banner

Sunday, November 15, 2020

URAIA WA DIWANI CCM KIVUKONI WAZUA UTATA

 


NA MWANDISHI WETU

Diwani wa Kata ya Kivukoni kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Sharik Choughule anadaiwa kutoa taarifa zisizokuwa sahihi kuhusu uraia wake ili kufanikisha azma yake ya kuwa kiongozi katika chama hicho.

Madai hayo yalianza kusambaa mapema mwezi uliopita lakini jitahada za Tanzania PANORAMA kumfikia kuyazungumzia hazikuweza kufanikiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutingwa na shughuli nyingi za kisiasa.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa kata hiyo aliyefikiwa na Tanzania PANORAMA na kukubali kuzungumza kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa kwa madai kuwa hataki aonekane ana nia mbaya dhidi ya mbio za kusaka uongozi wa kisiasa za Choughule, alisema awali kulikuwa na utata huo lakini ulitatuliwa.

Taarifa zilizokusanywa Tanzania PANORAMA zimeonyesha kuwa Choughule aliingia nchini kwa kutumia hati ya kusafiria ya India akiwa ameambata na ndugu yake wa kiume, ambao walikuja kumtembelea mjomba wao anayefanya biashara jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi umeonyesha kuwa Choughule na ndugu yake walikuja nchini kuonana na mjomba wao aliyekuwa ametwaa mali za baba yao baada ya kufariki dunia.

Washirika wa karibu wa Choughule wamekaririwa kuwa vijana hao wawili walishindwa kuafikiana na mjomba wao ndipo walipogoma kuondoka nchini kurejea India walikokuwa wakiishi na mama yao.

Kwamba ili kuzika mzozo baina yao, mjomba wao aliwaingiza katika moja ya kampuni zake kufanya kazi huku akiwataka wawe na subira ya kutatua utata wa umiliki wa mali hizo.

Imeelezwa kuwa mjomba (jina limehifadhiwa kwa sababu hajapatikana kuzungumza) alitoa taarifa ofisi za uhamiaji kuhusu uwepo wa vijana hao waliokuwa wakiishi nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria na walikamatwa na taratibu za kuwarudisha India zilianza kufanyika.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa vijana hao walilia na kupiga magoti mbele ya mjomba wao wakimuomba azungumze na maofisa wa Uhamiaji ili wasirejeshwe India kwa sababu walikuwa wakiishi maisha ya shida na mama yao baada ya baba yao kufariki na kwamba mjomba wao alikuwa hawatumii fedha kama alivyokuwa akifanya baba yao licha ya kujimilikisha mali zote.

Inadaiwa mjomba wao aliwapa sharti la kutomuuliza tena kuhusu mali alizotwaa kwa marehemu kama wanataka kiendelea kuwepo Tanzania, amri ambayo waliiafiki na yalifanyika mazungumzo wakaachiwa.

Afisa mmoja wa CCM wa Kata ya Kivukoni ambaye jina lake limehifadhiwa ameeleza kuwa ni kweli vijana hao waliingia nchini wakitokea India na kufikia kwa mjomba wao kabla ya kukamatwa na maofisa uhamiaji ambao waliwapakia kwenye ndege na kuwarudisha India ambako walikataliwa kuingia na kurudishwa hapa nchini.

"Ni kweli Choughule alikuja nchini akiwa na mwenzake. Walikuja kwa mjomba wao lakini baadaye kulitoka mtafaruku wakakamatwa na uhamiaji wakapandishwa ndege wakarejeshwa India ambako hawakupokelewa walirudishiwa uwanja wa ndege, wakarejea Tanzania.

"Hakukuwa na namna ikabidi wapokelewe hapa nchini wakarudi tena kuishi na mjomba wao ndipo zikaanza kufanyika taratibu za uraia na uhamiaji iliwasafisha kwa kuwapa uraia wakawa huru kujihusisha na shughuli za kisiasa na mpaka sasa Choughule anaendelea na siasa," alisema.

Choughule amekuwa akikwepa kulizungumzia suala hilo kwa zaidi ya wiki tatu sasa kwani licha ya Tanzania PANORAMA kufika ofisi za CCM Kata ya Kivukoni ambako hakupatikani na kisha kutafutwa kwa simu yake ya kiganjani na kuomba apewe muda kabla ya kuzungumza, hajatekeleza ahadi yake hiyo wala kujibu maswali aliyotumiwa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphery Polepole ambaye alitafutwa kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia suala hilo, simu yake imekuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi kwenye simu yake hakuujibu.

Kwa mujibu wa taratibu za Idara ya Uhamiaji, raia wa kigeni anaweza kupewa uraia kabla ya kuwa na sifa za kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa isipokuwa urais wa Tanzania akiishi nchini kuanzia miaka nane na kufuata taratibu za kuomba uraia ikiwemo muda wote wa kuishi nchini kuwa na kibali.

Tanzania PANORAMA limeperuzi sifa zinazotakiwa kwa wanachama wa CCM kugombea uongozi wa kisiasa ambapo ya kwanza inasomeka awe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment