banner

Monday, November 2, 2020

WAJANJA DAR WAHAMISHIA MAFICHONI VIWANDA VYA MIFUKO YA PLASTIKI ILIYOPIGWA MARUFUKU

 

 


NA MWANDISHI WETU

IMEBAINIKA kuwa baadhi ya  wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wanaendelea kutengeneza mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na serikali kutokana na kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.

Uchunguzi waTanzania PANORAMA umebaini kuwepo kwa viwanda hivyo katika makazi ya watu yaliyo nje kidogo ya jiji huku ikiwa haina vibali vyovyote vya uzalishaji wa vifungashio.

Aidha, maeneo vilipo viwanda hivyo kuna walinzi ambao hukaa umbali wa hatua 30 hadi 50 ambao kazi yao ni kuangalia kama kuna watu wanaofutilia uzalishaji au kuchunguza eneo la kiwanda kisha hutoa taarifa kwa walio kiwandani kusimamisha uzalishaji na kufunga kiwanda.

Uchunguzi wa kina wa Tanzania PANORAMA umebaini moja ya kiwanda cha mifuko ya plaskiti kipo eneo la Mbezi Kifuru kwa Richard ambacho mmiliki wake hafiki eneo la kiwanda bali ameweka walinzi wanaompatia taarifa za kila mtu anayefika kiwanda hapo kwa kumpigia simu.

Wakizungumza na Tanzania PANORAMA, wafanyakazi wa kiwanda hicho walisema wanajua wanafanya kazi kwa uficho na katika mazingira magumu lakini wanalazimika kufanya kutokana na ugumu wa maisha.

Msimamizi mkuu wa kiwanda hicho ambaye alikataa kujitambulisha jina lake alieleza kuwa kazi yake ni kuangalia usalama na kumpa taarifa bosi wake ambaye pia ni mjomba wake kuhusu wageni wanaofika kiwanda hapo.

“Kiukweli mimi ni msimamizi ila mjomba ndiye anajua kila kitu  mje wakati mwingine atakapokuwa hapa. Najua hatuna vibali na tunaendesha kiwanda kinyume cha taratibu lakini mkiongea na mjomba yeye anajua kila kitu,” alisema.

Mmiliki wa kiwanda hicho aliyefamika kwa jina la Ali Mbonde alipoongea na Tanzania PANORAMA kwa simu alisema anajua kila kitu lakini jambo hilo linahitaji mazungumzo badala ya kuandikwa kwa sababu litasababisha usumbufu usiokuwa wa lazima.

Tanzania PANORAMA inaendelea na uchunguzi wa sakata hili.      

No comments:

Post a Comment