NA ERNEST SITTA
MAISHA ya mnyama Fisi yana
mengi ya kuvutia kuyajua ambayo yanamsaidia binadamu kutambua umuhimu wa mnyama
huyu katika uso wa dunia.
Fisi wamegawanyika katika
makundi manne ambayo ni Fisi Madoa, Fisi Miraba, Fisi Kahawia na Fisi Aardwolf
na asili yao ni familia inayofahamika kwa jina la kitaalamu la Hyenidae.
Taungalie kwanza maisha ya
Fisi Madoa, mnyama anayetokea kwenye familia ya Hyenidae.
Kwa kawaida Fisi wote ni
wanyama wanatokea katika kundi la wanyama walao nyama.
Fisi madoa ana urefu wa
sentimita 77 kutoka mkiani hadi kwenye mabega akiwa amesimama.
Uzito wake ni kilo 63 kwa dume
na jike ni kilo 68, hivyo jike ni mkubwa kuliko dume.
Fisi madoa anabeba mimba kwa
muda wa miezi mitatu na nusu na huzaa watoto kuanzia mmoja mpaka wanne. Umri
wake wa kuishi ni miaka 50.
Aina hii ya wanyama
wanapendelea kukaa kwenye mashimo au mapango katika familia inayoongozwa na
mtawala ambaye ni jike na kufuatiwa na majike daraja mbalimbali za utawala
katika familia.
Sehemu hizo za mapangoni
hutumika kuishi na kulea watoto wa rika mbalimbali. Jinsia ya kike hukaa katika
himaya waliyozaliwa maisha yao yote lakini Fisi madume baada ya kufikia miaka
minne huanza kujiandaa kuondoka kwenye familia.
Fisi madume baada ya kutimiza
miaka minne hutoka na kujiunga na familia nyingine.
Fisi hawa huweka mipaka ya
himaya yake kwa kutumia utomvu wenye harufu kali kutoka kwenye tezi lililomo
ndani ya sehemu ya kujisaidia haja kubwa.
Mnyama huyu ni mahiri wa
kuwinda, ana uvumilivu na nguvu nyingi za shingo. Umbo la fuvu la kichwa lina
meno makali yenye uwezo wa kutafuna hata mifupa.
Kinyesi cha Fisi Madoa kina
rangi nyeupe kama chaki au chokaa.
Chakula kisipotosha familia
nzima ya Fisi wawindaji au wavizia mizoga husafiri kwenda mbali muda wa siku
moja au mbili kutafuta chakula kingine cha kutosheleza kundi zima na kurudi
kuwatapikia watoto wao.
Watoto wa Fisi Madoa
waliozaliwa na jike mtawala wanakuwa na bahati ya kuendelea kutawala, vivyo
hivyo wanaozaliwa na mama ambaye yupo daraja la chini huendelea kutawaliwa na hawapewi kipaumbele hasa katika
masuala ya chakula.
Katika jamii zetu za kiafrika
hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Fisi huhusishwa na imani za kishirikina na
hasa wanaposikika kwa milio tofauti karibia na mazingira ya makazi ya watu.
Lakini kiuhalisia sauti za Fisi
huashiria kuomba msaada endapo mmoja
ameona mawindo, mzoga au msaada kama kuna adui.
Fisi ni muhimu sana katika
mapori tengefu na hifadhi za taifa. Mfano katika mfumo wa kiikolojia wa Serengeti-Maasai Mara
Kenya unajumuisha wanyama mbalimbali wakiwemo wanyama wahamiaji - Nyumbu zaidi
ya milioni mbili ambao kila mwaka wanahama kutoka sehemu wanapozaa na kuenda
sehemu wasipozaa kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa, kutafuta chakula,
mazingira na maji.
Fisi Madoa na jamii nyingine
za Fisi huitwa bwana afya katika hifadhi kwa sababu ya kula idadi kubwa ya
mizoga ingawa kuna wanyama wengine kama Simba, Chui, Mbweha na ndege aina ya
Tumbusi ambao nao hula mizoga hiyo.
Hivyo bila Fsi kula mizoga
hiyo kwa idadi kubwa, hifadhi zingekuwa zinanuka na kukatisha wageni
kuzitembelea jambo ambalo lingechangia kupoteza mapato yatokanayo na utalii.
ERNEST SITTA NI MTAALAMU WA
ELIMU YA WANYAMA NA MIMEA AMBAYE AMEFANYA KAZI NA TAFITI MBALIMBALI KATIKA
HIFADHI TOFAUTI TOFAUTI HAPA NCHINI KWA ZAIDI YA MIAKA 10
No comments:
Post a Comment