Blog zimeeleza kuwa wanafunzi hao walitoroka shuleni wakiwa kundi na kurejea
alfajili huko mmoja wao akitokomea mahali kusikojulikana.
Uchunguzi wa Tanzania PANORAMA umebaini kuwa tukio
hilo lilitokea mwezi uliopita na mwanafunzi aliyetoweka anasoma kidato cha tatu
lakini uongozi wa shule na bodi ya shule wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za
kuficha tukio hilo na hajawatoa taarifa polisi za kutoweka kwa mwanafunzi huyo.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Dallas Mhoja
alipoulizwa na Tanzania PANORAMA alisema kupotea kwa mwanafunzi huyo akiwa
shuleni kunamuhusu mkuu wa shule, siyo bodi.
“Wewe vipi bwana, unajua kuwa mimi ni mwenyekiti wa
bodi? Sasa kupotea kwa mwanafunzi kunanihusu nini mimi? Mpigie mkuu wa shule
muulize huyo ndiye anakaa na hao watoto,. Mimi nashughulika na mambo makubwa ya
shule siyo suala na mtoto mmoja kupotea,” alisema Dallas.
Alipoelezwa kuwa taarifa za mwanafunzi kupotea akiwa
mikononi mwa uongozi wa shule na shule kutotoa taarifa polisi kwa zaidi ya
mwezi mmoja ni kubwa ikizingatiwa mpaka sasa hajapatikana alisema akipata
nafasi atafuatilia kwa mwalimu.
Tanzania PANORAMA ilimweleza Mhoja kuwa imefanya
uchunguzi wa kina kuhusu kupotea kwa mwanafunzi huyo na inazo taarifa kuwa
suala hilo limekwishafikishwa kwake lakini hajachukua hatua yoyote alisisitiza
kuwa kwa wadhfa wake wa mwenyekiti wa bodi hastahili kufuatilia mambo ya
wasichana wanaotoroka shule usiku na kupotelea wanakokujua hivyo aulizwe mkuu
wa shule.
“Aisee we mwandishi mbona una maswali ya kuudhi?
Nakwambia hayanihusu mambo wewe umeng’ang’ania kunibana tu unataka nini?
Mwenyekiti wa bodi na kupotea kwa mtoto mmoja wanahusianaje?
“ Mimi ni mwenyekiti wa bodi sihusika na kuangalia
watoto shuleni tena wanaotoroka shuleni usiku kwenda kwenye mambo yao? Halafu
wananogewa huko hawarudi? Muulize mkuu wa shule ndiye anayehusika na malezi ya
watoto,” alisema Mhoja.
Alipotafutwa mkuu wa shule kupitia simu yake ya
kiganjani, iliita bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment